Ndege yakatisha safari kisa rubani kusahau pasipoti

Abiria 257 wa Shirika la Ndege la United Airlines walikumbwa na mshangao baada ya ndege yao kurejea ghafla Marekani, ikiwa safarini kuelekea Shanghai, China kisa mmoja wa marubani alikuwa amesahau pasipoti.

Ndege hiyo aina ya Boeing 787, iliyokuwa ikitekeleza safari ya UA 198, iliondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Los Angeles (LAX) mnamo Jumamosi, Machi 22, saa 8 mchana. Baada ya takriban saa mbili angani, iligeuza mwelekeo na kutua San Francisco saa 11 jioni, baada ya kugundulika kuwa rubani amesahau pasipoti yake.

Kulingana na taarifa ya United Airlines kwa CNN, kampuni hiyo ilisema, “Rubani hakuwa na pasipoti yake ndani ya ndege. Tuliratibu upya safari na kuweka marubani wapya ili kuwasafirisha abiria usiku huo.” 

Baada ya kutua San Francisco, abiria walipatiwa vocha za chakula zenye thamani ya dola 30 kila mmoja na fidia nyingine kupitia mfumo wa malalamiko wa shirika hilo.

Aidha, ndege mpya iliondoka San Francisco saa 3 usiku na kutua Shanghai saa 6 baadaye, ikiwa imechelewa kwa takriban saa sita. 

Yang Shuhan, mmoja wa abiria waliokuwa kwenye safari hiyo, alisema alisikia sauti ya rubani kupitia mawasiliano ya ndani ya ndege, akisema kwa huzuni, “Nimesahau pasipoti yangu.” 

Ingawa baadhi ya abiria walimsifu rubani kwa uaminifu wake, wengi walilalamika kupitia mitandao ya kijamii, hasa kwenye RedNote, mtandao unaofanana na Instagram nchini China, wakieleza kuwa walikerwa na usumbufu huo. 

Yang, ambaye alikuwa safarini kurejea nyumbani Hangzhou baada ya safari ya kibiashara, alifika Shanghai saa 6 usiku, kisha akalazimika kusafiri tena kwa gari kwa saa mbili na nusu, hali iliyomchosha na kuathiri ratiba yake ya kazi Jumatatu.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *