Dar es Salaam. Ni nani yuko nyuma yao? Hili ni miongoni mwa maswali yanayogonga vichwa vya wadau mbalimbali wa demokrasia nchini, kwa kile kinachoendelea ndani ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Msemo wa “usimkatie mtu tamaa” ndio unaoakisi historia ya maisha ya Chaumma, kutoka kuwa chama kilichotazamwa kama msindikizaji hadi kuwa sehemu ya mijadala katika mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, na mitaani.
Ni Chaumma ile ambayo mikutano yake ya hadhara na kampeni, ukiacha mgombea, usingekuta watu wanaofika 200 kutia shamrashamra, lakini leo kimeujaza ukumbi unaochukua zaidi ya watu 1,000 na shangwe kama lote.

Nani aliyejificha nyuma ya mafanikio hayo? Kwa sababu Chaumma, iliyokuwa ikifanya mikutano yake na gari moja au mawili, ukiacha lile la mwenyekiti wao, Hashim Rungwe lakini sasa kinakodi mabasi kubeba wanachama kutoka mikoa mbalimbali kuwakusanya Dar es Salaam.
Isingekuwa rahisi kujua kama Chaumma inafanya mikutano yake ya ndani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, lakini sasa mkutano wake ndio habari ya mjini, kikiwapokea wanachama zaidi ya 3,000 waliojiondoa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mathalani, mkutano mkuu wa Chaumma wa mwisho uliofanyika Septemba 28, 2024, ulifanyika Hoteli ya Rungwe iliyopo Sinza, jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, ulimchagua ‘Mzee wa Ubwabwa’ kuendelea kukiongoza chama hicho.
Utofauti wa mkutano huo na mingine ya nyuma na hii iliyofanyika sasa ni mithili ya msemo wa Waswahili: “mbingu na ardhi”. Ndipo swali la nani mratibu wa hili linapoibuka.
Taarifa kutoka kwa viongozi waandamizi wa Chaumma zinaeleza kuwa ujio wa waliokuwa viongozi na makada wa Chadema umekifanya chama hicho kuwa na mtazamo na mwonekano mpya.
Lakini yote haya yanatokea ama yanaacha au kuzidisha maswali lukuki, je, nani yuko nyuma ya hao waliotoka Chadema kwenda Chaumma? Fedha za kugharamia mikutano, sare za chama na nyinginezo zinatoka wapi? Lengo la kuwafadhili linatoka wapi? Kwa nini sasa? Na mwisho wa yote, wanahitaji kitu gani?
Mzee wa Ubwabwa anasema, “Sasa ni chama cha ushindani na si kushiriki.”
Tangu Mei 7, 2025, waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema katika utawala wa Freeman Mbowe walipotangaza kujiondoa ndani ya chama hicho wakieleza kuwa watatangaza wapi watahamia, Mwananchi lilidokezwa na msiri kwamba watakwenda Chaumma.
Waliojiondoa ni waliokuwa manaibu katibu wakuu, Benson Kigaila (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar), Katibu wa Sekretarieti, Julius Mwita, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Catherine Ruge, na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema.

Kati ya hao, Halmashauri Kuu ya Chaumma imewateua Mwalimu kuwa Katibu Mkuu, Devotha kuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti Bara, na Kigaila kuwa Naibu Katibu Mkuu – Bara.
Mwananchi limezungumza na kigogo mwandamizi wa Chaumma ambaye naye anashangaa jinsi wanachama hao wapya walivyokuwa na fedha na hawajui wanazipata wapi, kwani kila kitu kwenye vikao vyao wamevigharamia.
“Yaani hawa jamaa wamegharamikia vikao vyetu vyote, cha Kamati Kuu, Halmashauri Kuu pamoja na huu mkutano wa kuwapokea. Chaumma ya jana si ya leo tena,” amesema kiongozi huyo na kuongeza:
“Tumeulizauliza hizi hela mmepata wapi, majibu hayaeleweki. Wanachotuambia tutulie wakisuke chama na twende kwenye uchaguzi, na wala tusiwe na wasiwasi katika hilo.”
Kwa nyakati tofauti tangu wajumbe hao wa sekretarieti watangaze kuondoka, viongozi mbalimbali wa Chadema na wanachama wao wamekuwa wakiwatuhumu wanaohama kuwa wamenunuliwa “wamefika bei” kwa maslahi yao binafsi.
Mei 8, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema – Bara, John Heche, akihutubia mikutano ya kampeni ya No Reforms, No Elections katika wilaya za Kyerwa na Karagwe mkoani Kagera, aliwashukia waliohama, akidai wamefika bei baada ya kupokea ahadi ya nafasi za uongozi, fedha, na vifaa vya kampeni katika uchaguzi mkuu ujao.

