Mzee wa Fact: Kuna filamu kuhusu maisha ya Simba, Azam

Leo ni siku ya Mzizima Dabi, Simba SC atawakaribisha matajiri wa Chamazi, Azam FC Uwanja wa Mkapa  kuanzia saa 10 jioni.

Huu ni mchezo wa 34 wa ligi baina ya timu hizi tangu zikutane kwa mara ya kwanza, Oktoba 15, 2008, kwenye Uwanja wa Uhuru.

Katika michezo 33 iliyopita, Simba inaongoza kwa kushinda michezo 13 huku Azam FC ikishinda 8.

Kuna mambo yanazungumzwa kuhusu mechi hii yakiwemo ya kweli na yasiyo ya kweli.

Katika makala hii, tutakuletea baadhi ya mambo hayo:

Jina Mzizima Dabi

Mechi hii inaitwa Dabi ya Mzizima kwa sababu ya historia ya timu hizi. Mzizima ni jina la zamani la kijiji ambacho baadaye kiligeuka kuwa mji wa Dar es Salaam. Lakini zaidi ya hiyo, Mzizima ni jina la ofisi kuu za zamani za Makampuni ya Bakhresa, eneo la Banda la Ngozi, jijini Dar es Salaam.

Mahali hapa kuna kıwanda kikuu cha kusaga ngano cha Bakhresa, na ndipo palipokuwa na ofisi kuu za tajiri Said Salim Bakhresa mwenyewe wakati akiifadhili klabu ya Simba miaka ya mwanzoni mwa 1980.

Mwaka 1982, Bakhresa akajitoa Simba na kuendelea na biashara zake hadi mwaka 2004 pale wafanyakazi wa kiwanda kile cha Mzizima walipoanzisha timu yao.

Timu hii iliyoanza kwa jina la Mzizima FC, iliendelea kuwa ya wafanyakazi hadi mwaka 2007 ilipochukuliwa na kiwanda na kuwa Azam FC kama inavyofahamika sasa.

Mahali ilipo sasa, yaani Chamazi, ilihamia mwaka 2010 lakini asili yake kabisa ni pale Mzizima.

Kupitia ofisi zake za Mzizima, tajiri Bakhresa aliifadhili Simba, na kupitia ofisi hizo hizo za Mzizima klabu ya Azam ilizaliwa.

Hii ina maana kwamba timu hizi mbili kuna wakati fulani ziliishi kwa kupata riziki yake kupitia Mzizima, ndiyo maana mechi baina yao ikawa Mzizima Derby.

2.Mechi za kukumbukwa

Tumeona huko juu kwamba Mzizima Dabi imefanyika mara 33 hapo kabla, kwenye ligi kuu. Japo asilimia kubwa ya mechi hizi zilijaa ubabe, undava na utemi, lakini kuna mechi tano muhimu ambazo zitabaki kwenye historia kwamba zilikuwa za kipekee, kabla, wakati na baada ya mchezo wenyewe.

I. Simba 0-2 Azam FC – 2008.

Hii ilikuwa mechi ya kwanza baina ya timu hizi kihistoria. Ilikuwa kwenye raundi ya saba ya msimu wa 2008/09, ambapo timu hizi ziliingia kwenye mchezo huu zikiwa na matokeo yasiyoridhisha, hasa kwa Simba.

Azam FC nao hawakuwa na matokeo mazuri lakini angalau unaweza kuwasamahe kwa sababu ndiyo walikuwa katika msimu wao wa kwanza, walikuwa wanajifunza.

Simba waliingia kwenye mchezo wakiwa wameshinda mechi tatu pekee katika sita zilizopita, mbili wakipoteza na moja sare.

Azam FC nao katika michezo yao sita iliyopita, walishinda miwili, wakafungwa mitatu na sare moja.

Kwa hiyo wakakutana Oktoba 15, kwenye Uwanja wa Uhuru na Azam FC kushinda 2-0 kwa mabao ya Jamal Simba Mnyate na Shekhan Rashid.

Matokeo ya mchezo siyo stori kubwa sana bali kilichotokea baada ya mchezo. Mashabiki wa Simba waliandamana kwa miguu kutoka uwanja wa uhuru hadi Magomeni, nyumbani kwa mwenyekiti wa klabu yao, Hassan Dalali, na kumtaka ajiuzulu.

Lakini haikuwa kiwepesi tu hivyo, walimshinikiza kwa mbinu chafu ya kumwaga kinyesi cha binadamu sehemu zote za nyumba yake.

Baada ya vinyesi kuzidi, Dalali akajiuzulu lakini siku iliyofuata akatengua uamuzi wake baada ya kuombwa na baadhi ya wanachama akarudi madarakani.

