
MANCHESTER, ENGLAND: ‘TUNAAJIRIWA ili tufukuzwe’. Hii ni kauli ya makocha wote hasa kwenye soka. Wanaamini wanaajiriwa ili wafukuzwe. Na kweli, mabosi wengi wa klabu za soka hawana dogo pale wanapoona mambo hayaendi na mara moja hufanya maamuzi makubwa ya kutimua kocha.
Ni makocha wachache zasa ambao wameondoka kwenye timu zao bila ya kufukuzwa. Kwa kumaliza mikataba wakiwa na mafanikio, waliomaliza muda wao na kustaafu na wanaoamua kuachana na timu kwa sababu nyingine maalumu.
Hata hivyo, wakiwa kwenye kazi yao hiyo, wengi huwa na presha ya kufukuzwa kutokana na matokeo mabovu na mwenendo wa timu, kama kilichomkuta Erik ten Hag akiwa Manchester United.
Kilichomwondoa Ten Hag ni matokeo mabovu ya Man United na hadi anaondoka aliiacha timu nafasi ya 14 huku akiondoka na kipigo kutoka kwa West Ham katika mchezo wake wa mwisho kusimamia.
Hata hivyo, siye pekee ambaye alikuwa amekalia kuti kavu, wapo makocha kwenye Ligi Kuu England, wanasubiri panga zipite shingoni na muda wowote wanakatwa kutokana na viwango vibovu vya timu zao msimu huu na kwenye safu hii ya Top 5, tunakuwekea makocha watano ambao wanachungulia mlango wa kutokea.
5. Gary O’Neil
Kocha wa Wolves. Ni mmoja wa makocha wawili wanaosaka ushindi wa kwanza kwenye vikosi vyao msimu huu.
Msimu wake wa kwanza, Wolves, O’Neil alifanya vizuri na alimaliza nafasi ya 14. Hata hivyo, mambo ni magumu msimu huu na hadi sasa kwenye msimamo iko nafasi ya mwisho (mkiani) na pointi tatu ilizokusanywa katika sare tatu huku mechi saba akipoteza na imecheza 10.
Huenda akawa mmoja wa makocha watakaofuata nyayo za Ten Hag kwa sababu kila siku timu inaonekana kuzidi kushuka kiwango na mchezo ujao itacheza dhidi ya Southampton na kuna uwezekano mkubwa akafungashiwa virago ikiwa atapoteza.
4. Russell Martin
Kocha huyu anaheshimiwa sana na mabosi wa Southampton kutokana na alichokifanya msimu uliopita kwa kuiwezesha kupanda daraja ikiwa ni msimu mmoja tangu iliposhuka.
Saints iliyopanda Ligi Kuu kutokana na mechi za mtoano, imepata tabu tangu kuanza kwa msimu huu na imeshinda mechi moja na kutoa sare moja katika mechi 10.
Mchezo pekee ilioshinda ni dhidi ya Ipswich, ambao pia wamepanda daraja hivi karibuni. Mchezo ujao dhidi ya Wolves unaweza kuwa na majibu juu ya hatma ya kibarua cha Russel kwa sababu Southampton haitaki kurudi tena Championship msimu ujao.
3. Oliver Glasner
Wakati anapewa kazi alitabiriwa angeiwezesha Crystal Palace kufuzu michuano ya Ulaya msimu ujao, lakini mambo yamekuwa tofauti.
Timu hiyo imekuwa katika kiwango kibovu msimu huu ikiwa nafasi ya 17 kwenye msimamo baada ya kushinda mechi moja na kutoa sare nne katika mechi 10 ilizocheza hadi sasa.
Imekuwa ni tofauti na msimu uliopita, hata staili yao ya kucheza ilikuwa inavutia ikiwa na nyota kama Eberechi Eze, Marc Guehi na Michael Olise na kusababisha timu nyingi kubwa kuwahitaji na hatimaye baadhi kuuzwa.
Ushindi wa hivi karibuni mbele ya Tottenham unadaiwa kupunguza presha lakini bado ajira ya kocha huyu ipo hatiani na katika mchezo ujao dhidi ya Fulham akipoteza hali ya kuilinda ajira yake inaweza kuzidi kuwa mbaya.
2. Julen Lopetegui
Mashabiki wengi walitarajia makubwa kutoka kwake kutokana na ukubwa wake na historia aliyoiweka katika timu mbalimbali alizowahi kufundisha.
Lopetegui ambaye amewahi kushinda Europa League akiwa na Sevilla, alifanya vizuri pia katika kikosi cha Wolves kabla ya kuondoka msimu uliopita baada ya kugombana na bodi ya timu hiyo.
West Ham walihisi walipata samaki mkubwa walipomwajiri kumrithi David Moyes. Usajili wa wachezaji wengi wakubwa ulifanywa lakini West Ham wameikuta katika nafasi ambazo hawakuzitarajia.
Hadi sasa imeshinda mechi tatu tu, kati ya 10 ikiwa inashika nafasi ya 14 kwa pointi zao 11.
Kuna uwezekano maamuzi magumu yakanyika kufikia Desemba mwaka huu juu ya Lopetegui kutokana na kutofikia matumaini yaliyowekwa kwake.
1. Kieran McKenna
Aliwahi kuhusishwa na timu mbalimbali kubwa za England baada ya kuipandisha daraja Ipswich lakini akaendelea kuifundisha timu hiyo.
Ameisaidia Ipswich kupanda daraja kutoka Ligi Daraja lapili hadi la kwanza na baadae Ligi Kuu lakini hali inayoendelea huenda akawarudisha tena Daraja la kwanza.
Inaelezwa mabosi wa Ipswich wanaangalia uwezekano wa kumbadilisha baada ya timu hiyo kutoshinda mechi yoyote kati ya 10 za mwanzo tangu kuanza kwa ligi msimu huu huku ikishika nafasi ya 18 kwa pointi zao tano