
Msimu wa kumi wa Kombe la Shirikisho la CRDB upo kwenye hatua ya awali kabisa na tayari droo ya raundi ya 64 imefanyika juma lililopita.
Hii ndiyo raundi ambayo timu za ligi kuu zinaingia kwenye mashindano.
Mashindano haya ambayo yalianza 2015/16 yakiitwa Kombe la Shirikisho la Azam Sports, yamejipatia umaarufu mkubwa na yanazidi kuongeza mvuto.
Lakini maandalizi yake yamekuwa ya zima moto kila msimu, kila mashindano.
Huu ndiyo muda sahihi wa waandaaji wa mashindano kutafuta uwanja wa fainali ili kutoa muda kwa wenye uwanja kuandaa bila presha.
Hivi kwanini TFF inashindwa kutangaza mapema viwanja vya fainali?
Watangaze kabisa viwanja vitakavyotumika kwa nusu fainali na fainali ya msimu huu wa 2024/25 na 2025/26 na hata 2026/27.
Mikoa itakayoandaa mechi hizo ikijijua mapema, itafanya maandalizi mazuri ya uwanja na kufikia siku ya mechi uwanja unakuwa na hadhi inayostahili mashindano.
Kuchelewa kutangaza uwanja husabanisha mechi kuharibiwa na ubovu wa uwanja kiasi cha kusababisha makocha kutowaruhusu wachezaji wao kuwa huru sana na mpira.
Ukipata mpira piga mbele watu wagombanie, ukisema ukae nao unaweza kusababisha matatizo kwa sababu uwanja hauruhusu.
Unaweza kusema unataka kukokota mpira ukadunda kwenye moja ya vinundu vya uwanja, ukatoka kwenye himaya yako na kuhamia kwa wapinzani.
Sasa hilo likitokea karibu na lango lako si ni hatari hiyo?
TFF inapokaa na kuandaa mashindano haya, inayaandaa kwa kiwango cha chini sana, sijui ubunifu umefikia mwisho au hawataki kuelekezwa?
Utaratibu wa kupeleka mechi za mashindano haya kwenye viwanja mbalimbali ulianza kama utani mwaka 2017 pale TFF chini ya Jamal Malinzi ilipoipeleka fainali Dodoma.
Ilikuwa kama namna ya kutembea na upepo wa nchi kwani wakati ule upepo ulivumia Dodoma kutokana na Rais wa Awamu ya Tano John Pombe Magufuli kuhamishia serikali mjini humo.
Lakini mwaka uliofuata, 2018, nao ukawa wa zimamoto. Fainali ikatangazwa kupelekwa Arusha kwa tangazo la ghafla.
Alipoingia madarakani Wallace Karia ndiyo akaongeza na mechi za nusu fainali kufanyika kwenye uwanja utakaoteuliwa na mamlaka.
Siyo wazo baya hata kidogo lakini TFF inatakiwa kuwekeza kwenye hili.
Mikoa inayopata nafasi ya kuandaa mechi hizi iimeshindwa kufanya maandalizi yanayostahili ukubwa wa mchezo huu kutokana na kuwa na muda mchache.
Ukiacha uwanja wa mechi, mikoa yetu haina viwanja ambavyo vina hadhi ya timu kufanya mazoezi kabla ya mchezo.
Viwanja ambavyo timu hufanya mazoezi huko husababisha mazoezi kabla ya mechi yawe kituko.
TFF inatakiwa iliweke hili kwenye kanuni za mashindano kwamba mkoa utakaopata nafasi ya kuandaa mechi hizi, uhakikishe pia unaandaa viwanja viwili vizuri vya mazoezi kwa ajili ya wageni.
Kuicheza nusu fainali au fainali kwenye uwanja wa kubahatisha “kunapunguza utamu” wa mchezo kwa sababu wachezaji hawawezi kufunguka barabara.
Lengo la awali lilikuwa kupeleka mechi hizi kwenye viwanja ambavyo havijawahi kuona burudani ya soka la kiwango kama hicho kwa miaka mingi au hawajawahi kuona kabisa.
Siyo kitu kibaya lakini basi maandalizi yaboreshwe.
Tanzania tuna bahati kwamba tunao mtu aliyewekeza mabilioni ya pesa kwenye mpira wetu.
Ili kumlinda yeye na kuwavutia wengine, kanuni ya maandalizi lazima ihusishe moja kwa moja kwenye mambo ya miundombinu.