
Wagonjwa wa kisukari wanaokabiliwa na matatizo ya ulemavu na wanatakiwa kupunguza uzito, wanahitaji mpango maalumu wa kupungua uzito wa mwili kama walivyoshauriwa.
Kupunguza uzito ni muhimu kwa kudhibiti viwango vya sukari na kupunguza hatari ya matatizo mengine yanayohusiana na kisukari.
Hata hivyo, njia zinazotumika lazima ziwe salama na zinazowezekana kwa hali yao, pasipo kusababisha sukari kushuka mara kwa mara.
Kuwa na mpango lishe bora kwa maana ya kuchagua vyakula vyenye afya. Vyakula vya wanga kama vyenye nyuzinyuzi nyingi ambavyo ni matunda, mboga, nafaka kamili kama vile shayiri, uwele, mtama, mahindi na ngano ambayo haijakobolewa.
Ulaji wa vyakula vya wanga hautakiwi uwe wa kiasi kikubwa, kipimo ni sawa na ngumi moja ya mgonjwa wa kisukari, ni vyema kwa kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu na kusaidia katika udhibiti wa uzito.
Protini kama samaki, kuku, maziwa, maharage na mayai hutoa protini bila kuongeza mafuta yasiyohitajika. Protini husaidia katika kudhibiti hisia za njaa na inaweza kusaidia katika kudumisha misuli.
Vyakula vilivyopikwa kwa mafuta ya mimea kama yale ya olive, parachichi, ubuyu na alizeti. Haya mafuta ni mazuri zaidi kwa wenye kisukari kwa sababu hayana lehemu, lakini pia hayatakiwi kutumika kwa kiasi kikubwa kwenye chakula.
Mboga za majani zina umuhimu mkubwa katika kupunguza uzito na kudhibiti viwango vya sukari kwa sababu ya faida zake nyingi.
Mboga za majani zina kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi, ambazo ni muhimu kwa kudhibiti uzito na viwango vya sukari.
Nyuzinyuzi huboresha mmeng’enyo wa chakula na pia hurahisisha upatikanaji wa haja kubwa na husaidia katika kupunguza tatizo la kukosa choo. Mboga za majani zina viwango vya chini vya sukari na kalori, ambazo ni muhimu katika kudhibiti viwango vya sukari.
Mboga za majani ni vyanzo bora vya virutubisho muhimu, madini na vitamini, kama Vitamini A, C, K na folate pamoja na madini kama chuma, potasiamu na magnesiamu, yote yanayosaidia katika kuboresha afya kwa jumla na kuimarisha mfumo wa kinga.
Mboga nyingi za majani zina viambato vya antioxidant vinavyosaidia kupigana na uharibifu wa seli na hivyo kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa.
Vinywaji vingine vinavyoweza kusaidia katika kupunguza uzito na kudhibiti viwango vya sukari ni pamoja na chai ya kijani na chai ya mnana. Chai ya kijani ina viambato vya antioksidanti vinavyoitwa catechins, ambavyo vinaweza kuongeza kasi ya kimetaboliki.