
Dar es Salaam. Wakati mataifa mbalimbali barani Afrika yakiendelea kufanya uwekezaji katika sekta ya elimu, wito umetolewa kwa nchi hizo kuweka mifumo itakayofanya elimu iendelee kutolewa hata yatakapotokea majanga.
Wito huo umetolewa leo Jumanne, Novemba 12 2024 na wadau wakati wa mkutano wa kimataifa wa ubora wa elimu ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) unaofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam ukihusisha washiriki kutoka mataifa ya 16 ya Afrika.
Hoja hiyo imetolewa kuweka msisitizo wa uwekezaji katika mifumo itakayoondoa vikwazo pale yanapotokea majanga ikiwamo mafuriko, magonjwa ya mlipuko na changamoto nyingine zinazoweza kuzuia wanafunzi kusoma.
Mshauri mwelekezi katika masuala ya elimu kutoka shirika la Hakielimu Dk Wilberfoce Meena amesema kwa miaka ya karibuni kumekuwa na mabadiliko yanayojitokeza katika mifumo ya elimu yakisababishwa na majanga mbalimbali hivyo ni muhimu kwa nchi kuwa na hatua za tahadhari.
Akitolea mfano wa mlipuko wa Uviko -19, mafuriko na matokeo mengine ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa yakidhoofisha utoaji wa elimu na wakati mwingine kusitisha kabisa shughuli za elimu.
“Hili ndilo limetufanya tukutane hapa kwa pamoja tukibadilishana uzoefu na wenzetu wa mataifa mengine wanafanya nini, lengo likiwa ni kutengeneza mifumo ambayo itawezesha uthabiti wa elimu. Isitokee kwa namna yoyote kwamba majanga yazuie utoaji wa elimu.
“Tunahitaji kuwa na mfumo thabiti wa elimu ambao unaweza kukabiliana na mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea na kuathiri utoaji wa elimu. Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa matumizi ya teknolojia na si hilo tu tunatakiwa kujipanga kwa namna yoyote ile kuhakikisha utoaji wa elimu haukutani na vikwazo,” amesema Dk Meena.
Kwa upande wake Mratibu wa TEN/MET Martha Makala amesema imefika wakati ni muhimu kwa nchi kuhakikisha ina mifumo bora, imara na thabiti ya elimu ambayo itafanya elimu iweze kutolewa zaidi ya darasani.
“Tunataka kuwa na mifumo iweze kutoa elimu hata nje ya darasa, tumeshuhudia majanga kama magonjwa ya mlipuko, matetemeko ya ardhi, mvua zinazosababisha mafuriko, tunapaswa kujiuliza je mifumo tuliyonayo inawezesha wanafunzi kuendelea kusoma yakitokea hayo.
“Zipo nchi ambazo zimepiga hatua katika eneo hilo ndiyo maana tumekutana kwa pamoja tushirikishane uzoefu katika kujenga mifumo bora na thabiti katika kuhakikisha tunatoa elimu iliyo bora, jumuishi na inapatikana kwa watu wote,” amesema Martha na kuongeza.
Kufanikisha hilo tutakuwa na mijadala mbalimbali ikiwamo uwekezaji wa rasilimali za ndani katika kusaidia na kuboresha sekta ya elimu, Tanzania tupo kwenye mageuzi ya kisera na mitalaa na mwaka 2028 tutashuhudia wanafunzi wa makundi mawili wakiingia kidato cha kwanza kwa maana wale watakaoishia darasa la sita na wale watakaomaliza darasa la saba mwaka 2027 hivyo ni lazima tujiandae,” amesema.
Akizungumza kwenye mkutano huo Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tamisemi Mohamed Mchengerwa amesema licha ya Serikali kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu, haiwezi kuwa na matukio chanya pasi ushirikiano wa wadau wa sekta hiyo.
Amesema asasi za kiraia zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa, hivyo ni muhimu kwao kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuikumbusha Serikali kutekeleza wajibu wake kwenye sekta hiyo muhimu.