Dar es Salaam. Kwa utafiti mdogo. Ambao sihitaji ruksa ya mitume na manabii kuniruhusu niseme. Huu ni utafiti wangu binafsi. Nimetumia miaka kadhaa ili kuukamilisha na kimsingi kazi hiyo imeisha na sasa naleta kwenu.
Nimegundua waalimu huolewa haraka sana. Na pia huolewa kwa wingi tofauti na fani zingine. Waalimu wana upako wao na ndoa. Yaani ukiwa mwalimu tu lazima uoe au uolewe kwa haraka sana.
Ni vigumu mwalimu aliye kazini zaidi ya miaka mitano, akaendelea kuwa singo. Siyo kwamba hakuna waalimu singo, wapo ila ni nadra sana. Akiwa singo ujue ndo anaanza kazi au mjane.
Na utafiti hausemi kama wanajua sana mapenzi. Ama wanajua sana kuvumilia shida. Au wanafahamiana na wauzaji wa jumla na rejareja wa limbwata. Lakini ujue tu ndoa na maticha ni kulwa na doto.

Mahakimu, majaji, wanasheria, waandishi, wanaharakati na wasanii. Asilimia kubwa wako singo ama. Wenye vyeo vikubwa, na wasomi sana pia wengi wako singo. Kujua mambo mengi hukimbiza waoaji?
Au ndiyo msemo wao ule wa unavyozidi kujielimisha sana ndiyo unazidi kuwa mjinga?
Ubize wa masomo hufanya wakae mbali na mambo ya kijamii ikiwemo uhusiano? Lakini kwa mwanamke mwenye akili, ndoa siyo jambo la bahati.
Ndoa ni uamuzi sahihi wa kuchagua mazingira sahihi ya kupata mume bora. Na mume bora hujengwa na mke bora. Mke anaweza kumfanya mume awe anavyotaka awe yeye.
Mume bora na baba bora hutengenezwa na mwanamke. Yaani mama mzazi au mkewe.
Huwezi kupata mume bora ukijiweka katika mazingira magumu. Mazingira yasiyo rafiki na uhusiano sahihi.
Na kwenye sanaa zetu mazingira ni kama hayatofautiani sana. Wakati asilimia kubwa ya waalimu huolewa. Pia asilimia kubwa ya wasanii hutoka kwenye familia masikini na tena masikini zaidi.
Kuna wasanii wa kishua ambao kwao ni mboga saba kujisevia. Lakini ni mmoja kati ya mia moja. Na wengi wao hujifurahisha tu kwenye sanaa. Ni ngumu kukutana na staa wa muziki kutoka familia bora.
Siyo kwamba walalahoi ndiyo waliojaaliwa vipaji pekee. Hapana! Shida ni kwamba sanaa ndiyo furaha yao pekee. Watoto wa kishua wana vitu vingi sana vya kuwapa furaha.
Wakati watoto wa walalahoi ‘wakiinjoi’ kufanya muziki au kucheza filamu. Wa kishua wao ‘huinjoi’ muziki kwa kucheza, kusikiliza au kutazama. Muziki na familia majalala ni kulwa na doto.
Wakati wa kishua wakicheza muziki kuvuja jasho kwa afya na furaha. Walalahoi kwao hucheza muziki na kuvuja jasho wapate ugali wao. Shida zao zinawapa mzuka wa kuimba na kucheza.
Kimsingi watoto wa kishua huishi maisha, ambayo walalahoi huota kuyaishi baadaye kupitia vipaji vyao. Yaani furaha na shibe ya mtoto wa kishua inawapa mizuka kucheza au kuimba muziki.
Hapa ni suala la saikolojia. Saikolojia ya masikini inataka kupata kile alichonacho mtoto wa tajiri. Saikolojia ya mtoto wa kishua inataka kuuburudisha mwili na akili kwa muziki wa masikini.
Saikolojia ya tajiri inatamani moyo na mwili wake uburudike tu.
Muziki ni sanaa ya mtu mnyonge na mlalahoi. Sanaa ya binadamu mwenye ombwe la ukandamizwaji. Ni kazi iliyogeuzwa biashara kubwa na matajiri.
Afrika ya Kusini, kabla ya siasa za ubaguzi kuondolewa. Walitengenezwa wanamuziki wengi. Siyo kwamba nchi ilibarikiwa sana vipaji. Bali maumivu yao waliyapooza kwa nyimbo.
Ni ngumu mtoto wa kishua kuwa na akili ya kutunga wimbo kama Nenda Kamwambie, Ukimuona au Naogopa wa Marioo. Lakini mtoto wa kishua ni rahisi sana kusababisha mtoto choka mbaya kuandika mashairi ya namna hiyo.
Muziki ni tiba kwa masikini. Muziki ni liwazo kwa mwenye njaa. Muziki ni maombolezo. Muziki ni kiburudisho cha nafsi iliyokinai. Ni kweli kwamba wasanii na umasikini ni ndugu mmoja.