
Dar es Salaam. Tamthiliya. Ndiko liliko kimbilio kwa waigizaji wetu. Hakuna tena filamu. Tunalazimika kutafuta ving’amuzi vya runinga tofauti ili tuwaone wasanii wetu tunaowapenda. Hili ni tatizo.
Na kibaya zaidi mbali ya vipaji vyao. Hawatumii jukwaa la mtandao kama wanamuziki. Hatuzioni kazi zao hadi tufungulie runinga. Tujazane sebuleni na watoto wetu au kwenye mabaa na wahudumu.
Maendeleo huja kama mafuriko. Husomba kila kitu na kuleta kila kitu hata visivyostahili. Hata gaguro ni kitu kilichopitwa na wakati. Kuna mabinti wa sasa hawajui hata linafananaje.
Hata neno gaguro anaweza kudhani ni jina la ugonjwa mpya. Maendeleo ni kama mafuriko. Yanasomba kila kitu unachokitegemea, na kuleta kila kitu hata usichotegemea.
Hata vijiwe vya kahawa vinatoweka. Sehemu pekee ambayo ungepata uongo wa kiwango cha PhD, ni katika vijiwe vya kahawa, huko ndiyo chanzo cha stori kama za Popobawa.
Lakini hii leo hakuna tena hivyo vijiwe. Maendeleo yamesomba kila kitu. Vijiwe vya sasa vipo kwenye magroup ya WhatsApp. Siku hizi ni ngumu sana kukuta watu wakizozana Bar.
Wengi wanakuwa bize na simu zao. Mianga ya ‘smatifoni’ tu kila meza. Soketi za umeme zimewekwa mpaka maliwatoni. Maana ndiyo kitu pekee kinauliziwa na walevi kabla bia.
Baa ikikosa miundombinu ya kuchaji simu. Utakunywa bia na mkeo. Watu wanataka kuwa hewani muda wote. Kimsingi baa yenye chemba za chaja hupendwa kuliko yenye madem.
Kaunta za baa na nguzo pamoja na kuta zake zimejaa soketi. Mtu kaenda na mchepuko wake hawasemeshani wako bize na simu zao. Tumekuwa kama majuha dunia ya sasa hivi.
Sasa maendeleo kwa sanaa ya filamu ni tofauti kidogo. Maendeleo yao ni ya dunia yao tu. Vigezo vya usanii kwa waigizaji haswa wa kike ni urembo, na wa kiume ni umaarufu.
Hizi tamthilia zetu zinazotamba kwa sasa. ‘Kwalite’ yao ipo kwenye vifaa vya ‘kushutia’, ipo kwenye mavazi na uzuri wa sura na umaarufu. Ukiwa na namba kubwa ya ‘folowazi’ Insta, basi unapewa ‘sini’.
Sio vibaya warembo na watu wenye majina nje ya filamu kuwa waigizaji. Lakini tatizo lipo kwenye kustahili, hapo ndipo linapokuja tatizo lenyewe.
Ni kweli wanafaa kuigiza?
Ni wachache sana wenye kuonesha kufiti. Uigizaji ni sanaa, siyo sehemu ya kuuzia sura au mavazi na nywele.
Ipo tofauti ya muonekano na uigizaji. Unamkumbuka Kemmy?
Yule mke wa Sembe katika mchezo wa ITV. Nani kama yeye kwa hawa wajasiriamali wa mitandao walioamua kuwa waigizaji? Nani wa kufanya hata nusu yake? Wengi ni wazuri wa sura siyo kazi.
Kasi ya watu wa muziki kimaendeleo ni kubwa kuliko wa filamu na maigizo. Tuna wanamuziki wa kimataifa. Kuna mapato makubwa kimuziki tofauti na filamu. Kuna kitu kinabidi kitazamwe vizuri.
Wengi wanaingia katika filamu si kwa sababu ya kupenda sanaa. Hawana mahaba na fani na hawajawahi kuwa nayo. Wanakuja kwa kasi kwa sababu wana kiu na njaa ya kutazamwa na wengi.
Ni hilo tu. Ndiyo maana hakuna ubunifu, hakuna kusonga mbele. Kuna ‘taimu’ fani hii inatia huzuni. Wapo walio na dhamira na vipaji vya kweli. Na kuna kundi lina nguvu na linataka wengine wasitambe.
Kundi hilo linataka sura na mionekano mizuri. Sio mbaya, ila vipi kuhusu vipaji na weledi wa fani? Vipi kuhusu mafunzo katika jamii kama moja ya makusudio ya sanaa yanavyotaka?
Kifupi tumepoteza mengi ya maana. Maigizo yenye uhalisia, vipaji vikubwa na vya uhakika. Hadithi za kibunifu na zenye mafunzo na miongozo bora kijamii. Kaole ya Dr Cheni na Nora, imebaki kumbukumbu nzuri tu.
Japo walifanya sanaa bila wawekezaji na muitikio mkubwa. Lakini waliacha alama muhimu za kukumbukwa. Hao wadau wa siku hizi wanashindwaje? Kwanini hawataki kutupa kilicho bora na sahihi?
Kama una uwezo wa kwenda kukodi majumba na magari ya thamani kwa ajili ya uzuri wa igizo, unashindwaje kupata wasaniii bora. Kwanini usisake vipaji halisi badala ya kuokoteza sura? Kina Christant Muhenga wako wapiKwa ushauri.
Kama kweli tuna uchu na maendeleo ya sanaa hii, kuna kitu tunatakiwa kufanya. Mwenye kipaji apewe nafasi na aoneshe kiwango halisi.
Sanaa haiwezi kukuwa kwa nyodo na mikogo wakati kazi ya maana hakuna. Sanaa haiwezi kupanda, kwa kutoa nafasi kwa kujuana kabla ya weledi. Wenye vipaji halisi wanatoweka.