Ndoa za utotoni zinavyozima ndoto za mabinti Meatu-1

Meatu. Katika mizunguko yangu ndani ya Kijiji cha Nyanza wilayani Meatu, mkoani Simiyu mbele ya nyumba iliyojengwa kwa matofali yasiyochomwa na kuezekwa kwa nyasi, namuona binti aliyeketi juu ya ndoo ya bluu.

Nakaribishwa na binti, ambaye nilimuuliza baba na mama wapo? Akajibu yupo baba, ndipo nilimuomba amuite.

Alifanya hivyo, kisha yeye akabaki ndani. Nilipohoji sababu ya yeye kutorejea, naambiwa kwa jamii ya Wasukuma, hairuhusiwi baba na mke wa mwanawe wa kiume kukaa sehemu moja.

Akili ilifunguka, aliyenikaribisha ni binti aliyefunga ndoa chini ya umri wa miaka 18.

Akiwa na umri wa miaka 17, tayari ni mke wa ndoa inayokaribia mwaka. Aliolewa akiwa na miaka 16, umri ambao alipaswa kuwa chini ya uangalizi wa wazazi na shuleni, lakini sasa ni mke wa kijana mwenye umri wa miaka 18, aliyeoa akiwa na miaka 17.

Familia hii bado ni tegemezi na inahitaji usaidizi wa wazazi. Ndiyo maana bado wanaishi nyumbani kwa wazazi wa mwanamume.

Binti anasema aliolewa baada ya kumaliza darasa la saba, akieleza alikosa nafasi ya kuendelea na kidato cha kwanza.

“Nilimaliza shule mwaka 2023 nikashindwa kuendelea na masomo. Nilikaa nyumbani hadi nilipopata taarifa ya mtu aliyetaka kunioa nikiwa simfahamu. Wazazi walishakubaliana ilibidi kwenda,” anasema.

Anasema halikuwa jambo gumu kwake kwani amekuwa akishuhudia mabinti waliomtangulia wakiolewa wanaposhindwa kuendelea na masomo ya sekondari.

“Hofu yangu ilikuwa namna ya kumudu kuishi na familia ninayokwenda, kwani ni watu nisiowafahamu kwa undani,” anasema.

Katika mazungumzo anaonekana bado hayupo tayari kupata mtoto. “Hee! mtoto kabisa, hapana, siko tayari kwa sasa,” anajibu alipoulizwa iwapo wakwe zake wakitaka mtoto kwa wakati huo.

Binti huyu hana elimu ya afya ya uzazi, hajui kuhesabu siku za mzunguko wake wa hedhi, huku matumizi ya njia nyingine za uzazi wa mpango ikiwamo kondomu yakiwa hafifu kwake.

Mume wa binti huyu, anasema alioa kwa sababu baba yake alitaka hilo lifanyike na alimlipia mahari.

“Sikuona tatizo kwa sababu hapa nyumbani mama yuko peke yake, nilimletea msaidizi na mtu wa kuzungumza naye, pia mtu ambaye anaweza kuangalia nyumba tukienda shambani, atupikie ili sisi tufanye kazi,” anasema kijana huyu mrefu zaidi ya mkewe, mwenye umbo kubwa la mwili lisiloendana na umri wake.

Anasema bado anajifunza vitu kutoka kwa baba yake wanayeishi naye, kwani mkewe ndiye mwanamke wa kwanza katika maisha yake.

Wawili hawa wanawakilisha kundi la vijana wanaooa au kuolewa wakiwa na umri mdogo katika jamii ya Wasukuma na maeneo mbalimbali nchini.

Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa yenye kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni kwa asilimia 34. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za Viashiria vya Malaria na Afya ya Uzazi za mwaka 2015/16. Uko nyuma ya Shinyanga inayoongoza kwa asilimia 59, ukifuatiwa na Tabora (asilimia 58), Mara (asilimia 55) na Dodoma asilimia 51.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo anasema takwimu zinaonyesha wasichana wawili kati ya watano, sawa na asilimia 40 huolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Anasema katika kupambana na tatizo hilo waliunganisha nguvu na mashirika yasiyokuwa ya Serikali.

Anasema: “Kwa mfano, Wilaya ya Maswa iliyo ndani ya Mkoa wa Simiyu, jitihada maalumu zimechukuliwa kukabiliana na ndoa za utotoni kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania. Kampeni ya miaka mitano ilizinduliwa chini ya kaulimbiu: “Mahari kwa mzazi kwa ndoa za utotoni si utajiri.”

Kupitia kampeni hiyo, anasema wasichana 102 waliokuwa wameingia kwenye ndoa za utotoni waliokolewa na kurudishwa shuleni kuendelea na masomo.

Sababu za wazazi

Akizungumza na Mwananchi, baba wa kijana aliyeoa katika umri mdogo kwenye Kijiji cha Nyanza, Meatu, anasema alimwozesha kumsaidia kujikinga na maradhi kwa kumuondolea tamaa za kuwa na wanawake.

Anasema ni kawaida kwa jamii yao, hasa kwa watoto wa kike kuolewa katika umri mdogo ambao bado hawajaharibikiwa na kujua mambo ya dunia.

Dhana hii inathibitishwa na jirani wa familia hii anayesema aliolewa akiwa na miaka 15 mwaka 1998, aliyemuoa akiwa amemzidi miaka mingi.

“Tangu mwaka huo hadi leo niko naye, tuna watoto 10. Niliolewa kwa sababu nilifeli darasa la saba na kukaa nyumbani kwa miaka miwili,” anasimulia.

