Naibu Waziri Mkuu wa Ubelgiji anaendelea na ziara yake katika maziwa makuu

Naibu waziri mkuu wa Ubelgiji pamoja na waziri wake wa mambo ya nje, wanaendelea na ziara yao kwenye eno la maziwa makuu kuhubiri amani, ambapo Jumapili ya wiki iliopita waliwasili jijini Kinshasa, baada ya kuzuru Uganda na Burundi.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Hii imekuwa ziara ya kwanza kufanywa na waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji kwenye eneo hili katika kipindi cha miaka 10, ziara yao ikilenga kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, mazungumzo ya kisiasa na usalama wa kikanda.

Mawaziri hao hivi leo watakutana kwa mazungumzo na rais Felix Tshisekedi.

Akiwa Bujumbura, waziri Maxime Prevot, alifanya mazungumzo na rais Evariste Ndayishimiye, ambapo walijadiliana kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili kiuchumi, kisiasa na usalama.

Aidha ziara yao pia imelenga kuzishawishi nchi za ukanda kudumisha amani hasa wakati huu mzozo wa mashariki mwa DRC ukitishia kuenea kwenye eneo zima.

Hata hivyo ziara ya viongozi hawa haitawapeleka nchini Rwanda, kutokana na nchi hizo hivi karibuni kusitisha uhusiano wao, kufuatia madai ya Kigali kuwa Brussels inaingilia masuala yake ya ndani kutokana na mzozo wa DRC.

Kwa muda sasa Ubelgiji imekuwa ikisisitiza kuwa njia pekee ya kutatua mzozo uliopo ni kwa pande zote kuheshimu uhuru wa mipaka ya kujitawala ya kila nchi, kurejea nyumbani kwa wakimbizi, kumalizwa kwa kundi la FDLR na nchi za kigeni kuondoa wanajeshi Wake kwenye ardhi ya Kongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *