
Dar es Salaam. Kauli ya kawaida inayotumiwa na wanawake walioolewa “Nakwenda kwa mama” ambayo huonekana kama ya kawaida na yenye malengo ya mapumziko au kutafuta utulivu wa muda, sasa imeanza kuchukua sura mpya.
Kwa mujibu wa utafiti wa Mwananchi, baadhi ya wanaume wanaeleza kuwa kauli hiyo sasa imegeuzwa kuwa silaha ya kuvunja ndoa.
Katika hali ya kawaida, wanawake huondoka kwenda kwao kwa ajili ya kujifungua, kusalimia wazazi au hata kupumzika tu.
Hata hivyo, kwa baadhi ya familia, kauli hiyo imekuwa kama “alama ya mwisho ya amani” kabla ya ndoa kusambaratika.
Jabir Omary mkazi wa mkoani Dar e Salaam, anasimulia namna kauli hiyo ilivyomtesa huku akikosa mtu wa kumjali kufuatia masaibu yake.
“Ndoa yangu ilidumu mwezi mmoja pekee baada ya kumaliza fungate na likizo niliyoomba kwa ajili ya kutumikia ndoa, lakini baada ya hapo sikuona tena umuhimu wa kuendelea na ndoa hiyo baada ya mke wangu kila siku kwenda kwao.
Anasema wao walikuwa wanaishi na mkewe Tandika na wakwe zake wanaishi Temeke Wailes, hivyo mkewe alitumia ukaribu huo kama kigezo cha kwenda kwao mara kwa mra.
Anasema kila alipokuwa akimpigia simu alimueleza yupo kwao na hata alipomueleza kubaki nyumbani kwake kwa ajili ya kuzoea mazingira, ilikuwa ni kibarua kigumu kwani alilazimika kumfuata kila anapotoka kazini.
“Alikuwa anakaa kwao hadi jioni akitaka kurudi ananiambia nimfuate nisipofanya hivyo harudi na kuamua kulala huko bila sababu za msingi. Hata niliposhirikisha wazazi walisema anakuwa mpweke hivyo napaswa kutafutiwa mtu wa kushinda naye,” anasema.
Anasema licha ya kuelezwa hayo hakuamini kama hiyo ni sababu ya mkewe kufanya hivyo, kwani hata alipokuwa akimsema alikuwa akimjibu kuwa anakwenda kwa mama yake na hawezi kupangiwa wapi pa kwenda.
Kwa kuwa ulikuwa utaratibu wa mara kwa mara aliamua kuachana naye, ili awe huru kubaki nyumbani kwao.
Si Omary pekee aliyekutana na mkasa huu, hata Huruma Hamad anasema kadhia hiyo ilimkumba baada ya mkewe kusema anakwenda kujifungulia kwa mama yake na kushindwa kurudi tena nyumbani kwake.
“Mke wangu aliniambia anataka anakwenda kwa mama yake kujiangalizia, hata baada ya kujifungua hakutaka kurudi na kudai kuwa bado analea,”anasema Hamad.
Anasema hali hiyo ilimuumiza kwani ilikuwa ni kawaida yake kila baada ya muda fulani, alikuwa akiomba kwenda kwa mama yake bila kueleza sababu za msingi.
Wakati Omary na Hamad wakisimulia hayo, wanaume wengine wawili wanaeleza kuwa kauli hiyo sasa hutumiwa kama kisingizio cha kuondoka kwenye ndoa bila kutafuta suluhu.
Wengine wanasema wake zao wakati mwingine hutoa kauli hiyo bila ya kuwapo kwa mzozo wowote na hupotea kwa muda mrefu au kutorudi kabisa.
Wasemavyo wanawake
Fatuma Hassan, mkazi wa Kigamboni, anaeleza kuwa kwenda kwa mama ni jambo la kawaida na si lazima lihusishwe na migogoro.
“Mwanamke ni binadamu, naye anahitaji kupumzika. Mara nyingine unapokwenda kwa mama, unapata nafasi ya kubadilisha mazingira na kupata msaada wa kulea mtoto,” anaeleza.
Kwa upande wake, Zainabu Athumani, anaeleza kuwa matumizi ya kauli hiyo yanategemea mazingira ya ndoa husika.
“Kwa mila zetu, mwanamke kwenda kwa mama wakati wa uzazi ni utaratibu wa kawaida. Tatizo linakuja pale ambapo safari hiyo haitajwi lini itaisha, au inageuzwa kuwa njia ya kutoroka majukumu ya kindoa,” anasema.
Rehema Haule, mzazi na mkazi wa Kinyerezi anasema ndoa ya mwanawe ilivunjika kutokana na kukosekana kwa misingi ya mawasiliano.
“Hofu na ukosefu wa uaminifu kwenye ndoa ndicho chanzo cha kauli hiyo kuwa na uzito tofauti. Wanawake hawapaswi kuogopa kueleza kuwa wanahitaji mapumziko, na wanaume hawapaswi kuchukulia kila safari kwenda kwa mama kama tishio la ndoa.”anasema.
Anasema mtoto wake alikuwa akimueleza anahitaji kupumzika hata alipojaribu kumrudisha kwake alimueleza uongo kuwa mumewe anamtesa hivyo anahitaji kupumzika.