“Tuna taarifa kuwa baadhi ya walioondoka wamepata ahadi ya kusaidiwa kifedha na vifaa yakiwemo magari na pikipiki ili wagombee ubunge. Sasa wajiulize, iwapo kweli watashinda baada ya kuhamia vyama vingine kwa sheria na mfumo huu huu, kama hawakuweza wakiwa Chadema, chama kinachoungwa mkono na Watanzania wengi,” alisema Heche.
‘Tunajua fedha zinapopatikana’
Leo Jumatano, Mei 21, 2025, Mwananchi limezungumza na Mrema na Kigaila juu ya mijadala na maoni ya watu, nani yupo nyuma yao? Kigaila amewajibu wanaohoji gharama za sherehe hizo, akidai wanajua fedha zinakopatikana.
“Kwanza niwajibu wanaohoji fedha nimetoka nazo wapi? Kwani walidhani wakati tunatoka Chadema tulikuwa hatujui fedha zinapatikana wapi? Itoshe kusema wadhamini waliokuwa wakitusaidia tulikotoka, tumekuja nao huku,” amesema.
Kigaila amesema amekaa Chadema kwa miaka 21 akikijenga, hivyo anajua fedha za kukiendesha chama alikokuwa akipata na haishangazi wao kuandaa shughuli zilizofanyika.

Hali ya ilivyokuwa katika hafla ya Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimepokea wanachama wapya zaidi ya 3,000 waliokihama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
“Waliokuwa Chadema sasa hivi wamebadilika wamekuja Chaumma. Mnashangaa nini? Kwani Chadema hawakuwahi kuwa na mikutano ya namna hii? Na je, waliwahi kuulizwa fedha wanazitoa wapi?
“Lazima ijulikane, viongozi waliokuwa Chaumma hawakuwa na fedha, lakini tuliokuja tumekuja na wadau, wadhamini, na watu wenye kujua kuchangishana,” amesema na kuongeza;
“Tuna uwezo wa kuchangisha. Wakati viongozi wa Chadema walifungwa Kisutu, aliyebaki nje nilikuwa mimi pekee. Tulitakiwa kutoa Sh milioni 450, tulitangaza watu wakachanga, tukalipa viongozi walitoka. Nani aliuliza fedha tulitoa wapi?”
“Hatuwezi kushindwa kuchangisha fedha za kulipa ukumbi huu kwa gharama ya Sh milioni 6. Maandalizi ya mikutano hii tulianza mara tu tulipotangaza kuihama Chadema. Tulishasema hatustaafu, tunaandaa jukwaa lingine, ndilo hili.”
Kwa upande wake, John Mrema, mmoja wa viongozi waliokuwa wakiumba kundi la G55, amesema ni kweli kuna wadhamini wanaowasaidia.
“Kwanza, wakati tunajiandaa kuhama, tulikuwa tunajua demokrasia ni gharama. Ni kweli wapo wadhamini waliotuchangia na wanaendelea kutuchangia, kama ambavyo walikuwa wanafanya miaka ya nyuma tulikokuwa, wanachangia kwa sababu wanajua umuhimu wa jambo hili,” amesema.
Wakati wakieleza hivyo, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema shughuli zote ziligharamiwa na kundi la G55, lakini wao walikuwa wanakaribishwa kama wageni.
“Tangu mikutano iliyofanyika Golden Tulip na hapa Ubungo Plaza, kila jambo wamefanya wao, pamoja na gharama za kulipa wajumbe kutoka mikoani na posho zao, wao wanajua,” amesema.
Mjumbe huyo kutoka Mkoa wa Songwe amesema walilipiwa gharama za nauli za kuja Dar es Salaam na kurudi. Mathalani, yeye alilipwa Sh226,000- Sh126,000 kwa ajili ya nauli (Sh63,000 kwenda na kiasi kama hicho kurudi) na Sh100,000 kwa siku kwa ajili ya malazi. Gharama hiyo ni kwa wajumbe wote wa Halmashauri Kuu kutoka kila mkoa wawili– Katibu na Mwenyekiti.
Johnson Mbaga, kada aliyepokelewa kwenye sherehe hiyo akitokea Mkoa wa Kilimanjaro, amesema uongozi wa chama hicho uliwakodishia mabasi manne ya kuwabeba na kuwarudisha.
“Tumeletwa kutoka Kilimanjaro. Tulikuwa na mabasi manne na baada ya kuja hapa, kila mmoja amepewa Sh10,000 fedha ya kula. Na baada ya mkutano, tunarudishwa kwa mabasi yaliyotuleta,” amesema Mbaga.
Alipoulizwa kuhusu gharama hizo, Mrema amesema hawakuwa wajumbe wengi, bali 64 pekee, hivyo hakikuwa kiwango kikubwa, kwani kuna baadhi ya mikoa nafasi zake hazijajazwa.
Tunakwenda kuzindua C4C
Anachokisema kiongozi huyo kinapewa nguvu na Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Salum Mwalimu, ambaye katika mkutano wa kuwapokea, amewaambia kuwa Mei 30, 2025, wanakwenda kuzindua Operesheni C4C (Chaumma for Change) jijini Mwanza, itakayofanyika kwa siku 16.
“Tunakwenda kuzindua Operesheni ya C4C chopa juu kwa siku 16 kuwaambia Watanzania msihofu, tuko tayari kubeba gharama zenu. Mashine ziko tayari, mitambo yote iko tayari. Kaeni tayari, tunakuja!
“Tutaweka wagombea katika majimbo yote 264 na manane yaliyoongezwa. Tukatetee maslahi ya wananchi na kwenda kuwasemea. Tunakwenda kushiriki uchaguzi kwa kishindo, tena kwa kishindo kweli kweli,” amesema na kuongeza;

