Manchester. Jana Ijumaa, Aprili 04, 2025, kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne (33) aliwaaga mashabiki wa timu hiyo akifichua kuwa hatoongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo baada ya huu wa sasa kufikia kikomo Juni mwaka huu.
Kuondoka kwa Kevin De Bruyne kunahitimisha miaka 10 ya nyota huyo ndani ya Manchester City, klabu aliyoitumikia tangu Julai, 2015 ilipomsajili kutokea Wolfsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’.

Andiko la Kevin De Bruyne akiaga rasmi Manchester City.
De Bruyne anaondoka Manchester City akiwa ameacha kumbukumbu ya kipekee ambayo imeainishwa na namba sita tofauti.
Kevin De Bruyne anaondoka Manchester City akiwa ametwaa mataji 14 ya mashindano tofauti katika kipindi cha miaka 10 aliyoitumikia.
Kati ya mataji hayo 14, sita ni ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mengine ni ya Kombe la FA. Kombe la Carabao na Ngao ya Hamii.
Ni namba inayowakilisha kiasi cha fedha ambacho Manchester City ilikitumia kumnasa Kevin De Bruyne miaka 10 iliyopita akitokea Wolfsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga
Kiungo huyo alinunuliwa kwa dau la Pauni 55 milioni (Sh191 bilioni) ambapo alisaini mkataba wa kuitumikia Manchester City kwa miaka sita.
Kwa mujibu wa mtandao unaohusika na utoaji tathmini ya thamani za bei za wachezaji wa www.transfermarkt.com, kwa sasa thamani ya Kevin De Bruyne ni kiasi cha Euro 27 milioni (Sh79.6 bilioni) ikiwa ni anguko la zaidi ya nusu ya thamani ya fedha iliyotumika kumsajili mwaka 2015.
Hadi anatangaza kuwa hatoendelea kuitumikia Manchester City, Kevin De Bruyne amehusika katika mabao 280 ya timu hiyo kwenye mechi 413 alizoichezea za mashindano tofauti.

Kati ya mabao hayo 280 aliyohusika nayo, mabao 104 amepachika yeye mwenyewe na amepiga pasi za mwisho 176.
Namba 36 inawakilisha idadi ya kadi ambazo Kevin De Bruyne ameonyeshwa katika kipindi chote alichoitumikia Manchester City.
Kadi hizo zote ni za njano na hajawahi kuonyeshwa kadi nyekundu katika miaka yote 10 aliyodumu ndani ya timu hiyo.
Kevin De Bruyne kwa sasa analipwa mshahara wa pauni 400,000 (Sh1.4 bilioni) kwa wiki ndani ya Manchester City, fedha inayomfanya awe mchezaji wa 10 kwa kulipwa mshahara mkubwa duniani huku katika Ligi Kuu England akishika nafasi ya tatu nyuma ya Erling Haaland anayeongoza na Mohamed Salah anayeshika nafasi ya pili.