Mzee wa fact: Vita vya Ronaldo na Ten Hag inamtesa Garnacho

Kwa mara ya kwanza tangu aondoke Manchester United mwaka 2022, Cristiano Ronaldo aliibuka wiki iliyopita na kurusha makombora kwa kocha aliyemuondoa klabuni hapo, Erik Ten Hag.

Ronaldo alikosoa mambo kadhaa ya Ten Hag katika uendeshaji wa klabu hiyo, hasa kauli yake ya kuwa Manchester United haipo tayari kwa ubingwa.

Awali baada ya maandalizi ya msimu mpya, kocha Erik Ten Hag akiongea na chombo kimoja cha habari cha Uholanzi, hakuipa klabu yake nafasi ya ubingwa wa England au wa Ulaya msimu huu.

“Bado tuna safari ndefu sana hadi tuje kufikia malengo ya kutwaa ubingwa”, alisema Ten Hag, akizungumza na jarida la AD Sportwereld.

Akizungumza kupitia kipindi cha podicast cha Rio Ferdinand Presents cha nyota mwenzake wa zamani wa Manchester United, Ronaldo hakukubaliana na maneno haya.

 “Kama kocha wa Manchester United, huwezi kusema eti huwezi kupambana kushinda ligi kuu au ligi ya mabingwa.”

 Kauli hii ikamfikia Ten Hag ambaye hakufurahishwa nayo, na akajibu kwa ng’ong’o pale alipoulizwa kama ameisikia.

“Yuko mbali huko Saudi Arabia, hivyo mtu yeyote anaweza akawa na mawazo yake na yeye ana haki ya kuwa na maoni. Ni sawa tu.”

GARNACHO ANAINGIAJE HAPO

Habari hii iliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari, akiwemo mwanahabari maarufu wa Italia, Fabrizio Romano.

Garnacho, kinda wa Manchester United ambaye ni raia wa Argentina na shabiki mkubwa sana wa Ronaldo, akaenda ku-like habari hii kwa Fabrizio Romano.

Hapo hapo mjadala ukaanza mitandaoni kwamba dogo kaonesha dharau kwa kocha wake kwa kuipenda habari inayomkosoa, tena kutoka kwa mchezaji ambaye ni adui wa kocha japo ni rafiki yake yeye.

Mchezo wa kwanza wa Manchester United baada ya sakata hili ulikuwa wa ugenini dhidi ya Southampton, Septemba 14.

Ten Hag akampiga benchi Garnancho kwenye mchezo huo, na kuibua minong’ono kwamba dogo anaadhibiwa kwa kuipenda taarifa ya kumkosoa kocha.

Zikiwa zimesalia dakika 17, Garnancho akapewa nafasi na dakika ya mwisho kabisa ya mchezo akafunga bao la tatu kwa Manchester United.

Dogo huyo alivyo na nongwa, akaenda kushangilia karibu na kocha wake kwa staili ya Cristiano Ronaldo.

Hii ikaibua tena mjadala kwamba dogo anamtafuta ubaya kocha wake.

Japo baada ya mchezo, Ten Hag akakanusha taarifa za kwamba alimpiga benchi kutokana na kupanda ile taarifa, akisisitiza kuwa ni maamuzi ya kiufundi.

Mapenzi ya Garnancho kwa Ronaldo yamemletea shida mara kadhaa kwenye kambi ya timu yake ya taifa, Argentina.

Hii ni kutokana na ushindani mkubwa kati ya nahodha wake Lionel Messi na Ronaldo.

Kitendo cha yeye kumhusudu zaidi Ronaldo badala ya Messi hakikupokelewa vizuri na wachezaji wenzake wa timu ya taifa, na kumfanya awe mpweke kambini.

Wachezaji wengi wa kizazi chake nchini Argentina ndoto zao ni kuwa kama Messi, lakini yeye akawa tofauti, ndoto yake ni kuwa Ronaldo.

Novemba mwaka jana Garnacho alifunga moja ya mabao bora dhidi ya Everton, kama bao la Ronaldo dhidi ya Juventus mwaka 2018.

Na kama haitoshi, akashangilia kwa staili ya Siuuu kama alivyofanya Ronaldo.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Argentina hawakuliacha hili lipite hivi hivi.

Nyota wa AS Roma ya Italia, Leandro Parades, akasema wanapokuwa naye kambini humtania sana kwa hilo, na mara zote amekuwa mpole akiishia kukaa kimya.

Yawezeka kwenye timu ya taifa akawa anataniwa na wenzake lakini siyo Manchester United.

Erik Ten Hag hawezi kufanya utani kwenye mambo serious kama haya, kwa hiyo bwana mdogo ajiangalie  hasa.

Ronaldo aliondolewa Manchester United kwa maneno maneno yake.

Usimuudhi mchinja mbwa, wazimu utakurudia…aangalie sana.

Ten Hag alimchinja Ronaldo, wazimu usije ukamrudia bwana mdogo!