
Katika historia ya mamlaka ya kitaifa ya soka nchini, kuanzia FAT hadi TFF, ni Leodeger Tenga pekee ndiyo aliongoza na kumaliza muda wake kwa amani kabisa.
Wengine wote waliishia kutolewa kwa nguvu na serikali baada ya tawala zao kuzalisha migogoro na mahusiano mabaya baina ya wadau wakuu wa mchezo huu, na hata serikali yenyewe.
Wallace Karia ambaye kwa sasa anamalizia muhula wake wa pili na ameshatangaza nia ya kugombea muhula wa tatu, anaelekea kupita njia ya Tenga kama kiongozi aliyetuliza hali na kujenga mahusiano mazuri baina ya wadau wote wa mpira.
Wafuatao ni viongozi wa mamlaka ya kitaifa ya soka hapa nchini, tangu 1964 pale Tanzania ilipotambuliwa na kupewa uanachama na Shirikisho la Soka la Kimataifa, (FIFA).
1. BALOZI J MAJJID
Kabla ya uhuru, wakati nchi ikiitwa Tanganyika, chama cha soka kiliitwa TAF, yaani Tanganyika Football Association.
Baada ya Muungano, mwaka 1964, jina likabadilika na kuwa FAT, yaani Football
Association of Tanzania.
Balozi J Majjid alikuwa rais wa mwisho wa TAF na wa kwanza wa FAT.
Yeye ndiye aliyekuwepo madarakani wakati wa muungano na ndiye
aliyeshughulikia uanachama wa FIFA.
Zaidi Majjid, atakumbukwa kwa kuanzisha ligi ya kitaifa, hii tunayocheza sasa ikifahamika kama NBC Premier League. Alianzisha ligi hii mwaka 1965 kwa jina la Klabu Bingwa ya Taifa, maisha yakaendelea hadi sasa ni Ligi Kuu ya NBC.
Hata hivyo, kuanzisha ligi hii ni kama alijipalia makaa ya mawe kwani ilimsababishia misukosuko mingi hadi alipoondolewa madarakani kwa nguvu na serikali.Ilikuwa mwaka 1969 katika mkasa uliosababisha mechi ya watani wa jadi, Simba (wakati ule ikiitwa Sunderland) na Yanga, isifanyike.
Sakata lilianzia kwenye mechi ya Sunderland na African Sports ya Tanga iliyoisha kwa sare ya 1-1.
Baada ya mechi Sunderland walikata rufaa wakitaka wapewe alama za mezani kwa sababu Sports walimchezesha kipa ambaye hakuwa amesajiliwa.
Lakini Sports wakajitetea kwamba walipewa barua rasmi ya ruhusa na FATkumtumia kipa huyo.
Wao ndiyo walioomba ruhusa hiyo kwa sababu hawakuwa na kipa wa akiba.
Kipa wao namba moja alikuwa safarini na timu ya taifa, kipa namba mbili alikuwa mgonjwa wa macho.
FAT ya Balozi J. Majjid ikawaruhusu watafute kipa mwingine ndipo wakampata huyo ambaye Simba walimlalamikia.
Kutokana na kosa la FAT kuruhusu timu kumtumia mchezaji ambaye
hakusajiliwa, pamoja na makosa mengine mengi huko nyuma, serikali ikamuondoa madarakani Rais wa FAT, Balozi J. Majjid na ikaivunja FAT yote, kisha kuweka kamati ya muda.
2. ALI CHAMBUSO
Aliingia madarakani kama rais wa kamati ya muda iliyoshika madaraka baada ya kuondoka kwa Balozi J. Majjid, lakini baadaye akapitishwa moja kwa moja.
Utawala wake ukawa wa matatizo na kushuhudia kwa mara ya kwanza ligi kushindwa kumalizika mwaka 1970.
Chambuso alikuja na sheria ya kuruhusu timu za mashirika, makampuni na
taasisi kushiriki ligi.
Bahati mbaya sana ni kwamba wachezaji wa timu za mitaani kama Yanga na
Sunderland walikuwa wakifanya kazi huko.
Kwa hiyo timu zao zikishiriki ligi maana yake timu za mitaani zitakosa wachezaji kwa sababu watachezea timu za kazini kwao.
Yanga na Sunderland wakagoma kucheza ligi hii, na FAT ikaamua kuifuta kabisa mwaka huo.
Kufutwa kwa ligi kukasabisha kukosekana kwa mwakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika ya mwaka 1971.
FAT ya Chambuso ikachukua jina la Yanga ambao walikuwa mabingwa 1969, na kulipeleka CAF kama wawakilishi wa Tanzania.
Kwa kuwa walipelekwa jina lao CAF, Yanga wanahesabia kwamba wao ni mabingwa wa 1970, lakini kimsingi mwaka huo haukuwa na ligi.
Hata hivyo, utawala wa Chambuso ndiyo ulioleta ligi yenye sura ya Muungano, kuanzia mwaka 1972 pale timu za kutoka Zanzibar zilipoanza kushiriki ligi hiyo.
Mwaka 1973 akatolewa na serikali katika muendelezo wa maelewano mabaya na kuundwa kamati ya muda iliyotakiwa kuandaa uchaguzi utakaotoa viongozi wengine.
3. SAID EL MAAMRY
Kama kuna kiongozi alipitia misukosuko kwenye utawala wake, basi Said El Maamry.
Aliingia madarakani mwaka 1973, katika uchaguzi mkuu uliofanyika Tanga. Uchaguzi huu ulihudhuriwa na wajumbe kutoka Bara na visiwani, na ndiyo uchaguzi wa mwisho kwa Wazanzibari kuchagua kiongozi wa mpira wa Tanzania.
Mwaka 1976, El Maamry alitolewa madarakani na serikali kufuatia mahusiano yake mabaya na dola.
Waziri wa michezo, Murisho Sarakikya, alimteua katibu mkuu wa FAT, Hassan Dyamwale, kukaimu nafasi hiyo.
Bahati nzuri huo ulikuwa mwaka wa uchaguzi na akaruhusiwa kugombea akashinda na kurudi madarakani.
Lakini mwaka 1986, tena akiwa Mexico kwenye Kombe la Dunia lile la Maradona kufunga bao la mkono wa Mungu, jumuiya ya vijana ya CCM ambayo wakati huo ilikuwa inasimamia michezo, ikamtoa na kuunda kamati ya muda chini ya mwenyekiti Mbeyela na Katibu Leodeger Tenga.
Kisha jumuiya hiyo ikaitisha uchaguzi na mwenyekiti wake, Seif Khatibu, ambaye miaka ya mwanzo ya 2000 alikuwa waziri wa michezo na ndiye aliyesimamia ujenzi wa Uwanja wa Mkapa, akampiga marufuku El Maamry kugombea, ndiyo ukawa mwisho wake.
4. MOHAMED MUSSA
Uchaguzi ukafanyika mwaka 1987 na akapatikana mwenyekiti mpya wa FAT,
Mohamed Mussa.
Utawala wake ukaangushwa mwaka 1991, kwa vita vya ndani kwa ndani.
Novemba 30, 1991, timu ya taifa ya Tanzania Bara (jina la Kilimanjaro Stars lilikuwa halijaanza), ilifungwa 5-0 na Uganda Cranes, na kutolewa
kwenye mashindano ya CECAFA Challenge Cup.
Wakati huo mashindano haya yalikuwa na heshima kubwa sana.
Zambia, ambao ndiyo wakaja kuwa mabingwa, walimleta Kalusha Bwalya aliyekuwa
akicheza PSV ya Uholanzi.
Bwalya na Majjid Musisi wa Uganda, wakawa wafungaji bora wa mashindano, kwa mabao yao matatu kila mmoja, huku Musisi akiyapata kwa hat trick yake dhidi ya Tanzania Bara.
Baada ya kipigo hiki, Halmashauri Kuu ya FAT ilikutana Mwanza, mwezi Desemba na kuuondoa uongozi wa FAT chini ya Mwenyekiti Mohamed Mussa.
Halmashauri Kuu ya FAT kilikuwa chombo kilichoundwa na wenyeviti wa mikoa wa FAT, na ndicho kilichokuwa na nguvu, nyuma ya mkutano mkuu ambao ulihusisha pia na makatibu wakuu wa mikoa.
5. MUHIDIN NDOLANGA
Kuondoka kwa Mohamed Mussa na katibu kukampa nafasi Muhidin Ndolanga, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Arusha, kuchukua nafasi kwa muda.
Ndolanga akaanza kazi Januari 1992 na alitakiwa kuongoza kwa muda hadi 1993 utakapofanyika uchaguzi mkuu.
Na katika uchaguzi huo uliofanyika Kibaha, Ndolanga akashinda na kuendelea kuwa mwenyekiti.
Utawala wa Ndolanga nao ulikuwa wa misukosuko kama wa Said El Maamry.
Vita vya ndani ya chama na mahusiano mabaya na serikali vilikuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya utawala wake.
Picha inaanzia mwaka 1995 pale Ndolanga kama mwenyekiti wa FAT alipogomea kuchangia Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Alisema serikali haiwezi kuunda chombo halafu kikawategemea wadau kinachowasimamia.
Waziri aliyekuwa na dhamana ya michezo, Profesa Juma Kapuya, akachefukwa sana na ukaandaliwa mpango wa kumtoa.
Tofauti na viongozi wote waliotangulia, kwa Ndolanga serikali ilikutana na chuma cha pua.
Mwaka huo kulikuwa na uchaguzi na mwenyekiti wa BMT alikuwa Said El Maamry.
Itaendelea wiki ijayo.