
Ramadhani ni mwezi mtakatifu kwa waumini wa dini ya Kiislamu, ni wakati wa kutafakari kwa kina, kuepuka vitendo viovu, na kudumisha umoja wa kifamilia na kijamii. Vilevile ni kipindi cha kufunga, kuomba, na kufanya matendo ya hisani. Hata hivyo, wakati wa kuendea yote hayo, familia nyingi pia ni kipindi hiki zinapambana na kuongezeka kwa gharama za matumizi kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya nyumbani.
Katika mwezi huu Ingawa hakuna mlo wa mchana, lakini matumizi ya chakula kwa mlo wa kawaida wa familia yanaongezeka, mfano uandaaji wa mlo wa jioni “futari” na chakula cha alfajiri kabla kupambazuka :daku”, na mengine, inaongeza gharama za chakula ukilinganisha na matumizi ya siku za kawaida.
Mathalan, utamaduni wa ulaji unachangia, kwa kawaida futari haiwi chakula kimoja, kwa mfano, ukichukua familia yeyote Magomeni, Ilala Dar es Salaam, au Barabara 7 kule Tanga mjini aghalabu utakuta meza ya futari ina mihogo, mandazi, vitumbua, mengine. Kuwepo aina za vyakula ambao ni mtindo wa ulaji wa Ramadhani, inamaanisha pia kuongeza matumizi ili kuweza kupata yote hayo. Hivyo si ajabu gharama kupanda.
Sambamba na hilo, kutokana kudumisha umoja na matendo ya hisani, ni ngumu pia kwa familia kuandaa chakula chao binafsi, kwa sababu matendo kama kutoa sadaka kwa jamii, kuwakaribisha wageni katika mlo wa pamoja yanahimizwa na mafundisho ya Kiislamu katika mwezi huu, na yanashamiri, hivyo, katika kuyakidhi yote hayo, inapelekea kuongeza gharama za bajeti ya matumizi kwa familia husika.
Vilevile, kupaa kwa bei za vyakula zimepaa katika sehemu mbalimbali za masoko zinaongeza makabiliano ya familia kumudu mahitaji ya msingi. Vyakula vikuu kama mchele, unga, sukari, viazi na vingine si ajabu kuona bei zimepanda katika msimu huu kutokana wa mahitaji kuwa mengi hivyo biashara wa mitaani na wauzaji katika masoko wanatumia fursa hiyo kupata faida ya ziada.
Changamoto zinawapata kwa familia za kipato kidogo, kuendana na kila hitaji la Ramadhani familia inaweza kujiweka katika hali ngumu ya kuweza kumudu matumizi. Katika muktadha kama huu, na kama inavyohimizwa katika maelekezo kuishi wa kiasi, na kuepuka israfu.
Ukweli ni kwamba haipunguzi chochote katika malipo ya saumu kwa kula vyakula kama uji, mihogo, viazi kama huna uwezo wa kumudu sambusa, chapati na michuzi ya nyama. Familia zijipatie mahitaji kwa kiasi cha uwezo wao na hakuna ulazima wa kujifananisha na wengine.
Vilevile, desturi ya kushirikiana kwa Jamii katika milo ya pamoja inaweza kuimarishwa na kuendelezwa kupunguza gharama za matumizi na kwa kugawana majukumu. Ingawa jambo hili si rahisi kwa kutokana na mtindo wa maisha wa maeneo ya mijini, lakini pembezoni mwa miji, vijijini, majirani wanaweza kuandaa futari za pamoja na kusaidia kupunguza gharama.
Hali kadhalika, kwa mashirika ya kijamii, watoa misaada, vituo vya misikiti, na kwa wenye uwezo wanaweza kutumia majukwaa hayo kujitolea kwa ajili ya kufadhili programu za kutoa futari na misaada mbalimbali ya kiutu kama inavyofanyika katika maeneo mengine ili kila familia iweze nayo kufurahia wasaa huu.
Ramadhan ni wakati wa kujisafisha kiroho, na isionekane kuwa ni mzigo wa kifedha. Familia zitimize wajibu wao wa kidini, kuimarisha ushirikiano wa jamii, na isijitwishe ulazima wa kuishi wa kifahari ikiwa haina uwezo huo.