
MAMBO bado hayajaeleweka kwa Kocha mpya wa Tabora United, Genesis Mang’ombe raia wa Zimbabwe baada ya kushindwa kupata ushindi tangu atue klabuni hapo akirithi nafasi ya Mkongomani, Anicet Kiazmak aliyeiongoza mechi 14 na kushinda nane, sare tano na kupoteza moja.
Mang’ombe aliyetambulishwa klabuni hapo Machi 28, mwaka huu na tangu timu hiyo iliposhinda bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji Februari 28, 2025 haijashinda tena.
Chini ya Mzimbabwe huyo, Tabora United imeng’olewa kwenye Kombe la Shirikisho kwa kufungwa penalti 5-4 na Kagera Sugar baada ya sare ya 1-1, kisha ikabamizwa mabao 3-0 na Yanga na jana imefungwa bao 1-0 na Pamba Jiji.
Akizungumza baada ya kichapo cha bao 1-0 mbele ya Pamba Jiji katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mang’ombe alilalamikia mambo manne yaliyochangia kufanya vibaya ikiwemo ugeni wake kwenye soka la Tanzania na ufinyu wa ratiba unasababisha uchovu kwa wachezaji.
Mambo mengine ni madhaifu ya marefarii yanayosababisha kutokuwa na usawa katika uchezeshaji na kuwanyima burudani mashabiki, huku changamoto ya umakini katika eneo la umaliziaji la kikosi chake nalo likichangia kumkwamisha hadi sasa.
“Mimi ni mgeni katika ushindani wa soka la Tanzania na najifunza mengi na jinsi mambo yanavyokwenda, yanayonisaidia na mwishowe tunachotaka ni kuimudu kila timu kwenye ligi,” alisema Mang’ombe na kuongeza;
“Ukitazama katika upande wa kucheza, tumefanya vizuri leo (juzi), nafikiri timu yangu imekosa tu bahati hasa kipindi cha kwanza kwani tumetengeneza nafasi kadhaa lakini umaliziaji ndiyo lilikuwa tatizo kubwa kwetu.”
Alisema uchovu wa safari baada ya kucheza mechi mbili dhidi ya Yanga na Pamba Jiji katika siku tatu, umewagharimu lakini akawapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kupambana bila kuchoka na kuonyesha soka la kuvutia.
“Mwamuzi hakupaswa kuongeza dakika tatu kwani muda mwingi ulipotea na hata ukiangalia faulo nyingi kwenye kuwania mpira tuliadhibiwa sisi, nafikiri hili eneo linapaswa kuboreshwa ili mchezo uwe wa haki kwa sababu mashabiki wanataka kuona mchezo wa kusisimua na siyo wa upande mmoja,” amesema Mang’ombe.
Aliongeza; “Hata hivyo, tunakubali matokeo, tunarudi kwenye ubao wa mazoezi kuyakabili madhaifu yetu na uimara wetu ili tusonge mbele. Naishukuru timu yangu kwa kupambana hadi mwisho.”