Mziki wa Maxi wamgusa Hamdi

KIUNGO mshambuliaji, Maxi Nzengeli juzi alifunga mabao mawili wakati Yanga ikitinga 16 Bora kwa kuiondosha Coastal Union kwa mabao 3-1 katika mechi ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho, huku kocha Miloud Hamdi akishindwa kujizuia kwa namna nyota huyo anavyomsapraizi uwanjani.

Katika mchezo huo, Maxi alifunga bao la kwanza katika dk2 kabla ya kuongeza jingine dk15 na Clement Mzize aliongeza la tatu dk21 baada ya Miraji Abdallah kuifungia Coastal bao la kufutia machozi dk18 kwa shuti kali la mbali, lililomshinda nguvu kipa Abuutwalib Mshery.

Bao alililofungwa Mshery, lilikuwa la kwanza kwa kipa huyo dhidi ya Coastal tangu aliposajiliwa dirisha dogo la msimu wa 2021-2022, akitokea Mtibwa katika dakika 540 alizokutana nao kuanzia ile akiwa na Mtibwa Sugar kabla ya kuhamia Yanga, nne zikiwa za Ligi Kuu na moja na Shirikisho.

Kocha wa Yanga, aliliambia Mwanaspoti amekuwa anashangazwa na maajabu anayoyafanya Maxi, hasa kwa jinsi anavyofanya kazi yake akisimamia misingi ya soka, hivyo kumrahisishia jukumu la kumuelekeza kwani hatumii muda mrefu awapo uwanjani.

Hamdi tangu aliyejiunga na Yanga chini yake timu imecheza mechi sita zikiwamo tano za Ligi Kuu na moja ya Kombe Shirikisho, imeshinda tano na kutoka sare moja, huku akitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Februari, alisema Maxi amekuwa akimshangaza mara kadha kwa utendaji wake.

“Nzengeli (Maxi) amekuwa mchezaji mwenye nidhamu ya juu, anaweza akatoka katika majeraha ukimpa nafasi ya kucheza anaonyesha kiwango cha juu. Wachezaji wa aina yake ni nadra sana,” alisema Hamdi na kuongeza;

“Navutiwa na aina ya uchezaji wake ana mchango mkubwa katika kikosi cha Yanga pia ni mchezaji mwenye nidhamu, ubora alionao unatokana na kujituma kwake uwanjani katika mechi na hata mazoezini nafurahishwa na upambanaji wake.

“Nzengeli (Maxi) anaonekana katika nafasi zote uwanjani ndiye mchezaji anayekimba kilometa nyingi uwanjani amekuwa na msaada mkubwa wa kubalansi timu iwe kwenye kushambulia unamuona na katika kukaba pia.”

Hamdi aliongeza, Maxi anampa vitu vingi uwanjani kutokana na kuweza kushambulia, pia ni mzuri kushuka kusaidiana na mabeki wa timu hiyo katika majukumu ya ulinzi.

Nyota huyo alikuwa mchezaji pendwa kwa kocha waliyemtangulia Hamdi kuanzia Miguel Gamondi na Sead Ramovic, japo aliumia na kuwa nje kabla ya kocha wa sasa kujiunga na timu.

Maxi alijiunga na Yanga akitokea AS Maniema ya DR Congo na msimu wake wa kwanza chini ya Gamondi alionyesha uwezo mkubwa akicheza kwa kujituma na kufanya kuwa mchezaji aliyecheza muda mwingi zaidi kwenye ligi ni mchezo mmoja tu ndiyo hakucheza dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hana msimu bora kama ulivyokuwa msimu wa kwanza alipokuwa akijiunga na Yanga hii ni kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mwanzoni mwa msimu huu.

Maxi hadi sasa kwa msimu huu Yanga ikiwa imecheza mechi 23, yeye amecheza mechi 18 akihusika katika mabao 10 ya Ligi Kuu baada ya kufunga manne na kuasisti sita, wakati Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo na alama 58 na kufunga mabao 58 na yenyewe kufungwa tisa kupitia mechi hizo 23 za Ligi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *