Mzize, Ateba wanavyofukuzia rekodi Ligi Kuu

Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuendelea Ijumaa hii kwa kiporo cha Simba dhidi ya Dodoma Jiji kupigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, lakini huku nyuma kuna vita nzito ya mastraika katika kufumania nyavu upinzani zaidi ukiwa kati ya Clement Mzize, Prince Dude na Leonel Ateba.

Hadi sasa ligi ipo raundi  wa 23 na zimeshapigwa mechi 179 zilizoshuhudia jumla ya mabao 400 yakifungwa, huku Mzize na Dube wa Yanga na kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua kila mmoja akifunga 10 wakifuatiwa na orodha ya nyota wengine wakiwamo mastraika na viungo washambuliaji wenye mabao kati ya tisa na saba wakiwa ndio vinara katika orodha ya wafungaji.

Katika mabao hayo 400 yaliyofungwa hadi sasa, 13 ni ya kujifunga na 213 yakiwekwa wavuni na nyota wazawa 101 na mengine 175 yakifungwa na nyota wa kigeni, lakini vita inaonekena ipo kwa washambuliaji wanaochuana kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu.

Licha ya kwamba ligi itasimama baada ya kiporo cha Simba na Dodoma Jiji, ili kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa na michuano ya Kombe la Shirikisho, lakini viwango vya baadhi ya washambuliaji na viungo washambuliaji katika kufunga mabao vimetoa picha ya vita kuwa ni nzito Bara.

Msimu uliopita vita ya ufungaji ilihusisha viungo wawili washambuliaji Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyeibuka kuwa Mfungaji Bora akifunga mabao 21 na asisti nane dhidi ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga 19 na asisti saba, lakini kwa msimu huu vita inaonekana kuwa mbichi ligi ikiwa raundi ya 23.

Zikiwa zimesalia mechi za raundi saba kwa kila timu kabla ya kufungwa kwa msimu, safu ya ushambuliaji imeingia vitani kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu ambapo hadi sasa kinara ni Mzize na Dube (Yanga) pamoja na Charles Ahoua (Simba) wamefunga mabao 10 kila mmoja. Dube ndiye mchezaji anayeongoza kuhusika na mabao mengi hadi sasa katika ligi ya msimu huu (17) kwani pia ameasisti mara saba.

Ukiondoa nyota hao watatu wa Simba na Yanga, pia kuna mshambuliaji Elvis Rupia wa Singida Black Stars mwenye mabao tisa akifuatiwa kwa karibu na Leonel Ateba na Steven Mukwala wote wa Simba, kila mmoja akiwa na mabao manane sawa na Peter Lwasa wa Kagera Sugar.

Orodha inaonyesha wachezaji watano Pacome Zouzoua na Aziz Ki (Yanga), Gibril Sillah (Azam),  Jonathan Sowah (Singida BS) na Offen Chikola wa Tabora United kila mmoja akifunga mabao saba na kwa mechi 61 zilizosalia kufunga msimu mambo yanaweza kuwa makubwa zaidi katika vita hiyo.

Licha ya kwamba katika orodha hiyo ya wafungaji hadi sasa ina mseto wa washambuliaji na viungo washambuliaji, lakini turufu ipo kwa mastraika zaidi kwani wameonekana kuwa moto akiwamo Sowah aliyetua dirisha dogo na kutumika katika mechi saba tu na amefunga mabao saba ikiwa na wastani wa kila mechi anafunga bao moja, mbali na Mukwala, Ateba, Mzize na Dube wanaobebwa na namba.

Mashabiki wa soka wana hamu kubwa ya kutaka kuona msimu huu, ni washambuliaji wazawa au wa wageni watakaoibuka kidedea kubeba kiatu cha dhahabu, kwani mara ya mwisho kwa straika kutwaa tuzo ya ufungaji bora alikuwa ni Fiston Mayele aliyekuwa Yanga aliyemaliza mabao 17 sawa na kiungo mshambuliaji aliyekuwa Simba, Said Ntibazonkiza.

Mayele alitwaa tuzo hiyo akimpokea George Mpole aliyekuwa Geita Gold, aliyemzidi bao moja katika mchuano wa msimu wa 2021-2022 akifunga 17 na Mkongomani huyo aliyepo Pyramids ya Misri akitupia 16 msimu huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *