Nani kasema kitanda hakizai haramu?

Canada. Kuna imani kuwa kitanda hakizai haramu. Uzoefu wetu unaonyesha kuwa kitanda kinazaa haramu japo huhalalishwa kwa visingizio mbalimbali kama mila, ujinga na ubutu wa teknolojia.

Ujio wa kipimo cha DNA unaonyesha kuwa kitanda kinazaa haramu tu.  Kusema kitanda hakizai haramu ni uchafu kimila.

Ni hatari, majuto, na makosa makubwa kwa wasioamini wala kukubali uchafu huu kuoa au kuolewa kwenye makabila haya. Kwani, hawana uwezo wa kudumisha mila.

Tuanze na mfano wa Jerome (si jina lake) ambaye anathibitisha kuwa kitanda kinazaa haramu. Jerome ana siri iliyojificha kwenye mila chafu za kujamiiana ndugu kwani, anafanana na babu yake kuliko baba yake.

Pia, kuna minong’ono kuwa mama yake alipewa mimba na baba mkwe. Siyo siri tena kwa wanaomjua.

Kisa kingine ni cha Giloli (si jina lake) binti anayetoka kabila moja na Jerome. Tofauti, yeye ni mtoto wa kaka wa baba yake aliyezaliwa kwenye ndoa.

Siri ya Giloli ilifichuka alipopata mchumba. Naye, hafanani na baba yake bali baba mkubwa. Alipochumbiwa, mchumba aliambiwa apelekwe kutambulishwa kwa baba mkubwa.

‘Baba’ yake aliishi mbali. Wanaojua, waling’amua na kufumbua fumbo lilojificha miaka mingi.

Jerome na Giloli wanatoka kwenye kabila lenye utamaduni wa kuchukuana ndugu kwa ndugu. Je katika jamii zetu wapo wangapi? Tafakari.

Wakati ukitafakari, ujiulize. Ni watoto wangapi hufanana na baba zao wakubwa, wadogo hata wajomba hata majirani uliowahi kusikia habari zao?

Akiwa bungeni, Profesa Palamagamba Kabudi, aliwahi kuwasihi Watanzania wasipime DNA za watoto wao.Huu ni ushahidi wa kwanza kuwa kuna Jerome wengi kuliko unavyoweza kufikiria.

Kuna makabila na watu wenye tabia ya kuzaa watoto nje ya ndoa wakiwa katika ndoa au nadhiri hasa makasisi.

Pia, zipo jamii zilizokubali na kuhalalisha jinai hii ambayo ni hatari kwa watoto na waliobambikiziwa. Katika makabila haya, watu hawa wako wengi, wanajulikana, na wengine wanakubalika chini ya dhana chafu ya kitanda hakizai haramu.

Nini sababu?

  Je jinai hii husababishwa na nini? Kimsingi, zipo sababu nyingi kama vile ukosefu wa uaminifu katika ndoa, mila mbovu, tamaa, kutoweza kupata watoto wa jinsi fulani kwa baadhi ya wanandoa, kubakwa, uzinzi, na mengine mengi.

Mila mbovu za ndugu kuchukuana ni chanzo kikubwa. Mfano, kuna makabila ambapo ndugu huchukuana kama mbuzi au panya bila kujali au kujua madhara ya kufanya hivyo.

Je utawajuaje? Utasikia kila baba anayekuja nyumbani ni ‘anko.’ Huu ‘uanko’ unaficha mengi.  Kuna makasisi wana watoto waliozaa na mahawara wao ambao huitwa anko na watoto wao wenyewe wa kuzaa.

Watu na makabila haya yapo na yanakubali mila na tabia hizi chafu kama vile watoto wa babu na bibi mmoja kuchukuana na hata wengine kuoana.

Huyu anamchukua mtoto wa baba mdogo, mjomba, shangazi, na wengine hata kuchukua wapwa zao ilimradi ‘wadumishe mila.’

Pia, kuna makabila yanayogeuza ndoa mali ya ushirika kwa kuruhusu baba mkwe au shemeji kumrithi mjane. Kama kurithi wajane ni jambo la kawaida, inashindikanaje wahusika kuchukuana hata kupeana mimba hata kabla ya kufiwa.

Ikitokea mtu atokaye kwenye jamii isiyokubaliana na mila hizi chafu kuoa au kuolewa katika jamii hizi, lazima ataumizwa.

Pia, watoto watokanao na dhambi hii huathirika kisaikolojia hata kiuchumi. Mfano mtoto ambaye baba yake halisi siyo mume wa mama yake, hawezi kumjua au kumfaidi mzazi wake.

Hivyo, kijamii, anakuwa ametenganishwa na mzazi wake halisi na kuunganishwa na mzazi bandia. Pia, inapotokea mzazi wake ana mali, hana uwezo wa kumrithi ukiachia kutowajua au kukua na ndugu zake. Pia, inapobainika, uwezekano wa kuvunja ndoa ni mkubwa.

Hamjasikia visa vya baadhi ya wanaume kuua watoto wasio wao au wanandoa wanaoua wenzao wagunduapo wamebambikiwa watoto? Je hapa kitanda hakijazaa haramu na jinai?

Je, nini kifanyike kuepuka unyama na utapeli huu? Tunashauri jamii zisifumbie macho jinai hii. Badala yake, tuelimishane madhara ya jinai hii kuepusha mateso kwa watoto, talaka, na vifo vyao hata wazazi wao. Hakika, kitanda kinazaa haramu. Kuweni macho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *