Naibu Waziri ashauri vituo vya mafuta kutouza kwa pesa taslimu

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itafanya uchambuzi yakinifu ili kuona njia sahihi ya kupunguza matumizi ya pesa taslimu (cash) kwenye vituo vya mafuta kote nchini.

Mpango huo wa TRA umekuja kufuatia ushauri uliotolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo kwa lengo kuondoa matumizi ya fedha taslimu katika ununuzi wa mafuta kwenye vituo vya mafuta na badala yake watumie njia za kielektroniki kununua bidhaa hiyo.

Nyongo ametoa rai hiyo leo, Mei 8, 2025, alipofungua kongamano la kwanza la kodi lililoandaliwa na Chuo cha Kodi (ITA) lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo lililoshirikisha taasisi zaidi ya 30, wadau mbalimbali ikiwamo Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo,  Nyongo amegusia changamoto ya ulipaji fedha taslimu  akieleza hilo bado ni tatizo na kushauri matumizi ya kielektroniki.

“Mfano, leo tukisema vituo vya mafuta visipokee malipo ya pesa taslimu watu wanunue mafuta kwa njia ya kielektroniki, nini kinashindikana?” amehoji na kuongeza:

“Yoyote mwenye simu, awe bodaboda, magari binafsi, malori, wakienda kujaza mafuta walipe kielektroniki, kila kituo watu wakinunua mafuta kwa kielektroniki, shida ipo wapi?” amehoji Nyongo.

Amesema hiyo ni rai yake kwa TRA kuona namna ya kulifanyia kazi kwa kuwa ni suala la kuamua na watu watalielewa.

Akifafanua jambo hilo, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema wazo hilo na mengine yote yaliyojadiliwa katika kongamano hilo, yanakwenda kufanyiwa uchambuzi yakinifu ili kwenda kwenye utekelezaji.

“Mawazo yaliyojadiliwa katika kongamano hili yote tunakwenda kuyafanyia analysis (uchambuzi) na ambayo yatahitaji kurekebishwa kwa mujibu wa sheria, tutakwenda kwenye sheria na tutashauri ikiwamo hilo la kupunguza matumizi ya pesa taslimu.

“Tutaangalia njia rafiki kwa atakayetumia cash na atakayelipa kidijitali, mfano kuweka incentive (motisha) kwa atakayelipa kidijitali,” amesema.

Kuhusu kongamano

Akizungumzia kongamano hilo la kwanza la kodi, Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA), Profesa Isaya Jairo amesema linakwenda kutoa majawabu hasa katika kuongeza wigo wa ulipaji kodi ili kuongeza mapato.

“Sisi tunafundisha wafanyakazi wa TRA, hivyo kongamano hili pia litasaidia kujua changamoto za kikodi ili wanafunzi wetu wazifahamu na kuzitumia,”

Amesema kongamano hilo litasaidia kuonyesha uhalisia wa biashara na hali ilivyo katika tasnia ya kodi, akigusia pia changamoto ya biashara zisizo rasmi ambazo zinasababisha kupunguza ulipaji wa kodi.

Kamishina Mwenda na Naibu Waziri Nyongo wamegusia pia changamoto na mafanikio ya ulipaji kodi ambavyo katika kongamano hilo vimejadiliwa.

“Kuna changamoto kubwa katika eneo la manufacturing (uzalishaji), kuna watu wanakwepa kodi na ambao tumewabaini, hatua dhidi yao zinachukuliwa bila kumuonea mtu,” amesema Kamishna Mwenda.

Ameyataja baadhi ya maeneo ambayo yana changamoto zaidi kuwa ni Mkuranga, Pwani na Chang’ombe Dar es Salaam ambako kuna watu wanazalisha usiku na baadhi wameshakamatwa.

“Kuna taarifa tumezithibitisha za watu kukwepa kodi, tuliowakamata hatua zitachukuliwa dhidi yao huku tukiendelea kutoa elimu,” amesema akibainisha mkakati wa TRA kuwa ni kupanua wigo wa kodi huku biashara zikikuwa kama yalivyo maono ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Watu walizoea kulipa kodi huku biashara zikifa, hili halipo tena na mkakati wa kupanua wigo kwenye kodi huku biashara zikikua,” amesema.

Katika kongamano hilo, Nyongo alizindua tuzo mbili ikiwamo ya mtoa taarifa za kikodi ambayo itatolewa kwa watu watakaowafichua wakwepa kodi.

“Taarifa zikifa TRA itachunguzwa na aliyemfichua mkwepaji kodi kuna zawadi ya Sh1 milioni hadi Sh20 milioni,” amesema.

Nyongo ameitaja tuzo ya pili kuwa ni ya ubunifu ambayo itatolewa kwa mtu atakayetoa wazo la kusaidia kupata kodi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *