
Dodoma. Wakati viongozi wa Chadema wakiendelea kuinadi kampeni ya ‘No Reforms No Election’ (hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi), Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imesisitiza Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 utafanyika na wanaotaka usifanyike hawataweza.
Kaulimbiu hiyo imekuja takriban wiki mbili tangu ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa chini ya Jaji Francis Mutungi, ilipokutana uongozi wa Chadema Machi 18, 2025 kujadili tafsiri ya ‘No Reforms No Election’, kwa muktadha wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Licha ya majadiliano ya takriban saa nne, hakuna muafaka wowote uliopatikana na ofisi hiyo ilisema ingewaita siku nyingine kuendelea na majadiliano.
Hali ikiwa hivyo, leo Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, ameweka bayana kuwa “Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 utafanyika bila kujali vikwazo vinavyowekwa na baadhi ya wanasiasa.”
Kwa mujibu na sheria na Katiba, masuala ya uchaguzi yako chini ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo inasimamia na kuratibu uendeshaji wa chaguzi kwa mujibu wa sheria ili kulinda demokrasia kwa manufaa ya wananchi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikiwa na majukumu ya usajili, uratibu na ufuatiliaji wa vyama vya siasa.
Kampeni yapigwa kila kona
Kauli ya Nyahoza haikombali na iliyowahi kutolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi kuhusu suala hilo, akisema kama kuna nia njema ya mabadiliko ofisi za wizara hiyo ziko wazi kwa yeyote kwenda kujadiliana.
Maswi mbali na kusema kuwa mabadiliko muhimu yalikwishafanyike kwenye sheria, alisisitiza kuwa “Chadema pekee haiwezi kuzuia uchaguzi kwa kuwa mchakato huo unawahusisha wananchi na chama zaidi ya kimoja.”
Mbali na hao, pia viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) – Amos Makalla, katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Taifa na Makamu Mwenyekiti, Stephen Wasira kwa nyakati tofauti wametoa kauli mbalimbali za kupingana na kampeni hiyo.
Wakati Makala akisema kampeni hiyo ina maana Chadema haitaki kushiriki uchaguzi na ikifanya hivyo, utakuwa mwisho wa kuwa chama kikuu cha upinzani, Wasira amekuwa anahoji watazuiaje uchaguzi, ambao ni mchakato na umekwishaanza.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kahama Machi 27, Wasira amesisitiza hakuna mwenye uwezo wa kuzuia uchaguzi huo “labda wawe wanaota ndoto ya mchana.”
Wasira alisema pamoja na kampeni wanazoendelea kuzifanya, hawana uwezo wa kuzuia uchaguzi usifanyike kwa sababu tayari hatua ya kwanza ya uchaguzi huo imeanza kwa wananchi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.
“Nasikia wanazunguka nchi nzima wakifika hapa Kahama, muwasikilize halafu muwaulize mnatumia njia gani ya kuzuia uchaguzi, maana Katiba inakataa, inasema hakuna uchaguzi kuahirishwa labda kama kuna vita na hata kama ikiwepo vita, inasema ni kwa miezi sita ndio unaweza kuahirisha ili vita iishe,” amesema na kuongeza;
“Hakuna jambo jingine linaweza kuzuia uchaguzi, lakini wamesisitiza wanaweza kuuahirisha, sasa muwaulize wanatumia mbinu gani kuuairisha, halafu niliwaambia nilipokuwa Bukoba, mbona uchaguzi umeshaanza, maana Dar es Salaam wamemaliza kujiandikisha na kujiandikisha ni sehemu ya uchaguzi,” amesema.
Kauli ya msajili
Katika kauli hiyo Nyahoza ameendelea kusisitiza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utafanyika bila kujali vikwazo vinavyowekwa na baadhi ya wanasiasa ambao hakuwataja.
Hata hivyo, inafahamaika kuwa Chadema ndiyo inayoendesha kampeni ya kuzuia uchaguzi ikiwa mabadiliko makubwa katika mfumo wa uchaguzi hayatafanyika.
Nyahoza ametoa kauli hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, uliofanyika leo Jumamosi Machi 29, 2025 jijini Dodoma.
Nyahoza, akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesisitiza kuwa, “kwa namna yoyote lazima uchaguzi ufanyike,” akiongeza kuwa maandalizi ya uchaguzi yanaendelea kama yalivyopangwa na vyama vyote vilivyosajiliwa nchini, vina haki sawa ya kushiriki.
Amesema siasa za majukwaani kwamba hakuna uchaguzi zisiwacheleweshe, badala yake waendelee kuwa na maandalizi ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu.
Amehoji nani anaweza kumwandaa mwanawe kufanya mtihani, halafu ghafla akaambiwa mtihani umeahirishwa atafurahi, wajumbe waliitikia kuwa haiwezekani.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa vyama vyote vyenye usajili wa kudumu katika Ofisi ya Msajili vina uzito sawa na hakuna chama kikubwa kuliko kingine, kwa hiyo milango ya uchaguzi ni kwa vyama vyote.
Majibu ya Chadema
Licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa kueleza hayo, Chadema kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa, Brenda Rupia kimesema maneno ya Nyahoza hayakwamishi ajenda yake.
“Sisi ajenda yetu ipo palepale na tulishamshirikisha Msajili Jaji Mutungi na Nyahoza akiwepo, kwa hiyo ama wamekubaliana nasi au hapana, sisi msimamo wetu ni pasina mabadiliko uchaguzi hautafanyika,” amesema.
Hata hivyo, amefafanua kuwa ajenda hiyo hailengi chama hicho kususia uchaguzi, bali kitazuia tukio hilo kufanyika na mbinu zinazotumika ni kuendelea kuyashirikisha makundi mbalimbali kulifanikisha hilo.
Alipoulizwa watafanyaje kuzuia uchaguzi, Brenda amesema utakapofika wakati ndipo itakapojulikana mbinu itakayotumika, lakini kwa hatua ya sasa wanashirikisha wadau mbalimbali.
Hata hivyo Jumatano Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akihutubia mkutano wa hadhara Sumbawanga mkoani Rukwa, alisema kugomea kila watakachokuwa wanaambiwa na Serikali ni miongoni mwa njia watakazotumia kuzuia uchaguzi kufanyika.
“Chochote wanachopendekeza tukisusie, tukikatae kila watakachotuletea na nimeangalia sheria za nchi sijaona sehemu kama tukikataa kwenda kupiga kura ni dhambi au tumevunja sheria, lakini ukweli wa Mungu ni kwamba hata kwa Katiba hii inawezekana kuahirisha uchaguzi,” alisema Lissu.
Kuhusu NCCR
Nyahoza ameitaka NCCR-Mageuzi iendelee kudumisha amani kama walivyoimba kwenye wimbo wa Taifa.
Mapema, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi -Bara, Joseph Selasini amesema mwaka huu hawadanganyiki hata kidogo kuingia katika ushirikiano.
Selasini amesema katika moja ya uchaguzi walifanya makubaliano ya walichokiita Ukawa, lakini kuna chama kilivisaliti vingine.
Amesema katika usaliti huo, wenzao walianza kupora majimbo, hata waliyokuwa wamekubaliana kugawana wao wakaona wana haki.
“Mfano ni Jimbo la Serengeti ambalo alikuwa akitoka katibu wetu mkuu tulisema libaki kwetu, lakini wenzetu wakapeleka mgombea wao na mwisho tukapoteza,” amesema Selasini.
Amesema mara kadhaa chama hicho kimeshaumwa na nyoka kwa hiyo habari ya ‘no reforms no election’ haiwezi kuwapotosha tena.
Amesisitiza kuwa NCCR-Mageuzi inataka kurudisha makali yake ya miaka ya nyuma kilipokaribia kuchukua nchi, na sasa inaingia kwenye uchaguzi kwa nguvu kubwa zaidi ya hiyo.
Nyongeza ya story imetoka kwa Noor Shija na Juma Issihaka