Hata hivyo, mechi hii haikupita salama iligharimu kazi ya kocha Krasmir Benzinski wa Simba na nafasi yake kuchukuliwa kwa muda na ‘super coach’ Silleyrsaid Mziray (marehemu).

II. Azam FC 0-3 Simba SC – 2009

Huu ulikuwa mchezo wa mzunguko wa pili na ulifanyika mara mbili kufuatia kuvunjika siku ya kwanza kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam.

Kwanza ulifanyika Machi 29, 2009 na kuvunjika, hivyo kurudiwa Machi 30, 2009 na Simba kushinda 3-0.

Crispin Odura wa Azam FC aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kwenye Dabi hii kuoneshwa kadi nyekundu siku hiyo.

Baada ya mchezo huu, kocha wa Azam FC, Neider Dos Santos, akasema hataki tena kuwatumia wachezaji waandamizi wa timu hiyo kwani walikuwa wakimsumbua.

Wachezaji hao ni pamoja na akina Shaaban Kisiga ‘Marlone’ na nahodha Shekhan Rashid. Akasema atawatumia vijana wa akademi kama Himid Mao na Tumba Lui.

Bahati mbaya kwake, akafukuzwa kazi siku iliyofuata. Nafasi yake ikachukuliwa Itamar Amorin, ambaye tutakuja kumuona huko mbele.

III. Azam FC 1-3 Simba – 2012

Ilikuwa Oktoba 27, 2012 Uwanja wa Taifa pale Azam FC, ilipokubali kichapo cha 3-1 kutoka Simba SC.

Baada ya mchezo huu Azam FC ikamfukuza kocha wake, Boris Bunjak, aliyedumu na timu hiyo kwa siku 80 tu.

Hata hivyo, siku chache baadaye ikazuka taarifa kwamba wachezaji wannę waandamizi waliihujumu timu hiyo.

Wachezaji hao walikuwa nahodha Aggrey Morris, kipa Deogratius Munishi ‘Dida, Erasto Nyoni na Said Morad.

Hapo ndipo John Bocco aliporithi kitambaa cha unahodha baada ya Aggrey kusimamishwa.

Shauri lao likapelekwa Takukuru na uchunguzi ukachukua takribani miezi sita. Na hakukutwa na hatia hivyo wakarudishwa kundini. Lakini kitambaa cha unahodha hakikurudi kwa Aggrey, hadi miaka sita baadaye.

IV. Simba 1-1 Azam FC – 2015

Hii ni moja ya mechi za kibabe zaidi kuwahí kuchezwa baina ya timu hizi. Ilifanyika Januari 24, 2015 kwenye Uwanja wa Taifa, sasa Mkapa.

Joto la mchezo lilianza kufukuta dakika chache kabla ya kuanza. Simba walitoa taarifa kwa Azam FC kutomtumia Amri Kiemba, mchezaji wa Simba aliyechukuliwa na Azam FC kwa mkopo kwenye dirisha dogo ambalo lilitoka kufungwa wiki moja kabla.

Wakati huyo Kiemba alikuwa ameshavaa jezi na alikuwemo kwenye kikosi kitakachoanza. Ukatokea mzozo baina ya timu hizi kwani Azam FC licha ya kumchukua Kiemba kwa mkopo, lakini walilipa ada ya mkopo huo hivyo waliamini kwamba angeruhusiwa kucheza.

Baada ya malumbano, Simba wakasema akivaa tu jezi na kuwepo hata benchi, watakata rufaa. Azam, FC wakaogopa na kumvua jezi Kiemba.

Naye akagoma na kuleta mtafaruku mkubwa. Kiemba alitaka kucheza mechi hiyo ili kuwakomesha waajiri wake wa zamani Simba, ambao walimtendea vibaya msimu huo hadi akalazimisha kuondoka, na kwenda Azam FC kwa mkopo.

Mchezo huu pia utakumbukwa zaidi kwa ubabe uliotawala baina ya wachezaji wa timu zote mbili kiasi cha Aggrey Morris wa Azam FC kumfanyia madhambi ya hatari Emmanuel Okwi wa Simba hadi akapoteza fahamu, akaenda kuzindukia hospitali.

V. Simba SC 3-1 Azam FC – 2019

Mchezo huu unaingia kwenye rekodi hii kwa kuwa uligharimu kazi ya benchi la ufundi la Azam FC chini ya Hans van der Pluijm. Ni moja ya michezo iliyotawaliwa na ubabe na utemi huku ufundi ukiwa kidogo sana.

Hans van der Pluijm akawa kocha wa tatu wa Azam FC kufukuzwa kazi baada ya kufungwa na Simba SC, na wa nne kwa jumla kwenye Mzizima Dabi.

Sajili la ajabu

Linapokuja suala la uhamisho, watu wengi hudhani ni rahisi tu kwa mchezaji kutoka Azam FC kwenda Simba au kinyume chake. Mifano huwa ni Patrice Mafisango mwaka 2011 na John Bocco na wenzake watatu mwaka 2017.

Lakini usidanganyike na hayo, hakuna uhamisho mgumu kama ule wa baina ya timu hizi mbili. Nikupe tu mfano, msimu uliopita wa usajili yaani dirisha kubwa la Agosti 2024, Simba SC walikataa kumtoa Aisha Manula kwa mkopo kwenda Azam FC ilhali wao hawamtumii.

Manula ni muendelezo wa masakata magumu ya usajili wa wachezaji baina ya timu hizi, kwa miaka na miaka. Ni rahisi kwa Yanga na Azam FC kubadilishana wachezaji, lakini siyo kwa Azam FC na Simba.

Mwaka 2015, timu hizi ziliingia kwenye vita kali ya kumwania winga teleza Ramadhan Singano.

Singano maarufu kama Messi ni mchezaji aliyekulia timu ya vijana ya Simba na kupandishwa timu kubwa msimu wa 2012/13.

Mwaka 2015, akaishitaki klabu yake kwa kamati ya sheria na hadhi za wachezaji akiilalamika kufoji mkataba na kuongeza mwaka mmoja zaidi kutoka miwili aliyosaini.

Simba wakapinga wakisema makubaliano yao yalikuwa miaka mitatu na ndivyo alivyosaini, kesi ikamkalia vibaya Singano kwa sababu Simba walikuwa na mkataba halisi yenye akiwa na maelezo tu ya mdomo.

Lakini hata hivyo, zikapigwa sarakasi na kesi ikabadilika juu kwa juu, kutoka malalamiko ya kufojiwa mkataba hadi stahiki kwamba Simba walimuahidi kumpa pesa za kupangia nyumba na bima ya afya, lakini hawakuwahi kumpa.

Hoja hiyo pia Simba wakaipangua wakisema walikuwa wakimpa kwa kumwekea kwenye mshahara wake. Na ukweli, kiwango cha mshahara walichokubaliana kilikuwa kidogo kulinganisha na alichokuwa akipokea, Simba wakasema kilichozidi ndiyo kilikuwa hela ya pango  na bima ya afya.

Lakini hakuna sehemu yoyote iliyoandikwa kuthibitisha madai hayo ya Simba, ikaamuriwa kwamba Simba walikiuka mkataba na Singano akahesabiwa kama mchezaji huru , akaenda Azam FC.

Hili liliwauma sana Simba na mwenyekiti wa kamati yao ya usajili, Zacharia Hans Poppe (marehemu), akaitisha mkutano na wanahabari pale basement Millenium Towers Makumbusho na kuwataka mashabiki wa klabu yao kususia bidhaa zote za Bakhresa.

Hata hivyo, Azam FC ni kama walikuwa wanalipa kisasi kwa Simba kwa walichokifanya miaka mitatu nyuma yake.

Simba SC waliwafanyia umafia wa kimyakimya Azam FC kwa kumchukua mchezaji wao Ramadhan Chombo ‘Redondo’, mwaka 2012.

Awali Redondo alitoka Simba SC kwenda Azam FC mwaka 2010, kama mchezaji huru  baada ya mkataba wake na Simba kuisha.

Akasaini mkataba wa miaka mitatu ambao ungemweka Azam FC hadi 2013, lakini baada ya miaka miwili, yaani mwaka 2012, akaibuka na kudai maktaba wake na Azam FC umeisha hivyo akasaini Simba.

Azam FC wakasisitiza kwamba mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja hivyo hawezi kuondoka.

Simba baada ya kugundua kwamba ni kweli Redondo alikuwa na mkataba na mambo yameshakuwa mengi, wakamtafuta kiongozi mmoja mkubwa serikalini ambaye ni mwanachama wao na kumuomba aongee na mzee Bakhresa ili Azam FC wamuachie mchezaji huyo.

Kiongozi yule akampiga simu na kumpa taarifa za uongo kwamba vijana wake wanataka kuwadhulumu Simba mchezaji.

Mzee Bakhresa alivyo hapendi migogoro na serikali, akawaamuru wanaye mara moja kuwaachia Simba huyo mchezaji ambaye hata yeye mwenyewe hakuwa akimjua.

Makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu, akaenda Mzizima, makao makuu ya kampuni, kuongea na viongozi wa Azam FC ili kulimaliza jambo hilo, ikawa hivyo.

Hii iliwauma sana Azam FC na ndipo wakalipa kisasi kwa Singano miaka michache baadaye.

