Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah asema Israel ni tishio la kweli kwa dunia

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ameonya kuwa sera ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kukalia kwa mabavu ardhi za wengine ni tishio sio tu kwa Palestina bali kwa eneo na dunia nzima.

Sheikh Naim Qassem alikuwa akizungumza Jumanne katika hotuba yake ya tatu ya televisheni tangu kuuawa shahidi kiongozi wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrallah. Ameongeza kuwa Israel ni utawala ghasibu ambao unahatarisha eneo la Asia Magharibu na dunia nzima.

Sheikh Naim Qassem ameashiria umuhimu wa muqawama na mapambano katika kukabiliana na mauaji hayo yanayoratibiwa na Israel na waungaji mkono wake.

Sheikh Qassem amesisitiza kwamba “Israel na waitifaki wake wanapigana vita na kufanya mauaji, na hivyo kutuacha bila chaguo ila kuchukua msimamo,”

Pia alifichua mpango wa pamoja wa Marekani na Israel katika eneo Asia Magharibi, akisema, “Marekai, shetani mkubwa zaidi, anataka Mashariki ya Kati mpya. Netanyahu ana maono sawa. Hii ina maana kwamba Marekani na Israel zinatekeleza mauaji haya ya kimbari kwa makusudi.”

Wapiganaji wa Hizbullah

Sheikh Qassem amesisitiza kuwa Hizbullah haitashindwa katika mgogoro wake wa muda mrefu na utawala wa Israel.

Amesema, iwapo Tel Aviv itawataka walowezi wa Kizayuni kurejea katika makazi yao katika maeneo ya kaskazini yanayokaliwa kwa mabavu, ni lazima isitishe hujuma zake dhidi ya Gaza na Lebanon.

Kiongozi wa Hezbollah ameonya zaidi kwamba kama uchokozi utaendelea, idadi ya makazi yaliyoteketezwa itaongezeka, na kuweka mamia ya maelfu – uwezekano wa zaidi ya milioni mbili – ya walowezi katika hatari.

Katika hotuba yake, Sheikh Qassem ameashiria Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa- shambulio la Oktoba 7, 2023 dhidi ya kitengo cha Kizayuni – akisema kwamba Wapalestina, wakiongozwa na Hamas, “walijaribu kuwaondoa wavamizi.”

Sheikh Naim Qassem amesisitiza kuwa mgogoro wa Hizbullah na utawala wa Israel hauwezi kutenganishwa na mapambano ya ukombozi wa Palestina.