
Dar es Salaam. Hoja tatu zimeibuka baina ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku wajumbe wakionywa kutobadili jenerali katikati ya vita.
Hoja hiyo imejibiwa kwa kuhoji uwezo wa jenerali mwenyewe ndani ya uwanja wa vita.
Hoja zingine ni ili chama hicho kiendelea kuwa imara kinahitaji mgombe kama Charles Odero anayeweza kuleta usuluhishi na nguvu mpya.
Nyingine ikielezwa chama hicho kinahitaji jenerali mpya mwenye msimamo atakayetoa kauli iliyonyooka na kuaminiwa na wanachama.
Hoja hizo kwa nyakati tofauti zimeibuliwa usiku wa leo Jumatano, Januari 22, 2025 na wagombea hao wakati wakijieleza mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu kujaribu kuwashawishi wawapatie kura za kuwawezesha kujishinda nafasi hiyo huku wakipigwa maswali na wajumbe hao.
Nafasi hiyo inayowaniwa na wagombea watatu, Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo, makamu wake bara, Tundu Lissu na Charles Odero ambaye muda mwingi alikuwa akijinasibu jukwaani kwamba hajaja kugombea nafasi hiyo kwa bahati mbaya.
Alichokisema Mbowe
Mbowe ndiye amekuwa mgombea wa kwanza kupanda ulingoni kujieleza akianza kwa kusema Chadema imetoka safari ndefu na sasa Taifa linajivunia uwepo wa chama hicho ambacho si tu kimekuwa kikuu cha upinzani bali chama makini.
Mbowe amesema mafanikio hayo ni kutokana na kazi makini waliyoifanya wakati wa uongozi wake licha ya changamoto walizozipitia wameweza kuifikisha Chadema hapo kilipo sasa na kuna kazi inayopaswa kufanyika.
Katika uongozi wake, Mbowe amesema wamefanya mambo mengine ya kukiheshimisha chama hicho akitoa nguvu akili na muda wake kukijenga chama hicho akisisitiza haamini kama kuna mtu atabeza mchango wake ndani ya chama hicho
Amesema katika huduma yake ndani ya Chadema ameibua vipaji ambavyo sasa vinahudumu ndani ya chama hicho na vyama vingine.
“Tunahitaji uzoefu nguvu na kujitoa pasipo na mawaa, nimejitoa kwenye chama hiki sasa ndugu zangu msiijaribu sumu kwa kuionja.
“Tunakwenda kwenye uchaguzi lazima tujipange na uchaguzi huo na kukirejesha heshima ya chama iliyoibiwa, ndugu zangu wanachadema hakuna kosa mtakalolifanya kama kubadilisha jenerali katikati ya vita,” amesema.
kufuatia swali hilo la kutobadilishwa jenerali vitani kuliibuka swali kwa wajumbe wakihoji kama haitakuwa sahihi kuiondoa CCM katika ya vita.
Swali hilo Mbowe amelijibu akisema akipewa nafasi ya kukiongoza chama hicho ataendelea kukijenga chama hatua kwa hatua akisisitiza katika hoja yake hakuwa na maana ya CCM katika msingi wa swali lake.
Kuhusu swali lingine la kama mgombea huyo ana fikra mpya za kusimamia rasilimali za chama, Mbowe amesema akiwa gerezani mwaka 2019 ndipo alikutana na mtaalamu wa kompyuta na kubuni mfumo huo bila kutumia ruzuku ya Serikali.
Amesema alitamani mfumo wa Chadema digitali uende kwa kasi lakini changamoto zilijitokeza ikiwemo kukosa mashine mbalimbali na hata hivyo tayari vifaa vimesambazwa maeneo mengi nchini.
Alivyosema Odero
Kwa upande wake mgombea Charles Odero, amesema nguvu kubwa aliyotumia kushinikiza serikali kusitisha tozo kwenye miamala ya simu inatosha kwa wajumbe hao kumuamini kushika nafasi anayoomba.
“Nikichaguliwa nitakwenda kuimarisha misuli ya uchumi kupitia dijitali, na tupo kwenye wakati ambao tunahitaji mtu mpya mwenye fikra mpya ili kufanya mabadiliko yanayohitajika,” amesema Odero.
Amesema kuwanyima Mbowe na Lissu kura ni jambo jema katika kukinusuru chama kwani yeye ndiye msuluhishi na mponyaji wa changamoto zinazokikumba chama hicho ikiwemo kushinda chaguzi zinazokuja.
“Sijaja hapa na kugombea nafasi hii kwa bahati mbaya ila nipo kimkakati katika kukinusuru chama hiki kwa kupambana na makovu na dhoruba kinazopitia,” amesema Odero
Alicholisema Lissu
Kwa upande wa Lissu ameanza sera zake kwa kueleza alivyokitumikia chama hicho tangu miaka 20 iliyopita na kwamba asingetamani kuwaeleza wajumbe kila nafasi aliyowahi kuishika.
Ameeleza wajumbe wanapaswa kuamua mitano tena ili iwe 26 italeta chochote, au wachague mabadiliko.
“Hatuwezi tukaendelea kwa namna ambavyo tumekuwa katika mazingira ya sasa,” amesema.
Lissu amedai mwaka 2019 waliibiwa uchaguzi na 2020 walipata mbunge mmoja bila jenerali wao kufanya chochote.
Amesema wanapaswa kuamua kwenda na mbinu, fikra na mikakati mipya.
“Ni wakati wa kubadilisha majanerali, ni wakati wa mabadiliko,” amesema.
Baada ya wagombea hao kujieleza kila mmoja kwa stahili yake shughuli inayofuatia ni utaratibu wa kuanza kupiga kura.
Upigaji kura ulianza rasmi saa 8 usiku
Endelea kufuatilia Mwananchi
(Imeandikwa na Juma Issihaka, Tuzo Mapunda na Baraka Loshilaa)