“Wale wote wenye nia ya kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia Chaumma, watangaze nia zao, na karibuni. Tutatoa utaratibu wa namna gani nia zao zitapokelewa,” amesema.
Mwalimu, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu – Bara wa Chadema kati ya 2014–2025, amesema hana shaka na ukuaji wa chama hicho, akieleza kuwa wana watu sahihi, wenye maarifa ya namna ya kukijenga kuwa chama kikuu nchini.
“Ninapotoa maelekezo ya kwenda kukisuka chama hiki, ninatoa kwa kujiamini kweli kweli. Ndani ya mwezi mmoja naamini mtaona Chaumma ikiimbwa kila mtaa, kata, jimbo, wilaya, mkoa—hadi Taifa zima. Sina chembe ya shaka kwa sababu tunayo kiu ya kweli ya kufanya hivyo, ile ile kiu ya miaka 10, 15 au 20 iliyopita,” amesema Mwalimu.
Amesisitiza kuwa matumaini hayo yanatokana na ukweli kwamba wananchi wengi wamechoshwa na utawala wa CCM, hivyo wana hamasa ya kweli ya kutafuta mabadiliko kupitia vyama mbadala.
Alichokisema Rungwe
Awali, akifungua mkutano huo, Rungwe amesema hakuna maendeleo ya kweli katika Taifa linalokabiliwa na changamoto ya lishe duni, akisisitiza kuwa msingi wa Taifa imara ni wananchi wenye afya bora.

“Taifa ambalo halina lishe, hakika halitaweza kuendelea. Ndiyo maana sisi Chaumma tunaamini ili kujenga Taifa madhubuti na lenye watu imara ni lazima tuhakikishe wanapata lishe madhubuti tangu wakiwa watoto.
“Huwezi kujenga taifa imara kama watu wake wanakuwa na shida ya utapiamlo. Ndiyo maana halisi ya kaulimbiu yetu ya ‘Ubwabwa kwa wote.’ Karibuni tukajenge Taifa lililoshiba na lenye afya njema,” amesema Rungwe.
Kiongozi huyo amewakaribisha wanachama hao wapya waliotangaza kujiunga, akisisitiza umuhimu wa kujenga chama imara kitakachoweza kushindana kwa hoja na CCM.
“Nawakaribisha sana, twendeni tukajenge chama ambacho kitashindana na kukabiliana na CCM kwa hoja madhubuti. Nina hakika kwa umoja wetu tutawashinda katika uchaguzi ulio huru na haki.
“Nawakaribisha wanachama wapya, tukapambane kwa hoja ili tupate mabadiliko ambayo yatalipeleka Taifa letu kufikia na kuishi misingi ya kuundwa kwa chama chetu,” amesema Rungwe.