Na suala la Azam FC ‘kuwakazia’ Simba kwa wachezaji halikuwa jambo geni. Mwaka 2011 vijana wawili walihitimu akademi ya Azam FC, Ibrahim Jeba (sasa marehemu) na Saimon Msuva.

Wakatolewa kwa mkopo ili wapate uzoefu na ukomavu. Jeba akaenda Villa Squad na Msuva akaenda Moro United.

Msimu ulipoisha wakatakiwa kurudi klabuni, lakini ‘wakuu’ Yanga na Simba wakavutiwa na vijana hao. Simba wakamchukua Jeba na Yanga wakamchukua Msuva.

Azam FC wakakataa Jeba kwenda Simba lakini wakamuacha Msuva kwenda Yanga. Hili lilileta mğogorö mkubwa sana kati ya Simba na Azam FC huku mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, akilumbana kwenye vyombo vya habari na Patrick Kahemele, aliyekuwa mratibu wa Azam FC.

Mwisho wa siku Simba wakakwama na Jeba akarudi klabuni, Msuva akaenda Yanga.

Usajili wa Mafisango

Nilisema kule juu kwamba watu humchukulia Mafisango kama mfano wa urahisi wa uhamisho wa wachezaji kutoka Azam FC kwenda Simba.

Na hii ni kutokana na uhamisho wake wa mkopo wa mwaka 2011 na mafanikio yake akiwa na Simba msimu wa 2011/12.

Lakini haikuwa rahisi hata kidogo. Mafisango licha ya ubora wake, ilikuwa lazima aondoke Azam FC kwa sababu alishageuka kirusi.

Mchezaji huyo aliyesainiwa na Azam FC mwaka 2010, akitokea APR ya Rwanda, alikuwa mtovu wa nidhamu kiasi cha kugharimu kazi ya kocha mkuu wa Azam FC, Itamar Amorim.

Azam FC ilienda Dodoma kucheza na Polisi ya huko (ambayo sasa ni Dodoma Jiji), na ratiba ya kurudi Dar es Salaam ilikuwa saa 12 asubuhi.

Ulipofika muda, wachezaji wote wakapanda basi, kasoro Mafisango, ambaye hata chumbani kwake hakuwepo.

Kocha akaamuru basi lisitoke hadi Mafisango atakapokuja. Akaja saa mbili asubuhi akiwa amelewa chakari.

Akaingia hotelini kuchukua begi lake na kuingia ndani ya basi la timu. Kocha akamtaka awaombe radhi wachezaji wenzake kwa kuwasubirisha muda wote huo, akakataa.

Timu iliporudi Dar es Salaam, kocha akawaambia viongozi wamuondoe Mafisango kwenye timu, nao wakakataa wakisema ni mchezaji mzuri na wamewekeza pesa nyingi kwake, kama alikosea basi aadhibiwe tu yaishe.

Kocha akasema ili amsamehe basi awaombe radhi wachezaji wenzake, bado Mafisango akakataa.

Kocha akasema kama Mafisango haondoki basi ataondoka yeye, viongozi wakasema sawa…kocha akaacha kazi.

Akaja kocha mpya, Mwingereza Stewart Hall, kutoka timu ya taifa ya Zanzibar. Naye baada ya muda mfupi akasema hamtaki Mafisango kwenye timu. Hapo sasa viongozi wakabidi wakubali kwamba ‘huyu jamaa ni tatizo’.

Kwa kuwa Hall alitokea timu ya taifa ya Zanzibar, alikuwa anamjua Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ na akataka afanye naye kazi Azam FC.

Mchezaji huyo alikuwa Simba, hivyo likuwa suala la mabadilishano ya mkopo kati yake na Mafisango.

Bocco na Aishi Manula

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Huu ni moja ya uhamisho ambao umewagharimu sana Azam FC kwenye macho ya wengi kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi au propaganda inayofanywa na wasioitakia mema klabu hiyo.

John Bocco, Aisha Manula, Shomary Kapombe na Erasto Nyoni, ni wachezaji walioenda Simba wakiwa huru baada ya mikataba yao na Azam FC kumalizika baada ya msimu wa 2016/17.

Mazungumzo ya mikataba mipya yalishindikana na wakaondoka. Mchezaji aliyemaliza mkataba hapangiwi kwa kwenda na klabu yake ya zamani…anachagua mwenyewe, na wachezaji hawa wakachagua kwenda Simba.

Jedwali la matokeo ya muda wote Mzizima Derby (ligi kuu)

TIMU              MP      W        D         L          GF       GA      PTS

Simba SC       33       13       12       8          44       32       51

Azam FC        33       8          12       13       32       44       36