Arusha. Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa sekta ya ujenzi nchini kwa kutoa mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza miradi kwa ufanisi, kupunguza gharama zisizotarajiwa na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.
Kupitia mafunzo hayo, NCC imelenga kuwajengea uwezo waajiri, makandarasi na washauri elekezi kusimamia mabadiliko ya kazi, madai, na migogoro kwa njia inayozuia upotevu wa muda, fedha na rasilimali nyingine. Ikielezwa kuwa hali hiyo inayopunguza gharama kwenye miradi ya ujenzi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa NCC, miradi ya ujenzi huathiriwa na mabadiliko ya kazi, ucheleweshaji wa kushughulikia madai na migogoro ambavyo kwa pamoja husababisha ongezeko la gharama, muda wa mradi na hata kushusha viwango vya ubora.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Mhandisi Tumaini Lemunge kutoka NCC amesema, “lengo letu ni kuona miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa gharama zilizopangwa na kwa ubora unaokubalika.”

Ameongeza kwa kusema kupitia mafunzo hayo, washiriki wamepata mbinu za kupunguza mabadiliko yasiyo ya lazima, kushughulikia madai mapema na kutatua migogoro kwa mujibu wa mikataba.
Wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi waliopata nafasi ya kushiriki wameeleza namna mafunzo hayo yatakavyowasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhandisi Lyda Osena kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema, “mafunzo haya yameniongezea uwezo wa kutambua, kuepusha na kusimamia migogoro na madai kwa njia ya kisheria. Vilevile, yatanisaidia kutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi, ndani ya muda, bajeti na ubora uliokusudiwa.”

Mkadiriaji Majenzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Davis Ryoba ameongeza, “nimepata uelewa mpya kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mikataba ya ujenzi. Sasa najua kuwa mabadiliko hayawezi kuepukwa kabisa, lakini yanahitaji usimamizi makini ili kuepusha gharama zisizokuwa za lazima.”
Kwa upande wake, Mwanasheria Elizabeth Kimako kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) amesema, “mafunzo haya yamenipa uelewa wa kusaidia taasisi yangu kuendesha miradi kwa ufanisi.”