
Wengi tumezoea kuwaona wanaume wa Kizungu wakiwafungulia milango wake zao wanapopanda au kushuka kwenye magari hata kuingia majumbani.
Wengi hutafsiri kitendo hiki kama mapenzi ya Kizungu au mapenzi stahiki japo inaweza kuwa zaidi ya haya. Na wanaofanya hivyo si wote.
Wapo Wazungu wenye tabia na matendo kama Waafrika ambao huwa hawawafungulii milango wake zao.
Hata hivyo, visa kama vitatu tulivyoshuhudia si mara moja wala mbili huku tulipo vinasema tofauti. Tunawajua dada zetu weusi ambao wanaweza kuwa wametokea Afrika au Amerika ya Kati walioolewa na wanaume wa Kizungu. Mara nyingi, ukiwaona, hakuna cha baba kumfungulia mama mlango wala kumbebea mikoba kama wafanyavyo waume wa Kizungu kwa wake zao wa Kizungu.
Mwanzoni hatukujali wala kulifuatilia hili. Tukiwa kwenye mkoa tuliofikia, tulikuwa na jirani Mzungu aliyekuwa ameoa mama mweusi, hatujui kama alikuwa akitokea Afrika au Visiwa vya Karibiani.
Wote walikuwa watu wazima kama kwenye miaka 60 na ushei. Kila walipokuwa wakitoka au kurejea nyumbani, kwa mara tulizowaona, utamuona mama amebeba mkoba wake. Cha mno, wakiingia au kushuka kwenye gari, baba hakuhangaika na kukimbia kama wengine wafanyavyo kumfungulia mkewe mlango.
Tulidhani ni hao tu. Baada ya kushuhudia wengine, tulianza kufuatilia na kuja na haya tunayoandika hapa. Kwanza, tulijiuliza ni kwa nini? Mpaka sasa hatujui sababu ya kufanya hivyo japo tunahisi kama kuna chembe za ubaguzi.
Maana, Walter, Mmarekani mweusi aliyeoa mama wa Kizungu anasema kuwa kila waendapo na mkewe, lazima watamshangaa. Anakiri kuwa watu wengi ni wabaguzi.
Tunaweza kuwa sahihi au la kutokana na, kama tulivyo gusia hapo juu, kuwa kuna Wazungu wasiofanya hivyo kwa sababu na mila wajuavyo.
Tumetumia kisa cha kufunguliana milango kama nyenzo ya kuonyesha ubaguzi kati ya wanandoa waliomo kwenye ndoa za rangi mchanganyiko usivyoepukika.
Wakati Walter akiongelea watu kumshagaa hadi wengine kujiuliza ‘hili baba jeusi’ linataka nini hapa, anasema pia, si rahisi kwake kutoka peke yake. Hatujui kama ni kwa ndoa zote, ila uzoefu wetu unaweza kusema hivi.
Ukiachia mbali malalamiko ya Walter kubaguliwa kwa kuonyeshwa mishangao hata kuhojiwa anachotafuta kwenye kusanyiko la Wazungu, yupo Mmarekani mweusi ambaye binti yake alikubali kuolewa na mvulana wa Kizungu.
Kwa ufupi, alikaririwa akisema: “Hata kama mwanamume anaonekana kuwa mzuri vya kutosha, nilihisi binti yangu hakujua alichokuwa akikitengeneza.”
Hapa, unaweza kuona kuwa ubaguzi uko pande zote ingawa, mara nyingi, wanaobaguliwa husukumwa na ubaguzi wanaotendewa hadi kugeuka wabaguzi. Hata hivyo, kwa Afrika ambako wengi huwaona Wazungu kama wakamilifu na wakombozi, itachukua miaka hali kubadilika au kubaini ubaguzi huu wa kimfumo.
Hata hivyo, mambo yamebadilika. Tunaye rafiki yetu kutoka nchi jirani anayeendesha magari makubwa ya mizigo aliyeoa mama wa Kizungu. Hivyo, mara nyingi, huwa safarini ama ndani ya nchi au nchi jirani ya Marekani, hasa ikizingatiwa kuwa tunaishi kilomita kumi tu kutoka mpakani mwa Marekani.
Marekani, kama ilivyokuwa kwa Afrika ya Kusini wakati wa utawala wa kibaguzi wa Wazungu wachache, ubaguzi wa rangi ulikomeshwa, lakini bado upo hasa kwa wanandoa.
Kwa mfano, kwa mujibu wa CBCNews (2017), huko New York, mnamo Machi, mwanamume mmoja mweusi mwenye umri wa miaka 66 aliuawa kwa kuchomwa visu na mtu aliyesema wazi wazi kuwa alilenga kukomesha ndoa za watu wenye rangi mchanganyiko. Kuonyesha ubaguzi, mwanamke aliyekuwa na marehemu hakudhuriwa.
Zaidi, Agosti mwaka 2016, huko Olympia, Washington, Daniel Rowe ambaye ni mweupe aliwajongelea wanandoa wawili waliomo kwenye ndoa ya watu wa rangi tofauti na kumchoma visu tumboni mwanaume mweusi mwenye umri wa miaka 47 na mkewe mwenye umri wa miaka 35.
Kwa bahati nzuri, waathirika hawa hawakufariki na mtuhumiwa alikamatwa.