Kauli ya “Nakwenda kwa mama” inaweza kuwa ya kawaida, ya busara au ya utata kutegemea mazingira ya ndoa. Ikiwa haina mawasiliano ya wazi na mipaka ya kuelewana, inaweza kuvuruga zaidi ya kusaidia, hivyo ni wajibu wa wanandoa wote wawili kujenga msingi wa mazungumzo na kuondoa hofu ya kuachwa kimya.
Wanaume kadhaa wanaeleza kuwa kauli hiyo imekuwa kama ‘kinga’ ya kutoachana na wake zao.
“Unapomwambia mke wako kuwa jambo fulani halikufurahishi, badala ya kuzungumza anakujibu, ‘Basi nitaenda kwa mama’. Hiyo imekuwa kama tishio la kimya kimya,” anasema Mwinuka Mwinuka, mkazi wa Tabata.
Mwanasaikolojia
Mtaalamu wa saikolojia, Clara Mwambungu anasema msingi wa sentensi hiyo unatokana na hitaji la mtu kutafuta faraja ya kihisia iliyosababishwa na mambo mbalimbali.
“Mama ni taswira ya mtunzaji wa maisha katika akili zetu, katika nyakati za dhiki, hivyo akili hurudi kwenye kumbukumbu za mwanzo za usalama. Ndiyo maana mtu mzima anaweza kusema ‘nakwenda kwa mama’ kama njia ya kutafuta utulivu wa ndani,” anasema Clara.
Anabainisha kuwa, kwa baadhi ya watu, tabia hiyo inaweza pia kuashiria hali ya utegemezi wa kihisia ambayo huendelea hata mtu anapokomaa kiumri, jambo linalohitaji msaada wa kisaikolojia iwapo litasababisha mtu kushindwa kujitegemea.
Mtazamo kidini
Mchungaji wa Kanisa la Baptist la mkoani Mbeya, Daniel Mgogo anasema kauli hizo zinatokana na wengi wao waliongia kwenye ndoa, kuingia kimwili lakini kiakili wapo nyumbani kwa wazazi wao.
“Bibilia inasema utawaacha baba na mama yako na kuambata na mwenza wako, sasa hii kauli ya nakwenda kwa mama mara kwa mara ni wazi kuwa bado akili zake zipo kwao,”anasema.
Anasema wapo wengine wameingia katika ndoa na kuacha nguo zao kwa wazazi kwa wale wanaoishi karibu, na kuamua kila anapotoka kwenye shughuli zake anakwenda kwao na kubadilisha nguo.
Hivyo anasema mazingira hayo ni ya kutengeneza familia za watoto waoga, ambao bado hawajajikubali katika kujitegemea na ndipo kauli ya nakwenda kwa mama inachukua nafsi kila anapojisikia kufanya hivyo.
“Mtoto akikaa kwa mwenza wake anaona kama hayupo huru na yupo kwenye mateso na msongo wa mawazo, hivyo uamuzi sahii ni kudai kwenda kwa mama yake au wazazi wake bila kumshirikisha mwenzake kujua nini tatizo,” anasema.
Naye, Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo anasema jambo la muhimu ni wazazi wa binti kujua kuwa wakishaozesha hawana madaraka tena kwa binti yao.
Kwa kutambua hilo anasema italeta nidhamu ndani ya ndoa na kuepuka kauli za kwenda kwa wazazi au mama kutojitokeza ndani ya ndoa kwa kuwa kila mmoja anajua majukumu yake.
“Katika dini ya Kiislam binti akishaolewa hana ruhusa ya kwenda sehemu yoyote bila ruhusa ya mumewe, hata ikitokea mzazi wake anaumwa au amefariki,” anasema Sheikh Kitogo.
Anasema kujenga mazoea ya kwenda kwa wazazi mara kwa mara, inatengeneza uongo wakati mwingine binti anakwenda safari nyingine akirudi kwa mumewe anasingizia alikuwa kwa mama yake.
Amedai kuwa hali hiyo inapunguza uaminifu wa mwanaume kwa wakwe zake, kwa kuamini kuwa wanaweza kuwa wanajua kila anachokifanya mtoto wao.
Nini kifanyike?
Mchungaji Mgogo anasema ni jukumu la wazazi na viongozi wa dini kutoa elimu kwa vijana wanapoingia kwenye ndoa kuwa jambo hiko sio sehemu ya majaribio, kwani wanatakiwa kujifunza ili kuishi kama wazazi wao.
“Kama mtoto anawaona wazazi wake wakiwa pamoja na hakuna anayesema anakwenda kwao ama kwa kukasirishwa au kutembea bila sababu za msingi, basi wanatakiwa kujifunza hapo,”
Anasema wazazi waache tabia ya kuona watoto wao kama wanaonewa na kutaka kujua namna wanavyoishi na wenza wao, kwani hilo linachangia kwa asilimia kubwa kutengeneza migogoro na watoto kudai kwenda kwa wazazi.
Kwa upande wake, Sheikh Kitogo anasema wazazi wawe na tabia ya kuhoji wanapomuona mtoto wao amefika kwao kwa kumuuliza mumewe kama anatambua safari ya mkewe.
“Wazazi wakiwa na tabia ya kuhoji, binti hata kama alikuwa na mambo yake hawezi kufanya na atakuwa na nidhamu ya ndoa yake kwa sababu wazazi wanakuwa na misimamo,”anaeleza.
Mbali na hilo, anasema viongozi wa dini wataendelea kutoa mafunzo mbalimbali ya Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie), ili kurudisha nidhamu ndani ya ndoa na kuepusha kauli zisizo na maana kwenye uimara wa ndoa.