Namna ya kuvunja mzunguko wa kuishi mshahara kwa mshahara

Namna ya kuvunja mzunguko wa kuishi mshahara kwa mshahara

Kuishi kutoka mshahara hadi mshahara ni mzunguko wa kuchosha unaowatega mamilioni ya watu wanaofanya kazi kwa bidii katika hali ya sintofahamu ya kifedha. Kila mwisho wa mwezi unahisi kama kusubiri kufikia sufuri, ukisubiri mshahara mwingine ili kuendelea kuishi.

Licha ya kufanya kazi kwa saa nyingi, au hata kushikilia ajira zaidi ya moja, pesa huonekana kutoweka haraka kama ilivyoingia. Lakini kuvunja mzunguko huu inawezekana, na kunaanza kwa mabadiliko ya fikra na mazoea bora ya kifedha.

Elewa mzunguko wa mshahara

Maisha ya mshahara kwa mshahara yanamaanisha kuwa kipato chako kinatosha tu kugharamia matumizi ya kila mwezi, huku ukibakiwa na kidogo au hakuna kabisa cha kuweka akiba.

Hali hii huacha pengo kubwa kwa dharura, haina nafasi ya kupumua, na hukosa mwelekeo wa uhuru wa kifedha wa muda mrefu.

Watu wengi hujikuta kwenye mzunguko huu si kwa sababu ya uvivu au uzembe, bali kwa sababu hawajawahi kufundishwa misingi ya kupanga bajeti, kuweka akiba, na kupanga vipaumbele vya matumizi.

Jua pesa yako inapoenda

Hatua ya kwanza na muhimu zaidi ya kudhibiti fedha zako ni kufuatilia matumiziyako. Huwezi kurekebisha kile usichokielewa. Kwa angalau siku 30 mfululizo, andika kila matumizi yako, hata yale madogo kabisa.

Hii inajumuisha kodi ya nyumba, bili za umeme, nauli, vocha za simu, vitafunwa, data, au matumizi ya wikendi. Tumia daftari rahisi, programu ya bajeti, au jedwali la Excel kupanga matumizi hayo katika makundi matatu: Mahitaji (kodi, chakula, usafiri, dawa), Matamanio (burudani, chakula cha haraka, nguo zisizo za lazima), na akiba au kulipa madeni.

Mara unapopanga haya yote kwa uwazi, unaweza kushangaa kugundua ni kiasi gani cha fedha kilikuwa kinapotea kupitia mianya midogo hasa kama vile vocha ndogondogo, maagizo ya chakula yasiyopangwa, au vifurushi vya simu usivyohitaji.

Linganisha kodi ya nyumba na kipato chako

Hatua nyingine muhimu ni kutathmini kiasi cha kipato chako kinachotumika kulipia kodi ya nyumba. Fanya hivi kwa kugawanya kodi yako ya kila mwezi kwa kipato chako cha jumla, kisha zidisha kwa 100 kupata asilimia.

Kwa mfano, kama kipato chako ni Sh800,000 kwa mwezi na kodi ni Sh300,000, basi asilimia inayotumika kwa kodi ni 37.5. Hii ni juu ya kiwango kinachopendekezwa na wataalamu wa fedha.

Kitaalamu, kodi haipaswi kuzidi asilimia 30 ya kipato chako cha jumla kwa mwezi. Zaidi ya hapo, kuna hatari ya mkazo wa kodi ambao unaweza kuathiri uwezo wako wa kugharamia mahitaji kama chakula, usafiri, akiba, au madeni.

Ikiwa kodi inakula sehemu kubwa ya kipato chako, zingatia kupunguza ukubwa wa nyumba, kuhama eneo la bei nafuu, kuishi na watu wengine kugawana gharama, au kujadiliana na mwenye nyumba kupunguza kodi. Kudhibiti gharama za makazi ni msingi wa ustawi wa kifedha wa muda mrefu.

Tengeneza bajeti halisi

Baada ya kufuatilia matumizi yako, tengeneza bajeti inayolingana na hali halisi ya kipato chako – si ndoto. Njia maarufu ya kupanga bajeti ni kanuni ya 50/30/20, ambapo: asilimia 50 ya kipato chako huenda kwa mahitaji, asilimia 30 kwa matamanio, na asilimia 20 kwa akiba au kulipa madeni.

Hata hivyo, kama kipato chako ni kidogo au hakina uhakika, unaweza kurekebisha asilimia hizi. Hata kuokoa asilimia 5–10 ya kipato chako kila mwezi kunaweza kuleta mabadiliko makubwa kadri muda unavyopita.

Lengo ni kutoa kipaumbele kwa matumizi muhimu huku ukitambua maeneo unayoweza kupunguza, kama usajili usiotumika, ununuzi wa ghafla, au usafiri wa gharama kubwa.

Anza akiba ya dharura

Watu wengi wanabaki kwenye mzunguko wa mshahara kwa sababu hutegemea mikopo au kuomba mshahara wa mapema kila dharura inapotokea.

Anza kujenga akiba ya dharura, hata kama ni Sh20,000 kwa mwezi. Hifadhi fedha hizi kwenye akaunti tofauti ili usishawishike kuzitumia. Hii itapunguza utegemezi wa mikopo na kukuongezea amani ya kifedha.

Kabiliana na madeni kwa mkakati

Madeni yenye riba kubwa kama mikopo ya simu au kadi za mkopo huzidisha mzigo wa kifedha. Andika orodha ya madeni yako yote, anza na lile lenye salio dogo au lenye riba kubwa zaidi.

Tumia mbinu ya “snowball” (anza na deni dogo) au “avalanche” (anza na riba kubwa). Ukishamaliza deni moja, elekeza kiasi hicho kwenye akiba au deni lingine. Epuka kukopa upya isivyolazima, na ukihitaji, jadiliana upya masharti au fanya muunganiko wa madeni ili yafaa hali yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *