
Miaka 30 iliyopita, kulikuwa na staa mmoja wa soka la Colombia, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi huko kwao. Unajua ilikuwaje?
Ni stori ya kuhuzunisha ya Andrés Escobar Saldarriaga (Gentleman), moja ya mastaa waliokumbwa na janga kubwa kuwahi kutokea kwenye soka.
Staa huyo alikuwa beki wa timu ya taifa ya Colombia na klabu za Atletico Nacional, alipigwa risasi na kupoteza maisha akiwa na umri wa miaka 27.
Ilikuwa ni baada ya fainali za Kombe la Dunia 1994 zilizofanyika Marekani.
Escobar alibebeshwa lawama kwamba ndiye chanzo cha timu yake ya Colombia kutolewa kwenye hatua ya makundi ya fainali hizo za Kombe la Dunia.
Beki huyo alijifunga kipindi cha kwanza katika mechi ambayo Colombia ilifungwa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Marekani.
Huo ulikuwa mchezo wa pili wa makundi kwa Colombia katika fainali hizo za dunia na kuifanya nchi hiyo kushindwa kuvuka hatua hiyo licha ya kuifunga Uswisi katika mechi ya tatu.
Kabla hata wiki haijaisha tangu Colombia itupwe nje kwenye fainali hizo, Escobar aliuawa nje ya kumbi moja ya usiku ya huko Medellin nchini humo.
Mtu aliyekamatwa na kuhusishwa na mauaji hayo alikuwa Humberto Castro Munoz, mlinzi na dereva wa kundi la wahalifu la wauza dawa za kulevya katika miji mikubwa ya Colombia.
Inaelezwa kulikuwa na mgogoro mkubwa wa biashara ya dawa za kulevya aina ya cocaine na maofisa wa soka la Colombia.
Makundi ya uhalifu ya wauza dawa za kulevya yalikuwa yakiwekeza kwenye timu za soka za Colombia, ambapo kuna wakati hata Atletico Nacional ilifadhiliwa na muuza dawa maarufu duniani, Pablo Escobar.
Mauaji ya beki Escobar yaliishtua dunia yakihusishwa pia na masuala ya kamari.
Licha ya kwamba sababu halisi ya beki huyo kupigwa risasi bado haijafahamika, kulikuwa na sintofahamu wengine wakihusisha goli la bahati mbaya alilojifunga kuwa chanzo.
Wacheza kamari wa upande fulani nchini humo waliamini beki huyo alijifunga makusudi ili ‘kuwachania mikeka’.
Miaka 30 imepita tangu kutokea kwa tukio hilo baya lililoishtua dunia, hapa nchini chokochoko zimeanza.
Waswahili husema panapofuka moshi, moto utawaka! Ndiyo hali halisi inayoendelea hivi sasa katika soka la Tanzania.
Mashabiki kuwazomea wachezaji na kuwahusisha na masuala ya betting pale wanapofanya makosa ya kimchezo imekuwa ni kawaida.
Si ajabu leo hii mchezaji wa timu fulani kuzomewa na kuambiwa amebeti pale inapotokea amefanya ndivyo sivyo katikati ya mechi.
Mifano ipo kwa baadhi ya wachezaji akiwamo kipa wa moja ya timu maarufu nchini kukutana na kadhia hiyo baada ya timu yake kufungwa mabao kwenye mechi tatu mfululizo, yeye akiwa golini.
Japo hakuna uhusiano wa mabao aliyofungwa na shutuma za betting kwa wachezaji, lakini baadhi ya mashabiki wanamnyooshea vidole kwa madai hayo, wakihusanisha aina ya mabao aliyofungwa, muda anaofungwa.
Nyuma ya pazia
Japo wamekiri kutojua undani wa kila mchezaji, kwa nyakati tofauti baadhi ya wachezaji wamesema madai hayo yanasababisha kuwatoa mchezoni hususani pale anapotokea kufanya kosa la kimchezo.
Hapa nchini, haijathibitika moja kwa moja mchezaji, kiongozi, refarii na watu wengine wanaohusika na soka kujihusisha na kamari au kupanga matokeo, lakini hivi sasa wachezaji ndiyo waathirika wa hilo, baadhi yao wakilaumiwa kubeti.
Wakati fukuto hilo likiendelea, baadhi yao wameeleza kinachochochea hali hiyo na wao kuhusishwa na kamari na namna wanavyokabiliana nayo.
Mchezaji wa Pamba Jiji inayoshiriki Ligi Kuu Bara, Ibrahim Abdallah anasema japo kila binadamu ana akili yake, lakini itakuwa ni fedhea sehemu inayokupa kipato cha uhakika kuihujumu.
“Tumesikia taarifa za wachezaji kubeti, hilo ni kosa, lakini inawezekanaje mtu unalipwa mshahara wa uhakika mzuri kisha anayekulipa mshahara unamhujumu?,” anahoji na kuendelea.
“Siwezi kumsemea kila mchezaji, maana kila mmoja na moyo na akili yake, hivyo kama kweli wapo wanaofanya hivyo, ni bora waachache kabla ya kufika kubaya,” anasema mchezaji huyo baada ya hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda kusema kuwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wanacheza kamari.
Kuhusu maneno na kejeli za mashabiki, Abdallah anasema maneno ya mashabiki huwa ni ya kawaida kwa mchezaji.
“Ukiyazingatia ndiyo yatakutoa mchezoni, si kwenye madai ya kamari tu, hata wakati mwingine unakosea kutoa pasi mtu anakutukana hadi na wazazi wako, lakini unachukulia kawaida maisha yanasonga, japo si kitu kizuri,” anasema.
Pius Buswita wa Namungo anasema wachezaji kuhusishwa na kamari kuna athari za moja kwa moja ambazo wanakutana nazo.
“Kuna nyakati maneno yanakutoa mchezoni kwa kuwa kuna vitu shabiki atavisema kutokana na uhalisia wako unajisikia vibaya kama binadamu,” anasema.
Anasema si Tanzania tu, hata Ulaya wachezaji wanafanya makosa uwanjani, kwa kuwa mpira ni mchezo wa makosa.
“Hakuna anayekosea makusudi uwanjani, lakini mashabiki siku zote wana maneno mengi na huwezi kuwakataza, mchezaji ukikosea halafu ukaambiwa unabeti, lazima utajisikia vibaya, wengine inawatoa mchezoni kabisa.
“Hata hivyo, ukweli wa kile kinachosemwa unakijua mchezaji, unajipa moyo kwamba maisha lazima yaendelee, kwani kuna siku utapatia, ukipatia mbona huwa hawasemi umebeti?,” anasema Buswita.
Wakati akisema hivyo, staa wa Coastal Union, Gerald Gwalala anasema mchezaji anapokosea uwanjani kwa bahati mbaya na kosa hilo kuhusishwa na kuwa amebeti ni kumkosea.
“Hata Ulaya makosa ya uwanjani yanatokea, wachezaji wakubwa kabisa wanakosea na ni jambo la kawaida kwa mchezaji, unapomhusisha na kamari ni kumkosea tena sana kwa kuwa anatoka jasho kwa ajili ya timu,” anasema.
Anasema, kejeli za mashabiki wapo baadhi ya wachezaji zinawatoa mchezoni kabisa, hasa wale ambao ni chipukizi.
“Kwa mchezaji mkubwa anachukulia ni kawaida, mfano ni mimi inapotokea nimepata vikwazo vya mashabiki, huwa inanipa hamasa ya kupambana na kufanya vizuri zaidi ili wakose cha kusema, lakini wapo wachezaji wanaweza kushindwa kucheza,” anasema.
Pamba wachunguzana
Katika muendelezo wa fukuto hilo, hivi karibuni, mlezi na mshauri wa timu ya Pamba ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda aliwashutumu wachezaji wa timu hiyo kujihusisha na kamari ikiwa ndiyo timu pekee ambayo imetoka hadharani kukemea hilo.
Aliwaeleza wazi wachezaji, benchi la ufundi na menejimenti ya klabu hiyo katika hafla ya chakula cha usiku kuelekea michezo ya mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara kwamba ana taarifa za upangaji matokeo ndani ya klabu hiyo ya Ligi Kuu.
Ili kuonyesha msisitizo wa madai yake, Mtanda alisema tayari wamewasilisha majina ya wachezaji wote wa kikosi chao kwenye Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufuatilia nyendo zao katika madai hayo.
Mbali na Pamba, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakitoa lugha za kuwashutumu wachezaji mara kadhaa kufanya betting wanapokuwa uwanjani.
Katika mechi kadhaa, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakitumia shutuma hizo kuwakebehi na kuwazomea wachezaji wakiwahusisha na na kamari.
Kanuni za Fifa zinasema hivi
Kanuni za Maadili za Shirikisho la Soka Kimataifa Duniani (FIFA) Ibara ya 27, inaelezea kujihusisha na kamari au shughuli kama hizo.
Inasema watu waliofungwa na kanuni hii wanakatazwa kushiriki ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika kamari, bahati nasibu au matukio kama hayo ama miamala inayohusiana na mechi za kandanda au mashindano na/au yoyote inayohusiana na shughuli za soka.
Watu waliofungwa na kanuni hii hawatakuwa na fedha za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja au maslahi (kupitia au kwa kushirikiana na wahusika wengine) katika shughuli, kama vile kuweka dau, kamari, bahati nasibu au matukio kama hayo au miamala inayohusiana na mechi za soka na mashindano. Maslahi ni pamoja na kupata chochote kinachowezesha faida kwa watu waliofungwa na kanuni hii wenyewe na/au wanaohusiana vyama.
Isipokuwa kwamba mwenendo husika haujumuishi ukiukwaji mwingine wa kanuni hii, ukiukaji wa kifungu hiki utaidhinishwa na faini ya angalau Faranga ya Uswisi 100,000 (Sh280 milioni) na kupigwa marufuku kushiriki katika masuala yoyote ya soka kwa muda usiozidi miaka mitatu.
Mastaa waliokutana na ‘rungu’
Kwenye soka huko duniani, baadhi ya mastaa wamekutana na ‘rungu’ la kufungiwa au kupigwa faini kwa kujihusisha na kamari huku kesi ya Ivan Toney ikiibua mjadala mkubwa kuhusu tatizo hilo.
Mbali na Toney, kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali ni mchezaji wa hivi karibuni kupigwa marufuku kwa kosa la kamari.
Tonali alijiunga na Newcastle United kwa ada ya pauni milioni 55 mwezi Julai 2023, alipoteza msimu wa 2023/24 pamoja na nafasi ya kushiriki Euro 2024 alipofungiwa kwa kosa la kamari.
Awali, alikiri kubashiri ushindi wa AC Milan japo adhabu yake ilipunguzwa kutoka miaka mitatu hadi miezi 10 hadi Agosti 2024.
Vilevile baadhi ya wachezaji kama Joey Barton na Daniel Sturridge walikumbwa na marufuku kali na faini kubwa, huku wengine kama Andros Townsend wakipata adhabu nyepesi kwa nyakati tofauti.
Itaendelea kesho