
Tunawaona bibi wa Kizungu na kijana Mwafrika uwanja wa ndege (hatuutaji) wakibusiana. Tumeamua kuandika haya juu ya utumwa kimapenzi ambao Waafrika ndio waathirika.
Utumwa huu umejikita kwenye mapenzi bandia ambapo mmoja wa ‘wapendanao’ humtumia mwenzake kulingana malengo na hadhi na rangi yake. Hatuzushi! Utaona vibabu/bibi vya Kizungu vikifunga ndoa na wavulana/wasichana wa Kiafrika.
Bila kupoteza muda hapa kuna tamaa, ujinga, na umaskini na hivi ndivyo vyanzo vya ukoloni na utumwa huu wa kimapenzi.
Katika mila za Kiafrika, mwanamume hutegemewa kuoa mtu ama wa umri wake au anayemzidi umri japo si kwa mbali sana.
Inapotokea mwanamume akaoa mwanamke sawa au zaidi ya mama yake au binti akaolewa na kibabu sawa na babu yake, jamii hustuka, kuhuzunika, kushangaa, kuchukia na hata kulaani.
Hakuna kitu muhimu katika ndoa kama tegemeo la kuzaa watoto ambao ndiyo malipo kwa jamii na wazazi. Ndoa bila mtoto kwa Mwafrika, ni janga.
Tujiulize, inakuwaje wahusika wanaweka kando hitajio hili muhimu? Kuna nini cha mno? Inakuwaje kijana wa Kiafrika kufunga ndoa na zee lisiloweza kumzalia au kumzalisha au kumuachia ujane?
Je, ni tamaa, ujinga, au umaskini ukiachia mbali kuabudia rangi ambapo mweupe, hasa Mzungu, anaonekana mali japo si mali kitu?
Katika ndoa hizi kama kweli ni ndoa, hatujawahi kuona Mwafrika mzee akioa msichana mzungu au kijana mzungu akioa bibi Mwafrika. Kuna tatizo. Si rahisi kupata majibu sahihi bila kudurusu.
Kwa akili ya kawaida, hili si jambo la kawaida, hasa kwa Waswahili. Kimsingi, katika ndoa hizi, mweupe ana mamlaka na Mswahili hana. Si vibaya kusema kuwa Mswahili anaolewa katika uhusiano huu.
Kiafrika, mwanamume huoa na mwanamke huolewa. Ila katika uhusiano tunaojadili, mwanamke/mwanamume wa Kiafrika huolewa na mzungu ambaye humuoa bila kujali jinsia.
Hata katika utumwa huu, Mswahili hutegemea akiolewa na Mzungu ataukata kwenda majuu na kuchuma madola.
Hapa thamani ya maisha ya binadamu ambayo ni kubwa kuliko chochote, huwekwa kwenye vitu vya ovyo kutokana na ujinga au umaskini kama masalia ya ukoloni wa kimila ambapo mtu mweupe ni mkombozi wa mtu mweusi.
Tuweni wakweli. Hivi kuna mapenzi ya kweli kati ya kizee cha miaka tuseme miaka 60, 70 au zaidi kuolewa na kijana wa miaka 30, 35 hata 40 au babu kuoa kigoli umri wa mjukuuwe?
Hapa tunapata dhana ya ubaguzi wa kujitakia ambapo mwathirika hujiona dhaifu mbele ya mkoloni wake bila kujali jinsia. Je, kuolewa na mzungu ni kuukata au kupatikana licha ya kudhihirisha ujinga, umaskini, na tamaa ya wahusika?
Tumeisha Ulaya kitambo si haba. Kuna kitu wanacho yaani ubinafsi/umimi ambapo mtu kujiona kama huru na asiyejali wengine isipokuwa yeye.
Hapa ndipo chanzo cha kwanza cha balaa hili kilipo mbali na ukoloni ambapo Waafrika wameaminishwa na wakaamini, iwe ni kwa kupitia dini au siasa kuwa wazungu ni wakombozi wakati ni waangamizaji. Utamuona Yesu mweupe wakati hakuwa mzungu. Mitume wote siyo Waafrika. Maandiko matakatifu yote ni ya kigeni na lugha zinazotumika kuyaeneza.
Huu ndiyo mzizi wa kila kitu. Waligundua, kutengeneza na kueneza ‘weupe’ kuwa ukombozi na wengine ni wenye dhambi. Unashawishika kuwa kila mtu anazaliwa na dhambi wakati mtoto mdogo ni malaika?
Utumwa kwa Waafrika ulianza tulipohujumiwa na kurubuniwa kuacha mila zetu tukakumbatia mila hatari za kigeni ziitwazo dini na ustaarabu japo si chochote wala lolote bali maafa kwetu.
Mzazi unajisikiaje kijana wako wa kike/kiume anapoolewa na bi kizee kuliko hata baba au mama yake kwa kisingizio cha ‘mapenzi hayana macho.’ Mapenzi yana macho.
Ndiyo maana, hayaishi bila kuwa na uhuru na utashi wa kuchagua, ambao katika balaa hili jipya haupo. Binadamu anapotumia njaa, tamaa, ujinga na umaskini kama nyenzo za kufikiri, anaweza kufanya jambo ambalo hata mnyama hawezi kufanya.
Tumalize kwa kuwashauri vijana wa Kiafrika kuacha kuuza utu wao eti kwa tamaa na ujinga wa kwenda majuu.
Wakishafikishwa ‘majuu’, huumizwa na kuwa watumwa zaidi wakaishia kujuta kama mmoja niliyekutana naye kwenye mji jirani aliyenyofolewa Arusha na kuishia kwenye utumwa.