
Mechi mbili za Taifa Stars dhidi ya DR Kongo kwa ajili ya kufuzu AFCON 2025, zilitoa somo kubwa sana kwa mamlaka zetu za mpira Tanzania.
Wenzetu Kongo walizichukulia mechi hizi kwa uzito mkubwa na kuwekeza pesa nyingi, ilihali sisi tukihamasishana uzalendo.
Wachezaji wa Kongo wameogelea mamilioni kwenye hizi mechi, sisi wa kwetu wametoka kapa.
Picha inaanza siku ya kuwasili. Wachezaji wa Kongo walipewa kila mmoja dola elfu mbili kwa siku, kwa siku zote nane ambazo walipaswa kuwepo timu ya taifa.
Wachezaji hao walianza kuwasili tarehe 7 Oktoba na wakaa kambini hadi tarehe 15 baada ya mechi ya Dar es Salaam.
Kwa siku hizo nane, kila mchezaji alipata dola elfu kumi na sita za Marekani, zaidi ya shilingi milioni arobaini za Tanzania.
Baada ya mechi ya Kinshasa, wachezaji wa Kongo walipewa pesa ambazo ni sawa na shilingi za Tanzania milioni 15 kama bonasi ya ushindi dhidi ya Tanzania.
Na baada ya mechi ya Dar es Salaam, wachezaji hao walipewa zaidi ya hizo kama bonasi ya ushindi na kufuzu AFCON.
Kwa jumla kwa siku hizo nane na mechi mbili dhidi ya Tanzania, kila mchezaji wa Kongo alipata zaidi ya shilingi milioni hamsini za Tanzania.
Sasa njoo kwa wachezaji wa Tanzania. Hawakupata pesa za kujikimu wala hakukuwa na ahadi yoyote endapo wangeshinda.
Mbaya zaidi, baada ya mechi ya Tanzania inaelezwa, Rais wa TFF Wallace Karia aliingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kuanza kulaumu kwamba wachezaji wanawaza hela tu badala ya uzalendo.
Eti timu ya taifa ni uzalendo, unapigania taifa lako, siyo kuchuma pesa.
Hata kama timu ya taifa ni uzalendo, ndiyo wasipewe hata shilingi?
Watu walidhani watasikia neno fulani la kutia moyo baada ya jasho lao jingi walilomwaga uwanjani, lakini wakaishia kulaumiwa ‘kupenda sana hela’.
Rais Karia akamalizia kwa kumtaka Mbwana Samatta kuwahamasisha wachezaji wenzake kwenye mchezo wa kufuzu CHAN, Oktoba 27.
Mawazo ni hamasa, hamasa, hamasa. Hivi kweli tunawaza kushinda mataji au kufanikiwa kimataifa kupitia hamasa bila kuwekeza hata shilingi kwenye mifuko ya wachezaji wetu?
Yawezekana TFF haina pesa za kutosha, hata wale Kongo waliooga ‘mapesa’ siyo bajeti ya chama chao cha soka, bali Serikali.
Na sisi Serikali tunayo, tena imara kuliko ya Kongo cha muhimu ni kwa TFF kutengeneza ushawishi kwa sababu Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameshaonesha nia ya kuunga mkono michezo, aelekezwe tu maeneo ya kuunga mkono.
Alinunua tiketi 20,000 kwa ajili ya ule mchezo, asingeshindwa kufanya zaidi ya hapo kama TFF wangepeleka ombi kwake.
Mama Samia amekuwa mstari wa mbele kufanya mambo mengi kuhusu mpira, akieleweshwa hili, hawezi kuliacha.
Timu ya taifa ni mali ya serikali, na ndiyo inakabidhiwa bendera na inapigiwa wimbo wa taifa.
Ni jukumu la TFF kukaa na Serikali kuielezea mahitaji halisi ya soka la kulipwa.
Hata kama kuchezea timu ya taifa ni uzalendo, lakini hawa wachezaji wana familia zao hawawezi kuzilisha kwa uzalendo.
Watoto wao hawasomi kwa uzalendo bali kwa kulipa ada. Wakiugua hawatibiwi kwa uzalendo bali kwa kulipia malipo yao.
Sasa kwanini kazini kwao walipwe uzalendo?
Hata wanajeshi wanapoenda vitani, hisisitizwa uzalendo, lakini hulipwa pesa, tena nyingi sana.
Wachezaji ni sawa na wanajeshi wanaoenda kulipigania taifa, wanaweka uzalendo mbele lakini lazima walipwe.
Yawezekana hata Samatta mara kadhaa amekuwa akitaka kustaafu timu ya taifa kuyakwepa haya.
Bila shaka yeye kama nahodha na mchezaji mkubwa, anawiwa kuwatetea wenzake, kama akina Samuel Eto’o walivyokuwa wakifanya enzi zao.
Lakini labda anaogopa kuchafua taswira yake kwa sababu atakuwa anafichua vitu ambavyo havitakiwi kufichuliwa.
Sasa ya kazi gani kujichafua ilhali anaelekea kumaliza soka lake, si ni bora awaachie tu timu yao!?
Ndiyo maana utasikia, ‘Samatta hajaitwa kwa sababu maalumu lakini tuliongea naye’.
Haya ni mawazo yangu yanayokuja kutokana na mambo yanavyokwenda. Siamini kama Samatta hakutani na hii presha ya kuwasemea wenzake.
Na TFF inawaonea hawa wwchezaji kwa sababu wanacheza soka letu la ndani na hawana mwamko kama wengine wanaocheza nje.
Ingekuwa nchi zingine, wachezaji wangegoma kuchezea timu ya taifa. Imeshatokea mataifa mengi sana, lakini hapa kwetu nani amvike panya kengele?
Tusiishie kuwahimiza wachezaji kuwa wazalendo. Hawa wachezaji wetu ni wazalendo hasa.
TFF na nyie kuweni wazalendo kwa kuwalipa pesa, hawa ni wachezaji wa kulipwa, wanatakiwa kulipwa!