Anasema kabla ya kuolewa kwa mahari ya ng’ombe 15, wanaume wanne walifika kwao kwa lengo la kumuoa.

Kwa mtazamo wake, binti anapaswa kuolewa kabla hajachezewa, jambo linaloweza kumfanya akose mume na hata kumpa shida katika maisha yake.

Wakati akizungumza na Mwananchi Machi 11, 2025 binti yake wa miaka 16 alikuwa ametoroka.

“Tumeshajua alipo tunasubiri walete ng’ombe, jana usiku (Machi 10) dalili za yeye kutoroka ni kama niliziona kwa sababu alikuwa akifanya vitu ambavyo sivielewi,” anasema.

Matatizo kiafya

Licha ya jamii kuona ni kutu cha kawaida, kuolewa na hatimaye kupata mimba za utotoni kunaweza kuleta matatizo ya kijamii na afya, kama anavyoeleza Dk Medard Ndayanse wa Hospitali ya Wilaya Bagamoyo.

Anasema mtu anapopata mimba akiwa na umri wa chini ya miaka 18 anakuwa hajakomaa kiakili wala via vya uzazi, jambo linaloweza kumpa matatizo wakati na baada ya ujauzito.

“Kina mama wengi ambao wako chini ya miaka 18 wanakuwa katika hatari ya kupata kifafa cha mimba hata kabla ya kujifungua. Pia wanakuwa katika hatari ya kujifungua kabla ya wakati,” anasema na kufafanua kuwa mtoto tumboni anakomaa kati ya wiki 37 hadi 40.

Anasema mabinti hao wapo katika hatari ya kupata watoto wenye uzito mdogo ikilinganishwa na uzito wa kawaida wa kilo 2.5 hadi kilo 3.9.

“Hawa wanakuwa katika hatari ya kupata watoto walio na uzito mdogo, watoto hawa huhitaji uangalizi maalumu, ndiyo maana hulazwa. Hii inaweka urahisi kupata maambukizi,” anasema.

Anasema pia nyonga zao zinakuwa hazijakomaa, jambo linalosababisha washindwe kutanuka vizuri kuruhusu mtoto kupita, hali inayochochea kujifungua kwa upasuaji.

Kwa ambaye hatapasuliwa akabaki na uchungu na mtoto akashindwa kupita, anasema hali hiyo inaweza kumfanya apate fistula.

“Mara nyingi watoto hawa hawajajiandaa kuwa wazazi, kiuchumi na kisaikolojia, wengine wanapata mimba isiyotarajiwa. Hiyo inawafanya kuwa katika hatari ya kupata msongo wa mawazo, kwa sababu wanawaza namna wanavyoweza kukidhi majukumu mapya kama mama, jamii inamtenga, wanamsema na kuongeza hatari ya kupata msongo,” anasema.

Kwa kuolewa katika umri mdogo mwanamke anaweza kupata watoto wengi katika maisha yake, hususani kama atashindwa kufuata njia za uzazi wa mpango.

Kwa jamii ya Wasukuma ni kawaida kukuta mama akiwa na watoto saba na kuendelea.

“Nilijifungua mara 10 lakini watoto walio hai ni wanane. Watatu mpaka sasa wameoa na wengine bado niko nao hapa, wananisaidia shughuli mbalimbali hasa shambani,” anasema Zubeda Mkomi, mkazi wa Kijiji cha Nzasa.

Kuwa na watoto wengi huenda ikawa sababu ya Mkoa wa Simiyu kuongoza kwa kuwa na wategemezi wengi kuliko idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi.

Idadi kubwa ya wategemezi isipodhibitiwa inaweza kuathiri uchumi kutokana na uzalishaji unaofanyika kutoendana na ongezeko la watu linaloshuhudiwa.

Kwa ujumla watu walio na umri wa mwaka 0 hadi 14 wanaongoza kwa kuwa wengi nchini, huku Mkoa wa Simiyu ukiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wategemezi ukifuatiwa na Katavi, Tabora, Geita, Rukwa na Kigoma.

Mikoa hiyo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto walio na umri huo ikilinganishwa na mingine nchini kwa mujibu wa ripoti ya mgawanyo wa idadi ya watu kwa umri na jinsi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Ripoti hiyo inaonyesha idadi ya watu walio chini ya miaka 15 ni asilimia 42.8 ya watu wote waliopo nchini kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Kwa mujibu wa mchanganuo, idadi ya watoto wa umri huo mkoani Simiyu ni asilimia 51.3 ya wakazi wote, Katavi asilimia 50, Rukwa asilimia 49.4, Tabora na Geita asilimia 49 na Kigoma asilimia 48.7.

Akizungumzia uwepo wa watoto wengi, mtaalamu wa uchumi na biashara, Oscar Mkude amesema jambo hilo linafanya watu wachache walio na uwezo wa kutengeneza kipato kuwa na mzigo mkubwa wa kusaidia familia, ikiwamo wanaozaa mapema, majirani na ndugu.

Hali hii anasema inaongeza mzigo kwa Serikali kwani italazimika kutumia nguvu kubwa kuhakikisha huduma za jamii zinafika kwa watu wote ili kuweka usawa, hivyo kufanya fedha nyingi zaidi kutumika.

“Unapokuwa na jamii maskini ni mzigo mkubwa kwa Serikali, lakini ikiwa jamii kubwa yenye kipato kikubwa ni mtaji kwa sababu wanakuwa na uwezo wa kuzalisha na kuuza,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *