Mzize, Dube waipaisha Yanga ikichanja mbuga kileleni

Yanga imezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam huku ikiiacha Simba iliyo nafasi ya pili kwa pointi tano.

Mabao yaliyofungwa na Clement Mzize na Prince Dube kwenye mechi ya leo, yameifanya Yanga kufikisha pointi 52 ambazo zimeifanya iendelee kutamba kileleni mwa msimamo wa ligi ingawa imecheza mechi mbili zaidi ya Simba, yenyewe ikiwa na mechi 20 huku mshindani wake huyo wa karibu akiwa amecheza mechi 18.

Mzize alitangulia kufunga bao la kuongoza la Yanga katika dakika ya 14 ya mchezo baada ya kuunganisha kwa shuti kali mpira ambao haukuokolewa vizuri na Iddi Habibu.

Bao hilo lilikuwa la 10 kwa Mzize na kumfanya azidi kuongoza chati ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Dakika ya 43, Prince Dube aliipatia Yanga bao la pili ambalo lilikuwa la tisa kwake baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona wa Stephane Aziz Ki.

Mabao hayo mawili yalidumu hadi filimbi ya mapumziko ilipopulizwa.

Katika kipindi cha pili, Yanga iliendelea kutawala mchezo lakini wachezaji wake wa nafasi za ushambuliaji walishindwa kutumia nafasi nyingi walizotengeneza, kuipa timu yao mabao ya ziada.

Wakati mchezo huo ukielekea ukingoni, Jonathan Sowa wa Singida Black Stars aliipatia timu yake bao la kufutia machozi akimalizia kwa ustadi mpira uliotemwa na kipa Djigui Diarra.

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Fountain Gate ambayo imevuna pointi moja  dhidi ya Tabora United, imeendelea kusota Ligi Kuu Bara kwa kushindwa kuibuka na ushindi katika michezo saba mfululizo sawa na Jakika 630.

Mara ya mwisho kwa Fountain Gate kuibuka na ushindi Ligi Kuu Bara ilikuwa Desemba 13 mwaka jana dhidi ya Coastal Union kwa mabao 3-2.

Fountain Gate ambao kwenye mchezo wa kwanza waliifunga Tabora United kwa mabao 3-1, walikuwa na wakati mgumu kuifungua ngome ya wapinzani wao licha ya kutengeneza nafasi kadhaa kupitia kwa washambuliaji wao, William Edger, Daniel Joram na Shaaban Pandu.

Tabora ikiwa na Offen Chikola mwenye mabao sita na asisti mbili na Heritier Makambo mwenye mabao matano na wenyewe walikuwa na wakati mgumu kama ilivyokuwa kwa Fountain Gate, licha ya kila upande kucheza soka safi.

Kwa matokeo hayo, Tabora (33) ambayo ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi imepunguza tofauti ya pointi kutoka tano hadi nne kati yao na Singida BS (37) ambao walipoteza jana dhidi ya Yanga kwa mabao 2-1. Fountain wapo nafasi ya saba na pointi