Dar es Salaam, Wasanii wa kuwatazama kwa jicho la tofauti ni pamoja na Chilla. Huyu ni tatizo sana. Fundi. Ndiye picha sahihi ya fleva za Kibongo. Kuna ‘taimu’ mtu unajiuliza kakwama wapi? Usipate jibu.
Ukikutana naye na akakueleza yake unaishia kumuombea kwa Mungu. Timing mbovu na mikwamo ilileta ‘stresi’ kwa wasanii wengi. Chanzo ndio hicho, basi la Kiba, Bella na wegineo likamuacha njiani Chilla.

Bila hilo wasingepata ‘dili’ kibwege na ‘kushaini’ kirahisi. Wangefanya kazi kubwa, maana unapotoa kitu unatazama aliye mbele yako. Mbele kuna Chilla utatoaje pini la ovyo ili utoboe?
Unatoaje pini jepesi ukitegemea kiki? Chilla yupo katika kundi la wasanii wakali wasiopata kile kitu wanachostahili. Kuna ‘testi’ ya ‘gem’ imetoweka kutokana na mafuriko ya Unaijeria na Amapiano.
Wengi wapo kando kwa kushindwa kwenda na kasi. Wengine kuzidiwa na matumizi ya dawa za kulevya na ‘stresi’. Wa ‘stresi’ wengi wao wako kando ya game kwa kukorofishana na wasimamizi wao.

Bushoke alitoweka kinamna hiyo. Siyo kuishiwa mashairi au kukosa studio. Bushoke ni yule yule ama pengine ni bora zaidi. ‘Of’Kozi’ ndio maana leo hii yupo na mshua wake mara kadhaa na bendi yao.
Utajiri wa sauti, uwezo wa kuandika na kuimba wa Chilla ni utajiri. Chilla anachokosa ni akili ya kujiongeza. Hii akili ipo kwa wachache na sasa naiona kwenye ubongo wa Marioo. Yule dogo noma.
Hapo kati ilikuwa kwenye ubongo wa mtu mmoja tu, Diamond. Lakini kwa sasa wengi wanajua wapi na wapi wapite. Ukiachana na Mondi kuna Kiba, Konde, Darassa, Marioo, Rayvanny na Jux.
Kuna dogo kama Chino, Mbosso, Jay Melody na madogo wengine kibao. Wanaufanya muziki vyema na kusonga kwa njia nyingi. Huku ‘dijito platifomu’ ikivimbisha zile akaunti zao.
Chilla siyo tu usimamizi. Bali hata kujua tu nani anastahili kusimamia kazi zake hajui. Siku ubongo wake ukiamka na kujua afanye nini kwa njia ipi. Watu kibao watakimbia mji.
Chilla ni wale wasanii wanaoweza kugeuza njano kuwa buluu. Tena ni kwa usiku mmoja tu. Kasikilize lile pini la ‘Taabasamu’, achana na Blue na kiitikio cha Steve R&B.

Kasikilize mwishoni mwa wimbo, Chilla kavuruga kila kitu. Kaonesha yeye ni nani na Steve RnB ni nani. Asubuhi ya AY na FA? Vipi My Boo ya Jafaray? Hizo ni chache kati ya nyingi. Huyu ni fundi!
Chilla ni mgodi unaozurura mitaa ya Dar. Badala ya kupishana na Davido kwenye ‘maeapoti’. ‘Kuselfika’ na pisi za maana kwenye majukwaa ya nje ya Bongo. Mwamba kakwama wapi? Hatujui.
Wakati nikiwaza ya Chilla. Ghafla nasikia stori na ‘klipi’ za Lulu Diva na Hemed Phd. Wakitukanana ovyo ovyo, huku pisi kali Nana Dollz na Dolly Rest zikitwangana. Sababu ya ugomvi hakieleweki.
Nainuka na kwenda zangu kwenye kiota cha jirani. Eneo langu tengefu kwa ajili ya kupunguza uhai wa figo. Kwa vimiminika vinavyolainisha na kusawazisha mambo magumu kwa ‘hedi’. Tungi tungini.
Nimekaa kaunta kwa dakika kadhaa bila kusikilizwa. Najipa imani kuwa pengine kunizoea sana ndo chanzo. Naamua kujipa moyo kwa kupitia jumbe kadhaa za WhatsApp. Grupu zote stori ni Zuchu na Mondi.

Kwamba wametemana rasmi na ujumbe kaandika Zuchu eti. Ndipo nagundua wahudumu walikuwa wanateta hilo hilo. Nikawasamehe na kuwaagiza kinywaji changu ili nihame kimawazo.
Zuchu ana nguvu za kuandika kwa kutemana Simba la Masimba. Yaani penzi lao limekuwa ratiba ya shoo au kipindi kipya kwenye tivii. Au penzi lao ni ‘sirizi’ kiasi kwamba lazima awataarifu watazamaji?
Simba la Masimba ni boss wake ukiachana na mapenzi. Unatoaje taarifa hiyo nyeti kirahisi hivi? Yes! Maneno ya Zuchu si mageni hapa mjini. Labda kama umekuja leo kutoka Ubena Zomozi.
Mwaka unatoweka na kiki za ajabu ajabu. Mpaka mtu unajiuliza huu ni mwaka 2024 au 2012? Pigo za kiki zilitoweka na watu wasiojulikana. Mbona Komasava ilitoka bila kiki? Mbona tamthiliya zinakimbiza bila kiki?
Hata ukienda bar, ukianza kuona wahudumu wazuri kuliko ‘waifu’. Inuka haraka sana, pombe imeteka eneo lote la ‘ploti’ ya ubongo. Na inataka kujenga nyumba ya kuishi kabisa.
Ukiona kiki zinazidi ujue uwezo wa kufikiri wa msanii umeyumba sana. Kiki ni dalili ya upungufu wa muda wa kufikiria. Kiki ni ndugu moja na uvivu wa kutafakari. Kiki udugu wake ni ujinga.