Dar es Salaam. Ukipata nafasi ya kufika kule Mbozi, Mbeya. Ukakutana na habari za watu waliotajirika kutokana na kilimo cha kahawa. Unaweza kuwehuka, kujiona kama mtu uliyechelewa kweli kweli. Wakati unarudi, shuka Mafinga pia fuatilia stori za mamilionea.
Walioupata utajiri kwa biashara ya miti na mbao. Unaweza kudhani watu kinachowapa utajiri haraka ni mbao pekee! Pitia Ruaha Mguyuni. Na hapo utakutana na wakulima wa nyanya na vitunguu. Watakuonesha ‘kosta’ zao na fuso walizonunua kwa kilimo cha msimu mmoja pekee.
Aisee kama una akiba flani, utanunua shamba muda huohuo. Kuachana na ajira ghafla. Utaaga washikaji na nduguzo wote. Huku ukitoa ahadi za kwamba ukirudi wajiandae kuachana na bamia. Ni mwendo wa ‘flleti’, ‘steki’, korekore, tasi na misosi yote ya hadhi ya nyota tano.
Ukitoka pale ukaenda hadi Mang’ula na Ifakara. Ukakutana na habari za watu wanavyopiga pesa za mpunga. Kichwa kitawaka moto. Utajizabua vibao na kujimaindi. Halafu utajiuliza, “Nilikua wapi siku zote hizi?” Ukitoka kule jisogeze hadi Kariakoo.

Kisha kutana na ‘mabizinesi mani’ wa maduka. Wanaofuata dili na bidhaa huko China, UK, Thailand na Dubai. Utapigwa butwaa kuona watu wakiongelea mamilioni kwa mibilioni, kama wanaongelea elfu kumi kumi.Usipokuwa na utulivu utaamini kuwa biashara zinazolipa ni maduka.
Tena unaweza kuanza kuhangaika kupata fremu pale! Nenda na Arusha kutana na stori za mabilionea wao wa madini. Utaacha kila kitu na kuanza kuhangaika na madini. Hapo hujasikia wanaopiga dili la utalii. Ile Kariakoo utaona cha mtoto sana!
Wakati ukiendelea kutafakari, rudi mtandaoni. Kukutana na wanaoitwa ‘netiweki maketingi’. Wakikuelezea stori zao, wakikusimulia walivyonunua ‘vogi’. Wakikuonesha picha walizokua wanakula bata. Mbao utaona biashara ya utumwa. Maduka Kariakoo utaona michosho. Mpunga utaiona madudu.
Ngoja niuchune kukupeleka kwenye fursa ya samaki. Kuzitoa Mwanza na kupeleka Congo. Ngoja nisikurushe roho na habari ya korosho, ambazo huwapa ubilionea Wamakonde kibao. Ngoja nikaushie habari ya ufuta! Hii ndiyo utadata uwe mwehu kabisa.
Usipokuwa na utulivu wa fikra. Habari za fursa za biashara na ujasiriamali. Zinaweza kugeuka kuwa kama miluzi mingi, ikakupoteza. Asikudanganye mtu kwamba kuna biashara bora zaidi ya nyingine. Biashara ni fursa yoyote unayoona inaweza kukupa utajiri.
Kuna matajiri kutokana na umiliki wa shule. Wengine umiliki wa mabasi. Wapo wa vituo vya mafuta. Wengine kwa kumiliki ardhi na makazi. Wengine kwa udalali mbalimbali. Usisahau dili linalomtajirisha huyu, mwingine dili hilo hilo linaweza kumfilisi jumla na kumpoteza kabisa!
Siyo kila fursa inayompa faida John, inaweza kukupa na Ashura. Fuatilia kwa umakini utabaini kuwa mafanikio hayakai katika uzuri wa fursa. Bali yanatokana na mneba fursa. Tujifunze fursa mbalimbali, lakini ifike sehemu tuchague fursa moja bila kurukaruka.
Utajiri hauji kwa kuwa bize na kila dili lililopo. Bali huja kwa kujifunza fursa nyingi na ‘ku-stiki’ na eneo moja. Ama maeneo ambayo, yatakutambulisha kwa watu wengi. Lazima ifike mahali utambue kila mtu anahitaji fedha za kutosha. Lakini hatuhitaji kiwango sawa na malengo yetu hayafanani.
Fursa zipo nyingi kuwa makini katika maamuzi. Usiwe na wasanii wa Bongo Fleva au Bongo Movie. Wanafanya dili nje ya sanaa zinazofanana kama sare za wafungwa. Analo anza nalo mmoja wote wanataka kufanya hilo hilo. Uvivu wa kufikiri.

Wanapiga mpunga mrefu, lakini mishe zao ni zilezile nje ya sanaa yao. Baba Levo na ‘Koi Mzungu’ dili la ‘Komedi’. Kiba na Mondi ‘midia’. Kuna Jide na Shishi, Eshe na Isha wote ni ‘misosi’. Achana na wa ‘onilaini tivii’. Kuna Anti na Wolper na mishe za vipodozi.
Ilifika wakati kila mwanamuziki akawa na wasanii wake. Kwa kuamini Mondi anapiga bao kuwamiliki kina Konde. Lakini haina maana wapige chini hizo dili. Kwa sababu ni bora kuliko sanaa ionekane inachozalisha majina mjini makubwa yenye njaa.
‘Ene wei’ ni suala la muda kila mtu hizi mishe zitampa wazimu. Na wao siyo wajinga kufanya dili zinazofanana. Ni kwa sababu kama taifa hatukuandaa vijana na ushindani wa soko la ajira au fursa. Watu wanaenda na upepo kama jezi za Palmerias.