
Unguja. Siku moja baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutangaza iko katika hatua za mwisho kuandaa nauli elekezi kwa waendesha bodaboda, baadhi ya madereva wa vyombo hivyo wameomba viwango hivyo vizingatie umbali wa safari, wakisisitiza huduma wanazotoa hazifuati njia maalumu (ruti) kama ilivyo kwa daladala.
Wakati waendesha bodaboda wakitaka upangaji wa nauli uzingatie masafa ya safari, baadhi ya wananchi wamependekeza kuundwa kwa chombo maalumu cha usimamizi kitakachoweka na kusimamia utekelezaji wa viwango vya nauli, pamoja na kuwachukulia hatua watakaokiuka taratibu zitakazowekwa na Serikali.
Maoni hayo yamekuja kufuatia kauli iliyotolewa katika Baraza la Wawakilishi na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Nadir Abdulatif Yussuf, aliyesema Serikali iko katika mkakati wa kuweka bei elekezi kwa bodaboda.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Mei 16, 2025, Msemaji wa Chama cha Bodaboda, Moh’d Mahmoud Hassan amesema kuwekewa kiwango cha nauli kwao itakuwa changamoto, kwa sababu wao hutoza kulingana na masafa ya safari.
Amesema kupanga kiwango cha nauli katika usafiri wa daladala ni rahisi kwa kuwa ruti zao zinajulikana kuanzia mwanzo hadi mwisho, lakini kwa upande wa bodaboda hilo litakuwa gumu kwa kuwa hawana ruti maalumu.
“Tunaweka nauli kulingana na umbali wa safari na makubaliano kati ya dereva na abiria. Mfano, nikitoka Tobo la Pili, si lazima niishie sehemu moja tu kama Bandarini,” amesema Hassan.
Dereva mwingine wa bodaboda, Adam Hafidh, amesema hatua hiyo itakuwa changamoto kwao, hasa kwa abiria wanaosafiri masafa marefu. Ameeleza kuwa Serikali inapoweka kiwango cha nauli inapaswa kuzingatia umbali na mizigo ya abiria, kwani viwango visivyozingatia hali halisi vitaathiri wateja wa maeneo ya vijijini.
“Kwa kawaida tunamtoza abiria kulingana na masafa na aina ya mzigo. Serikali iangalie hilo. Mfano, mtu akiwa na mzigo awe na kiwango chake, na asiye na mzigo awe na chake pia,” amesema Adam.
Kwa upande wao, baadhi ya abiria wameunga mkono uamuzi wa Serikali kuweka viwango vya nauli kwa bodaboda, wakisema gharama za sasa ni kubwa na huwatesa wananchi.
Zuwena Mmanga, mkazi wa Saateni, amesema Serikali imefanya jambo jema kuingilia kati suala hilo kwani baadhi ya madereva hutoza viwango vya juu kupita kiasi.
Naye Burhan Kassimu amesema anaunga mkono hatua hiyo, lakini ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha utekelezaji unafanyika badala ya kuishia kwenye majadiliano bungeni.
“Safari ya Sh500 kwa daladala, bodaboda wanatoza hadi Sh3, 000. Wanafanya biashara kwa faida kubwa sana huku wananchi wakiteseka. Serikali iweke chombo maalumu cha kusimamia utekelezaji wa viwango hivyo,” amesema Burhan.
Ameongeza kuwa kutoka Tobo la Pili hadi Malindi nauli ni Sh2, 000 hadi Sh3,000, na kutoka Malindi hadi Kisonge ni Sh2,000, viwango ambavyo vinawaumiza wananchi.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Haji Ali Zubeir amesema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri, wana mpango wa kuweka nauli elekezi, lakini kwa sasa bado hawana bodi ya wakurugenzi.
Amesema pindi bodi hiyo itakapopatikana, watapanga nauli elekezi kwa usafiri wa bodaboda. Aidha, amesema mamlaka hiyo inatambua changamoto wanazokumbana nazo wananchi kwa kutozwa nauli kubwa, na wamejipanga kupanga viwango vitakavyosaidia watumiaji wa huduma hiyo.
Zubeir amesema jambo hilo liko katika utaratibu, litapelekwa kwenye bodi, kisha kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohammed kwa ajili ya kulitangaza rasmi.