Ndege za kivita za Israel zalenga maeneo kadha ya kusini mwa Lebanon – IDF
Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema kwamba Israel imetambua mpango wa Hezbollah unaotarajia kulenga na kurusha makombora upande wa Israel ambao IDF imesema kuwa unalenga raia.
‘Tunaondoa tishio lolote dhidi yetu kwa upande wa nyumbani,; alisema Hagari akiongezea kwamba makumi ya ndege za kijeshi kwa sasa yanatekeleza mashambulizi kwenye maeneo kadhaa wanayosema Hezbollah wamekita kambi kusini mwa Lebanon.’
Ameongeza kwamba, ‘Tutaendelea kuondoa tishio lolote na kushambulia vikali kundi hilo la kigaidi la Hezbollah.’
Maafisa wa Israel wanatarajiwa kujadiliana na wajumbe wa masuala ya kigeni wa mataifa washirika kuhusu hatua itakayofuata.
Kama tulivyoripoti awali, Rais wa Marekani Joe Biden amewaamrisha maafisa wa taifa lake kuwasiliana kwa karibu na Israel kuhusu yanayojiri kwa sasa.
Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant amezungumza na Waziri mwenzake wa Marekani Lloyd Austin, na kumueleza kwamba Israel ‘ilikuwa imetekeleza shambulizi mahsusi lililolenga Hezbollah ili kuzuia tishio kubwa ‘ dhidi ya raia wa Israel.
Maafisa hao wawili walizungumzia umuhimu wa kuzuia vita kuzuka katika eneo kuu la mashariki ya kati, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la Israel.
Lakini taarifa hiyo iliongezea suala ambalo Waziri Gallant alilisisitiza kuwa Israel ‘ingetumia mbinu na nguvu zote ilizo nazo kuondoa tishio lolote dhidi yake’ na kwamba ‘imejiandaa kutuma majeshi yake na kuchukuwa hatua nyinginezo za kijeshi.’
Wakati huo huo, waziri wa masuala ya kigeni wa Israel Katz, amewaandikia barua mabalozi kadhaa akiwaomba msaada kwa ajili ya taifa lake kujilinda dhidi ya Hezbollah, Iran na makundi yanayowaunga mkono.