
Dar es Salaam. Takriban nchi 33 zimethibitisha kushiriki maonyesho ya kimataifa ya utalii ya Swahili International Tourism Expo (Site) yanayotarajia kufanyika kati ya Oktoba 11 na 13, 2024 nchini Tanzania.
Maonyesho hayo yanatoa fursa kwa Tanzania kuwa na uwezo wa kufikia masoko katika nchi ambazo bado hazijaleta watalii wengi licha ya kuwa na watu wengi.
Maonyesho hayo yanabebwa na kauli mbiu isemayo, “Tembelea Tanzania kwa uwekezaji endelevu na utalii usio mithilika.”
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, leo Jumanne, Septemba 24, 2024 Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema uwepo wa maonyesho hayo unalenga kuimarisha mtandao wa wafanyabiashara waliopo katika sekta ya utalii wa ndani na nje ya nchi.
“Kuna watu wanaotoa huduma na bidhaa za utalii na wapo wadau ambao hununua vitu hivyo, hii itakuwa ni fursa ya wao kukutana na kubadilishana uzoefu,” amesema Mafuru.
Amesema tayari wamepokea uthibitisho wa ushiriki wa wadau 145 kutoka nchi 33 na kati yake zipo nchi ambazo ni masoko ya kimkakati.
Baadhi ya nchi zilizothibitisha ushiriki ni China, Denmark, Finland, Japan, Afrika Kusini, Kenya, Ethiopia, India, Oman, Uholanzi, Nigeria, Brazil, Ujerumani, Uganda na Lesotho.
Miongoni mwa mambo yatakayofanyika ndani ya siku hizo tatu katika ukumbi wa Mlimani City ni kuonyesha mazao ya biashara yaliyopo katika sekta ya utalii ili wanunuzi wakutane na wazalishaji kuendeleza mnyororo mzima.
“Pia, kutakuwa na mikutano ya biashara ambayo itawakutanisha watoa huduma wa Tanzania na wale wa nje ya nchi, semina mbalimbali zinazolenga kuwapa taarifa wadau wa utalii ikiwamo wauzaji bidhaa juu ya namna bora ya kufungasha bidhaa zao ili kuweza kufikia masoko ya nje,” amesema Mafuru.
Pia, kutakuwa na jukwaa la uwekezaji ili watu wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo wapate taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya uamuzi wenye faida.
“Tutashirikiana na wenzetu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili mtu ajue anawezeka Tanzania, kuna incentives kiasi gani, kodi zilizopo katika sekta ya utalii na masuala ya kifedha yapoje,” amesema Mafuru.
Mbali na hayo pia, wahudhuriaji wa mkutano huo watapata wasaa wa kushiriki katika ziara ya mafunzo na tayari maeneo sita yameandaliwa yanayopatikana katika ukanda wa Kusini, Magharibi na Zanzibar lengo likiwa ni kuwaonyesha wadau kuwa utalii wa Tanzania si wanyama pekee.
Haya yote yanafanyika wakati ambao Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji wa sekta ya utalii na sasa ina uwezo wa kuchangia asilimia 17 ya Pato la Taifa huku asilimia 25 ya fedha hizo ni za kigeni.
“Utalii unakua na ipo fursa ya kukua zaidi kwani kuna masoko ambayo hayajafikiwa zaidi au yanafanya kidogo tofauti na matarajio yetu. Tunahitaji kukua kwa sekta ya utalii katika masoko mapya, haya tuliyonayo ya Ulaya na Marekani na Afrika lakini sasa tunataka kwenda maeneo ambayo hayajatuletea watalii,” amesema Mafuru.