Mzee wa Fact: Chan 2024 iwe funzo kwa mashindano yetu ya ndani

Shirikisho la soka Afrika, CAF, limesogeza mbele fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani, CHAN, kutoka Februari hadi Agosti mwaka huu.

Fainali hizo zilizokuwa ziandaliwe na nchi tatu za Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya na Uganda, zimekwama kutokana na sababu kadhaa iliwemo kutokamilika kwa maandalizi ya wenyeji.

Taarifa ya CAF iliyotolewa Januari 14, 2025 ilisema fainali hizo

Wataalamu wa ufundi na miundombinu wa CAF ambao baadhi yao wameweka kambi Kenya, Tanzania na Uganda, wameishauri CAF kwamba muda zaidi unahitajika kuhakikisha kwamba miundombinu na nyenzo zote zinakuwa katika kiwango cha hadhi ya kuandaa mashindano yenye mafanikio.

Suala siyo viwanja vya mechi pekee kama ambavyo watu wanadhani, kuna viwanja vya mazoezi,  usafiri wa mashabiki, mahoteli, mahospitali na mambo mengine mengi yanayohitajika kwa mashindano ya aina hii.

Hili linapaswa kuwa somo kubwa kwa mamlaka zetu za soka hapa nchini zinapofikiria kuandaa matukio makubwa ya mpira.

Siyo tu waangalie uwanja wa mechi, hapana…kuna mengi sana ya kuangalia.

Sasa hivi kama nchi tumeamua kuwa na mfumo wa mashindano fulani katika kituo kimoja.

Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano na Kombe la Shirikisho la CRDB na hata Kombe la Mapinduzi.

Mashindano haya hufanyika katika kituo maalumu ambapo wenyeji huhangaika na maandalizi ya uwanja wa mechi tu, basi.

Hakuna anayejali upatikanaji wa hoteli za kutosha, achilia mbali ubora wake.

Hakuna anayejali upatikanaji wa kwanza viwanja vya mazoezi, achilia mbali ubora wake.

Tuchukulie mfano Kombe la Mapinduzi lililofanyika Pemba wiki iliyopita.

Pemba ni sehemu ambago ambayo haina sifa hata moja ya kuwa mji.

Hakuna sehemu za maana na za uhakika kuuza chakula. Waziri wa Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, ni shahidi.

Alilazimika kwenda kula chakula cha usiku kwenye kibanda cha mama ntilie, alipohudhuria moja ya mechi za mashindano hayo.

Hakukuwa na viwanja vya mazoezi zaidi ya uwanja wa mechi. Mara kadhaa timu zikigongana hapo kufanya mazoezi katika siku ambayo pia kuna mechi na kusababisha baadhi ya mechi kuchelewa kuanza.

Uwanja huo huo pia ulikuwa ukitumika kwa mazoezi ya gwaride la wanajeshi kuelekea sherehe za mapinduzi hivyo kufanya ratiba ya mazoezi ya timu kuwa ngumu sana.

Pemba hakuna hoteli wala nyumba za kutosha za kulala wageni.

Hakuna nyumba za kupangisha (apartments).

Ilibidi watu wapangishe nyumba zao za familia kwa wageni.

Unapanga chumba kitupu, halafu unakodi kitanda na godoro…hiyo ndo Pemba.

Sehemu ya starehe ni moja tu, inaitwa Mess, ambayo hadhi yake ni ya chini sana…saana!

Mungu bariki mashindano ya mwaka huu hayakuwa na watu wengi.

Ni maafisa wachache tu wa serikali, timu shiriki pamoja na kikosi cha luninga cha kuonesha mashindano hayo…lakini bado Pemba ilizidiwa.

Vipi kama lingekuja kundi kubwa la waandishi kutoka bara tu, kama ambavyo huwa pale Unguja?

Vipi kama lingekuja kundi kubwa la mashabiki kama ambavyo huwa Unguja?

Pemba ni mfano wa miji mingi ya Tanzania ambayo hupewa mzigo mzito wa kuandaa matukio mbalimbali ya michezo hasa soka.

Mamlaka huangalia kitu moja tu,  uwanja wa mechi, basi.

Hawajali timu zitafanya wapi mazoezi,  mashabiki watakaokuja watalala wapi, watastarehe wapi kabla na baada ya mechi na kadhalika.

CAF imetufundisha hilo na tulichukue kama somo kuanzia sasa.

Aprili kutakuwa na Kombe la Muungano. Popote litakapofanyika, somo la CAF lihusike.

Halafu zitakuja nusu fainali na baadaye fainali za Kombe la Shirikisho la CRDB…tulizingatie somo la CAF.

Tumekuwa tukisema kwamba kuna faida kubwa ya mashindano makubwa kama CHAN na baadaye AFCON kufanyika nchini kwetu.

Sasa moja ya faida hizo iwe hilo somo, siyo tu kusema, ‘watakuja wageni na tutaitangaza nchi yetu’.

Na pia tuangalie namna wenzetu wanavyoandaa matukio yao iliwemo thamani wanayotoa kwa wadao wao kama waandishi na wengine wengi.

CHAN iwe funzo…tujifunze ili tufanikiwe!