Napoli, Inter na vita ya Ubingwa Serie A

Napoli, Inter na vita ya Ubingwa Serie A

Imebaki vita ya wawili kati ya timu 20 zilizokuwa zikishindania taji la Ligi Kuu Italia, Seria A, Inter Milan na Napoli zitasubiri michezo yao ya mwisho itakayopigwa kesho Ijumaa, Mei 23 ili kumpata bingwa baada ya timu hizo kupishana kwa tofauti ya pointi moja kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Napoli inayoshika nafasi ya kwanza kwenye msimamo ikiwa na pointi 79, kesho itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Diego Armando Maradona kuikabili Cagliari katika mchezo huo wa maamuzi ya kumsaka bingwa wa Seria A msimu huu, wakiwa wameshaandaa suti za kushangilia ubingwa.

Kwa upande wa Inter Milan wao watakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Giuseppe Sinigaglia kukabiliana na vijana wa Cesc Fàbregas, Como 1907 ambao wamekuwa wasumbufu hasa wanapokuta na timu kubwa.

Inter Milan inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 78 italazimika kupata ushindi wa aina yoyote kuhakikisha inajiweka pazuri kubeba taji la Seria A, endapo kama wapinzani wao Napoli watapata matokeo ya sare au kupoteza kabisa.

Napoli ndiyo inapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo msimu huu kutokana na nafasi walionayo kwani wanahitaji ushindi wa aina yoyote bila kujali matokeo ya wapinzani wao.

Mara ya mwisho Napoli imechukua taji hili msimu wa 2022-2023, kisha Inter Milan ikachukua msimu uliopita wa 2023-2024 ambapo mpaka sasa wanaonekana kulitetea taji lao ambalo wamelichukua mara 20 katika vipindi tofauti.

Pengine Inter Milan, wangekuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa huo kama wasingeruhusu matokeo ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Lazio wikiendi iliyopita, kwani iwapo wangeibuka na ushindi wangekuwa wanaongoza ligi kwa pointi 80 kwani siku hiyo wapinzani wao Napoli walilazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Parma.

Katika michezo ya kesho makocha wa timu zote mbili kwa upande wa Inter Milan, Simone Inzaghi atakosekana katika sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo uliopita vilevile kwa kocha wa Napoli, Antonio Conte naye hatakuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata katika mchezo uliopita.

Timu ya Juventus ndiyo inayoshikilia rekodi ya kuchukua taji la Seria A mara nyingi ikifanya hivyo mara 36 wakati ikiwa ndiyo imelichukua mara nyingi kwa mfululizo ikifanya hivyo mara tisa kwanzia mwaka 2012 hadi 2020.

Iwapo Napoli itabeba ubingwa wa Seria A, msimu huu utakuwa ni wa nne baada ya ule iliyochukua mwaka 1987, 1990 na 2023 kwa upande wa Inter Milan kama wakiibuka na ubingwa watafikisha jumla ya mataji 21.

Endapo kama Napoli ikipoteza mchezo wa kesho dhidi ya Cagliari na Inter Milan ikapata sare dhidi ya Como timu hizo zitakuwa zimelingana pointi na zitapangiwa kucheza mchezo wa kumtafuta Bingwa wa Seria A msimu huu kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *