
Naibu Rais wa Kenya aliyeng’olewa madarakani, Rigathi Gachagua, ameishambulia serikari ya bosi wake wa zamani, Rais William Ruto, akisema imeziba masikio kwa vilio vya watu walioichagua akisisitiza kwamba hatimaye ataondolewa lawama zote “alizobambikiziwa” alipoondolewa mamlakani.
Bwana Gachagua amesema kuwa moja ya madai ya kuondolewa kwake madarakani ni kuhujumu serikali kwa kumwambia Rais William Ruto ukweli kuhusu dili za bilionea Adani ambao hatimaye umetimia.
“Nilikuwa mtu pekee ambaye ningethubutu kusema ukweli kwa Rais. Kabla ya kuondolewa mamlakani, nilimwambia Rais Ruto kwamba mpango wa Adani haukuwa mzuri kwa nchi. Kulikuwa na ufisadi mwingi katika mpango huo. Majibu kutoka kwa rais yalikuwa ni kufanikisha kuondolewa kwangu kwa madai kwamba nilikuwa nikihujumu serikali yake,” amesema Gachagua.
Aliyekuwa naibu rais wa Kenya amesema “Serikali imeziba masikio kwa vilio vya watu waliowachagua na kama si serikali ya Marekani kuingilia kati, mikataba ya Adani ingetekelezwa.”
Majuzi, Rais wa Kenya William Ruto aliamuru kufutwa mchakato wa ununuzi ambao ulitarajiwa kukabidhi udhibiti wa uwanja mkuu wa ndege wa nchi hiyo kwa kampuni ya India ya Adani Group baada ya mwanzilishi wa kampuni hiyo kufunguliwa mashtaka nchini Marekani.
Chini ya mpango huo wenye thamani ya karibu dola bilioni 2, Adani Group lilipaswa kuongeza njia ya pili ya kurukia ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na kuboresha kituo cha abiria mkabala wa kukodishwa uwanja huo kwa miaka 30.