Nactivet yaonya wanawake kutegemea akili bandia katika ubunifu

Arusha. Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactivet) limewaonya wanawake dhidi ya utegemezi wa mifumo ya akili bandia (AI) katika shughuli zao za ubunifu.

Hata hivyo, limeshauri wanawake kuendeleza maarifa ya kibinadamu ili kuboresha ubunifu wao na kuimarisha kwa ujuzi wa teknolojia na siyo kutumia mifumo ya akili bandia pekee.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, leo Jumatatu, Machi 10, 2025, Mwenyekiti wa wanawake kutoka Nactivet, Deborah Ngalemwa, amesema utegemezi wa AI una hatari ya kupunguza uthamani wa ubunifu.

“AI inatoa fursa kubwa za kurahisisha kazi za ubunifu, lakini kuna hatari ya kupunguza uthamani wa ubunifu wa mtu binafsi endapo itategemewa kupita kiasi.

“Tunapoadhimisha wiki ya Siku ya Wanawake Duniani, tunapaswa kuangalia na hili la kuitumia AI (akili bandia) kama nyenzo ya kusaidia, lakini si kama mbadala wa fikra na ubunifu, kwani kutegemea AI kupita kiasi kunaweza kusababisha kupotea kwa upekee wa kazi zetu na kupunguza ushindani katika soko la ajira na ujasiriamali,” amesema.

Amesema kuwa Nactivate imetumia maadhimisho hayo kuhamasisha wanawake kuegemea katika ufundi kwa sababu imekuwa ikileta fursa kwa kinamama wengi kupata ujuzi na kukuza uchumi wao kupitia biashara za bunifu zao.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wasichana walioko shuleni kuzingatia elimu ya ujuzi na maarifa ili kukidhi soko la ajira kitaifa na kimataifa.

“Pia, wazazi wajitahidi kukuza watoto wao katika ujuzi. Sio unamuona mwanao anajifunza kusuka, au kushona au hata kutengeneza vitu mbalimbali, unamkataza. Inatakiwa umjue mapema na umuendeleze awe mbunifu, kwani dunia ya sasa inataka wataalamu wa ufundi na ubunifu,” amesema.

Awali, Mhadhiri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Dk Elias Kimaro, alieleza kuwa AI ni nyenzo muhimu katika kuboresha bunifu, lakini matumizi yake yanapaswa kusimamiwa kwa uangalifu ili kuepusha athari kama vile kupotea kwa ajira na udhaifu wa ubunifu binafsi.

Aliwataka wanawake kuimarisha ujuzi wa kiteknolojia kwa kushiriki mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kutumia AI kwa njia sahihi.

“Vilevile, nawasihi kuendeleza maarifa ya kibinadamu ili kuboresha ubunifu wenu bila kutegemea mifumo ya akili bandia pekee,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *