Mzize na rekodi tamu Yanga, Dube naye usipime

Dar es Salaam. Clement Mzize ameiongoza Yanga kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya KenGold leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam baada ya kupachika mabao mawili huku mengine yakipachikwa na Prince Dube, Pacome Zouzoua na Duke Abuya.

Mabao hayo yamemfanya Mzize kuongoza chati ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu akifikisha mabao tisa, moja zaidi ya nane yaliyofungwa na Elvis Rupia ambaye aliongoza chati hiyo kwa muda mrefu.

Licha ya kumuwezesha kuongoza chati ya ufungaji bora, mabao hayo mawili yamemfanya Mzize kujiwekea rekodi yake mwenyewe ya kufunga mabao katika mechi tano mfululizo za Ligi Kuu.

Kabla ya kufunga mabao hayo Mzize alikuwa amefunga katika michezo dhidi ya Kagera Sugar, Fountain Gate, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons.

Mzize alifunga bao moja katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons ambayo Yanga ilipata ushindi wa mabao 4-0, kisha akafunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji waliyopata ushindi wa mabao 4-0.

Mzize alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Fountain Gate na akafunga bao moja katika ushindi wa mabao 4-0 ambao Yanga iliupata katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar.

Katika mechi ya leo, Mzize alifunga mabao hayo katika dakika ya sita ya mchezo na dakika ya 42.

Bao la kwanza la Mzize alilifunga kwa shuti la wastani la mguu wa kulia akiunganisha mpira uliookolewa vibaya na beki Bilali Abdi na bao la pili alipachika katika dakika ya 42 akiunganisha mpira uliotemwa na kipa Castor Mhagama alipokuwa katika harakati za kuokoa krosi ya Chadrack Boka.

Mabao mengine katika mechi ya leo yamepachikwa na Dube aliyefunga katika dakika ya pili na dakika ya 45, Pacome Zouzoua akifunga katika dakika ya 38 na bao la ushindi lilifungwa na Duke Abuya katika dakika ya 84.

Dakika moja baada ya Abuya kufunga bao hilo, KenGold walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Seleman Bwenzi aliyefunga kwa shuti la moja kwa moja kutokea katikati ya uwanja wakati akianzisha mpira ambalo lilimshinda kipa Djigui Diarra.

Ushindi huo umeifanya Yanga ifikishe pointi 45 zinazoifanya iwe kileleni mwa msimamo wa ligi ikisubiria matokeo ya mchezo wa Fountain Gate dhidi ya Simba, kesho Alhamisi, Februari 6, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati.

KenGold inashika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imekusanya pointi sita katika mechi 17.