Ndejembi awaka watumishi kutoa siri za ofisi

Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amesema changamoto kubwa aliyokutana nayo katika wizara hiyo ni baadhi ya watumishi kujihusisha na utoaji wa siri za ofisi.

Ndejembi ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 16, 2025 wakati akifunga kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Dodoma.

“Jambo ambalo, ninataka mfikishe kwa walio chini yenu ni usiri, jambo ambalo likiwa ni premature (halijaiva) likizungumzwa tu, halijafanyiwa unalikuta liko nje,” amesema.

“Jambo linaweza kuwa ni utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Serikali lakini unakuta tayari jambo hilo liko nje, tuna changamoto kubwa sana ya usiri katika wizara yetu,” amesema.

Amesema wakati mwingine inakuwa ni suala la michoro ya ndani ya wizara yao lakini haujapitishwa wala kujadiliwa unakuwa umetoka nje ya wizara.

Ametaka wajumbe hao wa baraza kuwaeleza wafanyakazi wenzao wawe na kifua cha kutunza siri za ofisi, hivyo imekuwa ni kilio kikubwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ni jambo hilo.

Amesema mambo yanayotolewa nje ya ofisi wakati mwingine inakuwa ni ya kufikiria na hayajashirikisha viongozi wengine wa Serikali.

Aidha, Ndejembi amewataka wafanyakazi hao kujiandaa kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali kabla ya kustaafu ili kuwapatia mapato mara baada ya muda wao wa kazi kuisha.

Pia amesema kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha kuwajali kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35, wafanyakazi hao wanatakiwa kuonyesha ufanisi kwa kuongeza makusanyo ya mapato.

“Nilipokuwa napitia bajeti yetu, nilikuwa naona kiwango cha makusanyo tuliopangiwa ilikuwa ni Sh250 bilioni lakini hadi mwezi huu tumeshakusanya Sh138 bilioni tunaona kuwa hatujafikia malengo,” amesema.

Akimkaribisha waziri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Anthony Sanga amesema kuanzia mwakani watakuwa na zawadi kwa wale waliofanya vizuri katika makusanyo ya tozo na ada za ardhi.

“Tulikuwa tunashirikiana uzoefu wale waliofanya vizuri wamefanya nini na wale waliofanya vibaya nini kimewakwamisha lengo ni kufanya vizuri,” amesema Sanga na kuongeza kuwa watakuwa na timu ambayo itakuwa na vigezo vya kupima ufanisi wa kila mkoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *