Mzize akutana na Wydad AC

SIKU za mshambuliaji Clement Mzize ndani ya Yanga ni kama zinahesabika baada ya kubakiza hatua moja tu kukamilisha dili lake la kutua Wydad Athletic ya Morocco.

Wydad imezidi kupiga hatua kubwa ya kumng’oa Mzize ndani ya Yanga, baada ya sasa kumalizika makubaliano ya kimaslahi kati ya Waarabu hao na mshambuliaji huyo.

Meneja anayesimamia dili hilo, Zambro Traore, amekutana na Rais wa Wydad, Hicham Ai Manna nchini Morocco na kufikia hatua nzuri ya makubaliano ya kimaslahi na mshambuliaji huyo.

Wydad inataka kuboresha zaidi safu yake ya ushambuliaji ambapo umri wa Mzize mwenye miaka 21, pamoja na ubora wake umeishawishi klabu hiyo kuweka dau walilolitaka Yanga ili imchukue mwisho wa msimu huu.

Taarifa zinasema klabu hiyo inataka kuipa Yanga Sh1.7 Bilioni kwenye kununua mkataba wa mshambuliaji huyo ambaye pia anaitumikia timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Msimu huu ndani ya Yanga, Mzize ni staa muhimu akiwa kinara wa ufungaji katika kikosi cha timu hiyo akifunga mabao 10 katika Ligi Kuu sawa na mshambuliaji mwenzake Prince Dube.

Hatua pekee iliyosalia sasa ni Hicham kumalizana na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said ambapo Wydad inataka kuimaliza haraka.

Yanga wako tayari kumuuza Mzize mwisho wa msimu huu huku pia uamuzi huo ukienda sambamba na kutafuta mrithi wake akitajwa kuwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah ndiye ambaye anakwenda kuvaa viatu vyake.

Ingawa wasimamizi wa Mzize wanafanya siri lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa kulikuwa pia na kikao kati ya mshambuliaji huyo na Hicham wakati akiwa nchini Morocco hivi karibuni na kikosi cha Taifa Stars.

Endapo dili hilo litakamilika, Mzize anaweza kuwa staa wa pili Mtanzania kwenye safu ya ushambuliaji ya Wydad akitanguliwa na Seleman Mwalimu aliyetua hapo Januari mwaka huu akitokea Singida Black Stars.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *