
MAFANIKIO yaliyoletwa na Kampuni ya magari ya Toyota kutokana na ubora wa gari lao aina ya Toyota R5, yamewapa mzuka madereva wa mbio hizo kutaka kuendelea nayo katika mashindano yajayo.
Gari hilo lililoendesha na dereva Yassin Nasser na msoma ramani wake Ally Katumba kutoka Uganda lilisababisha kumaliza wakiwa washindi na kutwaa ubingwa wa Taifa kitengo cha NRC 2, wakiwa na timu ya Moil.
Wakiendesha gari hilo, pia walishinda mashindano ya Mkwawa yaliyofanyika mkoani Morogoro, huku wakimaliza nafasi ya pili katika mashindano ya Guru Nanak yaliyofanyika Arusha.
Dereva wa mbio za magari kutoka Morogoro, Waleed Nahdi alisema kuna baadhi ya madereva wamepanga kutumia kampuni hiyo wakiwamo Ahmed Huwel na Samir Shanto na wako katika mchakato wa kuleta ya kisasa zaidi.
“Ahmed Huwel na Samir Shanto huenda wakatumia gari aina ya Toyota kwani wamenza mchakato wa kuleta ya kisasa zaidi,” alidokeza na kuendelea madereva wengine pia huenda wakaanza kutumia aina hiyo kutokana na kuleta matokeo mazuri kama ilivyokuwa kwa timu ya Moi ambao waliibuka na taji la dereva na msoma ramani bora wa mwaka 2023.
Hii huenda ikawa mara ya pili katika kipindi cha miaka 25 kama Huwel ataleta Toyota ya kisasa mashindanoni tangu mara ya mwisho kutumika
Mwaka 1998 na aliingia katika mbio hizo kwa mara ya kwanza akitumia Toyota Celica GT4.
Gari aina ya Toyota zilitamba hadi kufikia miaka ya 90 mwishoni na baada ya hapo hadi miaka hii, mbio za magari nchini zimekuwa ni ushindani wa Subaru Impreza na Mitsubishi Evolution katika barabara za vumbi zikilipita Skoda Fabia lililoletwa na dereva kutoka Kenya, Manvir Baryan na Ford Proto lililotumiwa na Ahmed Huwel miaka ya karibuni.
Hata hivyo, baada ya raundi zote nne mwaka jana, Mitsubishi ndiyo iliyoshinda nafasi zote tatu za juu, huku Manveer Birdi akishinda nafasi ya kwanza kwa ubora akiwa na Mitsubishi Evo 9, akifatiwa na Gurpal Sandhu aliyeendesha Mitsubishi Evo 10, ya tatu ikienda kwa Randeep Birdi, akiwa na Mitisbishi Evo 9 na kuiacha Toyota R5 ya Moil team nafasi ya nne.
“Kwangu mimi Mitsubishi ni gari bora sana kwani lina kasi na hutulia vyema barabarani,” alisema Birdi baada ya kuitumia kushinda ubingwa mwaka jana.