Naibu Waziri amtaja kada Chadema shujaa aliyejitoa kwa wengine

Dar/Babati. Aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Manyara, Dk Derick Magoma, amehitimisha safari yake ya mwisho duniani huku Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, akisema amefariki dunia akiwa shujaa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya uokoaji wa watu kwenye maafa ya mafuriko Hanang, mkoani Manyara.

DkMagoma, ambaye mwaka 2015 na 2020 aliwania ubunge wa Hanang kupitia Chadema, alifariki dunia Februari 9, 2025, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani.

Safari yake ya mwisho imehitimishwa leo Jumanne, Februari 11, 2025, kijijini kwao mji wa Magugu, Kijiji cha Matufa, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara katika maziko yaliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji, akiwemo Dk Mollel na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Katika salamu zake, Dk Mollel amesema Dk Magoma alikuwa miongoni mwa watu waliotoa msaada katika maporomoko ya mafuriko yaliyotokea Desemba 3, 2023, na kusababisha vifo vya watu 89, majeruhi, na uharibifu wa mali na miundombinu.

Amesema enzi za uhai wake alifanya kazi kubwa huku akijua tatizo lake la saratani lililomsumbua kwa miaka miwili, lakini alipambana katika uokozi wa manusura wa ajali hiyo.

“Tayari Dk Magoma aliyelala hapa alikuwa anajua saratani yake haiwezi kupona na alijua anaweza kuaga dunia wakati wowote, lakini tulikuwa naye,” amesema Dk Mollel

Kwa mujibu wa Dk Mollel, pamoja na Dk Magoma kutambua hali yake, bado alinyanyuka na kwenda kuwasaidia Watanzania wenzake waliokumbwa na maafa Hanang. Baada ya kumaliza hotuba yake, Dk Mollel alitoa rambirambi ya Sh1 milioni.

“Baada ya kufika hapa leo, kesho nitakuja tufanye mazungumzo na wewe, shemeji yangu, kukupatia Sh4 milioni kumaliza shida zilizopo lakini kukuomba kama utaridhia watoto alioacha wakasomeshwe katika shule iliyopo kwenye mradi wetu,” amesema Dk Mollel.

Katika maelezo yake, Dk Mollel alianza kwa kusema tatizo la saratani ni kubwa, katika miaka mitatu iliyopita, watu waliokuwa wanakwenda Hospitali ya Ocean Road wengi walibainika kuwa saratani zilizokuwa zimefikia hatua ya mwisho, hivyo haitibiki.

“Tulipokwenda na Kamati ya Bunge kwa kuangalia taarifa zote, iligundulika baadhi ya watu waliokuwa wakifika Ocean Road wanakuwa wamechelewa. Wengi walikuwa wanakwenda kwenye dawa za kienyeji ambazo mara nyingine zinaongeza ukubwa wa tatizo,” amesema.

Dk Mollel amesema asilimia 20 ya wagonjwa wote waliokuwa wanakwenda katika hospitali hiyo walikuwa na saratani hatua ya kwanza na ya pili. Baada ya kubaini hilo, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaita wataalamu Ikulu.

“Ilikuwa hatua mbaya, na alitutaka kuja na suluhisho kuhakikisha jambo hilo halijitokezi tena. Serikali iliwekeza Sh6.7 trilioni kwenye sekta ya afya, hususan katika eneo hili la saratani,” amesema.

Naibu waziri huyo amesema baada ya hapo wameanza kuona matokeo, kwani walipotembelea na Kamati ya Bunge Oktoba 2024, walikuta asilimia 75 ya Watanzania wanaokwenda Ocean Road wakiwa na saratani hatua ya mwanzo, ambayo inaweza kutibika.

“Kinachosaidia ni kwamba sasa kuna madaktari wanaozunguka mikoani na moja ya mambo wanayosisitiza ni kutambua magonjwa haya mapema ili wawahi tiba na kujenga uwezo kule chini,” amesema.

Dk Mollel amesema Serikali imewekeza rasilimali kubwa katika eneo hilo, akisema kuna mashine mpya inayoweza kugundua saratani itakayotokea miaka 10 ijayo, na Afrika ni nchi nne pekee zinazomiliki mashine hiyo.

“Kwa miaka ya nyuma, mtu akipata uvimbe chini ya sakafu ya ubongo, alipofika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alifunguliwa kichwa chote ili kutolewa uvimbe. Leo, ukipata uvimbe kwenye sakafu ya ubongo, kuna mashine mpya zinazotumia njia ya pua, hivyo uvimbe unapasuliwa bila kufungua kichwa, na tiba hii sasa inapatikana nchini,” amesema.

Alichokisema Lissu

Lissu amesema chanzo cha kifo cha Dk Magoma ni ugonjwa wa saratani uliomsumbua kwa miaka miwili.

Amesema katika miaka 40 ya maisha yake duniani, Dk Magoma hakufariki vitani bali kwa tatizo la saratani, ugonjwa ambao bado unabaki kuwa fumbo kubwa.

“Binafsi sikuweza kwenda kumuona alipokuwa amelazwa Muhimbili. Kazi zilinizidi, lakini pia niliogopa kumuona akiwa mgonjwa kitandani akisumbuliwa na saratani kwa miaka miwili,” amesema.

Lissu amesema kwa kipindi hicho, ilikuwa inampa hofu, huku akisema Dk Magoma anayebaki kwenye kumbukumbu yake ni mtu aliyekuwa mwenye furaha, anayependa kucheka na kutabasamu muda wote.

“Magoma hakuwa mtu wa kuhuzunika, Dk Magoma ambaye anabaki kwenye kumbukumbu zangu anayecheka na kuchekesha muda wote na kutabasamu muda wote kwa sababu ni mtu safi,” Amesema Lissu.

Waombolezaji wakiaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Manyara, Dr Derick Magoma nyumbani kwake Kimandolu jijini Arusha leo Februari 10, 2025. Picha na Bertha Ismail

Awali, katika msiba huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless ema, alitoa ushauri kwa Serikali kufanya utafiti wa kina kubaini kiini cha ugonjwa wa saratani, akisema limekuwa tatizo kubwa ambalo haliangalii umri tena.

“Tulianza kumsaidia Magoma, na daktari aliyekuwa akimtibu alishauri kuwa kama tungeweza kumpeleka India, angeweza kupona. Nilianzisha kundi la kuchangisha michango, na asilimia kubwa ya waliochangia hawakumfahamu Magoma, lakini bado walichanga,” amesema.

Kuchangia ujenzi wa msikiti

Wakati wa maziko hayo ilikusanywa michango kwa ajili ya kusaidia uenzi wa msikiti ambao Dk Magoma enzi za uhai wake aliahidi kuchangia Sh15 milioni. Ukusanyaji wa michango hiyo uliendeshwa na Lema na waombolezaji mbalimbali walijitokeza kuchangia.