Mzize anavyozidi kuwapa mawazo Waarabu

Clement Mzize ni Jina kubwa kwa sasa kwenye soka la Bongo. Kipaji murua cha kizawa. Kwenye akauti za mitandao za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuna picha na video zake likiwamo moja ya mabao yake bora kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika alilolifunga dhidi ya TP Mazembe.

Hii ndiyo maana anaimbwa sana. Anatakiwa na kila klabu kutokana na kiwango chake na tayari baadhi ya timu zilishatuma ofa mezani. Nini kitatokea. Tusubiri tuone.

Hata hivyo, namba zake kwenye Ligi Kuu Bara si mchezo tangu apandishwe timu ya wakubwa akitokea ile ya vijana na mchezo wake wa kwanza kutambulishwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar Septemba 13, 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kilichofuata ni historia.

Katika mchezo huo, aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Farid Mussa dakika ya 80 Yanga ikiongoza kwa mabao 2-0. Ingawa hakufunga lakini dakika 10 tu alizocheza zilitosha kuandika jina lake kwenye historia ya kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wakibeba taji hilo mara tatu mfululizo.

Hadi sasa Mzize amecheza Yanga kwa misimu mitatu na amefanya makubwa na kusababisha vigogo wa soka Afrika ikiwamo Wydad Casablanca ya Morocco kuisaka saini yake.

MZ 01

ALIVYOANZA KUTUPIA

Mzize alipandishwa kikosi kikubwa akitokea kile cha pili na aliyekuwa Mkurugenzi wake wa Ufundi, Mwinyi Zahera na Kocha Said Maulid msimu wa 2021/22.

Bao lake la kwanza alifunga dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na katika misimu mitatu aliyocheza amefikisha mechi 70 na kufunga mabao 21 kwenye mechi za Ligi Kuu pekee.

MABAO YAKE

Msimu wake wa kwanza 2022/23 alicheza mechi 20 akifunga mabao matano na kutoa pasi moja ya bao, 2023/24 alicheza mechi 29 akifunga mabao sita na kuasisti saba na msimu huu hasi sasa Yanga ikiwa imecheza mechi 21 na zote akipata nafasi ya kucheza, amefunga mabao 10 na kutoa pasi tatu za mabao.

Hata hivyo, kama ilivyo kwa nyota wengi wanaopandishwa, huwa hawaingii kikosi cha kwanza moja kwa moja na ndivyo ilivyokuwa kwa Mzize na ameruka vihunzi vingi hadi kujihakikishia namba katika vikosi vya makocha tofauti kutokana na ubora wake licha ya kuanza kwa kupata dakika chache za kucheza hadi kuaminiwa.

MZ 02

MBELE YA MAYELE, MUSONDA, DUBE

Ubora wa mchezaji haujifichi. Katika misimu yake mitatu kama mshambuliaji, Mzize amecheza katika nafasi hiyo na nyota wengine kama Fiston Mayele, Kenedy Musonda, Hafiz Wontah Konkon, Joseph Guédé Gnadou na Prince Dube lakini ameonyesha ubora wake na kupenya mbele ya nyota hao wa kigeni.

Katika msimu wake wa kwanza akicheza pamoja na Fiston Mayele aliyekuwa mshambuliaji tegemeo wa kikosi hicho na kucheza kwa mafanikio misimu miwili akifunga mabao 33, Mzize ambaye alikuwa akiingia dakika za jioni alitumika kwa dakika 641 katika mechi 20 na kufunga mabao matano na asisti moja.

Dirisha dogo, licha ya Yanga kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji kwa kumsajili Keneddy Musonda, Mzize bado aliendelea kupambana na msimu wa pili kinara wa mabao akiwa ni Mayele aliyefunga 17, nyota huyo anayetumia miguu yote miwili na mwinye mwili jumba, alivunja rekodi yake ya mabao na kufikisha saba katika mechi 29 akicheza dakika 1404.

Hata baada ya kuondoka Mayele na kudhaniwa Musonda ndiye angerithi mikoba yake kwenye kupachika mabao, hajawa tishio kwa Mzize na aliendelea kuonyesha moto wake akipata nafasi zaidi za kucheza na kuongeza kasi ya kujituma.

Mbali na Musonda, Yanga ilimuongeza pia Hafiz Konkon aliyeshindwa kudumu kwenye kikosi hicho kwa kushindwa kuendana na kasi na alifunga bao moja tu, huku Mzize akiendelea kuonyesha ubora wake na huu ndiyo msimu wake bora akiwa amecheza mechi 21 na kufunga mabao 10 hadi sasa akiwa ni mmoja wa wanaowania kiatu cha ufungaji bora wa msimu ligi kuu.

NABI AMWAMINI, AITWA STARS

Aliyekuwa Kocha kipenzi cha Wanajangwani, Nasreddine Nabi ndiye alianza kumtumia baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana.

Hata hivyo, licha ya kumpa dakika chache za kucheza, alionyesha kiwango kutokana na kutumika katika mechi nyingi msimu wake wa kwanza hadi kupata nafasi ya kuitwa kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars mwaka 2023.

Kutokana na kiwango chake na kumpa dakika chache, Nabi aliwahi kusema hakuwa na haraka ya kumtumia mshambuliaji huyo baada ya kumwelewa na hakutaka kumpa presha, huku akimtabiria anaweza kuwa mmoja wa washambuliaji hatari wa Kitanzania miaka ijayo.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga alishawahi kuweka wazi kuwa chini yake hakutaka kumpa presha mshambuliaji huyo alikuwa anaamini kuwa atakuja kufanya vizuri.

MZ 03

VITA KWA GAMONDI ILIKUWA KUBWA

Kwa Kocha Miguel Gamondi Mzize hakuwa na muda mzuri licha ya kuwa na ubora na hakumtumia kama chagupo lake la kwanza.

Kocha huyo Muargentina alimtumia zaidi Stephane Aziz KI kama mshambuliaji tegemeo. Hata hivyo, Mzize hakukata tamaa na aliendelea kuwa wa moto kwa muda aliocheza.

Pamoja na kuonyesha ubora, akiwamo pia Musonda, ni kama Gamondi hakuridhika na alihitaji kuongezewa mshambuliaji mwingine na chaguo likawa kwa Dube.

Hata hivyo, licha ya ujio wa Dube ambaye naye amekuwa wa moto msimu huu akionekana kuwa mrithi wa Mayele, hata hivyo hakuanza na kasi na kwa Mzize ni kama ametiwa ndimu na amekuwa imara zaidi na wawili hao hadi sasa wamelingana mabao wakiwa nayo 10 kila mmoja.

KWA RAMOVIC KATAMBA

Baada ya kuondoka Gamondi, Yanga ilimleta Kocha raia wa Ujerumani Sead Ramovic na alimpa nafasi zaidi Mzize acheze sambamba na Dube huku Musonda akisubiri benchi.

MZ 04

KASI, NGUVU, MIKIMBIO

Unora wa Mzize ambaye amekuwa kipenzi cha Wanajangwani, ni wazi unatokana na kasi, nguvu, mikimbio yake na ufundi miguuni pamoja na mashuti.

Mzize ana uwezo wa kukokota mpira kwa kutumia miguu yote na haishangazi kuona klabu mbalimbali kubwa barani Afrika na Ulaya zikipigana vikumbo kuwania saini yake.

Hilo limemfanya awe na uwezo wa kutumika katika nafasi zote za mbele na amekuwa pia akirudi kusaidia kukaba na kutengeneza mashambulizi licha ya kuwa ndiye mfungaji na makocha waliomfundisha wamekuwa wakimtumia katika nafasi zaidi ya moja.

NAFASI HII NDO ANAIPENDA

Mshambuliaji huyo mwenyewe alishawahi kufunguka anafurahi zaidi akitumika pembeni (winga) kutokana na mguu wake wa kushoto kuwa na nguvu ya kukokota mpira na kuingia nao ndani ya 18, licha ya kuwa na uwezo wa kucheza popote atakapopangwa.

MZ 05

HAZINA TIMU YA TAIFA

Kama alivyowajhi kusema Nabi, Mzize atakuja kuwa mmoja wa washambuliaji hatari ndivyo inavyosadifu na kwa sasa ni mmoja wa nyota wa kutumainiwa Stars.

Mzize anatajwa kuja kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Stars kwa miaka mingi akiwa ni mrithi wa nyota wa timu hiyo ambao muda unawatupa mkono kama nahodha Mbwana Samatta, John Bocco aliyestaafu na Simon Msuva.

Kwa maelezo yoyote mtu anaweza kutumia kumwelezea chipukizi huyo aliyetokea Iringa, ulikuwa mwanzo mzuri kwake kwenye timu yenye ‘Presha’ kubwa zaidi kutoka kwa mashabiki wake na kuisaidia kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili ya Kombe la FA na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika misimu yake mitatu hadi sasa.

MZ 06

OFA ZA MZIZE

Inaripotiwa presha inaendelea kuwa kubwa kwa mabosi wa Yanga kutokana na ofa zinavyomiminikia kumhitaji mshambuliaji wao huyo mzawa.

Inaelezwa Yanga kwa sasa inapiga hesabu za kufanya biashara ya mshambuliaji huyo, wakitafuta na kupima kwa mizani ofa kubwa zaidi ambayo pia itakwenda kumboresha kinda huyo.

Ofa hizo zimeibua maswali kwa mashabiki wakijiuliza ni kwa nini uongozi unashindwa kufanya biashara ya kumuuza na kutafuta mastaa wengine watakaoisaidia Yanga bila uwepo wake.

Mshambuliaji huyo alianza kutafutwa na Olympic Marseille ya Ufaransa, ambayo ilimtumia Mkurugenzi wa ufundi wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera aliyesema Marseille walishatuma mualiko wa kinda huyo kutakiwa kwa majaribio ya wiki mbili yatakayofanyika nchini humo.

Marseille ilimuona kinda huyo katika mashindano ya soka la vijana chini ya miaka 20 na alionyesha kiwango bora akifunga mabao saba na kuwa mfungaji Bora.

Baadae Mzize alihusishwa na Azam FC kwa timu za ndani wakimwekea mezani Sh400 milion, sasa mambo yanazidi kuwa mazuri upande wake akitajwa kutakiwa na Wydad ya Morocco na Al Ittihad.