
KIUNGO wa Zed FC ya Misri, Maimuna Hamis ‘Mynaco’ amesema kufunga na kuzuia kwake ni kawaida sana ndio maana anasifika kwa jambo hilo.
Kiungo huyo wa zamani wa Simba Queens, Yanga Princess na JKT Queens huu ni msimu wake wa pili kuitumikia timu hiyo na amekuwa kiungo tegemeo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mynaco ambaye anaweza kumudu nafasi zote za kiungo alisema amekuwa akibadilishiwa majukumu kutegemeana na mechi husika hivyo anapocheza namba 10 hufunga au kutoa asisti na anaporudi chini hujitahidi kuzuia mashambulizi.
“Kwenye mpira kuna moments tatu, wakati una mpira, hauna mpira , kuutafuta mpira ili kuumiliki kwahiyo kama sina mpira nitazuia, na kama ninao nitashambulia,” alisema Mynaco.
Aliongeza kuwa Ligi ya Tanzania ilimkomaza kwani ligi ya Misri ina ushindani hivyo kama asingepata uzoefu WPL ingekuwa ngumu kutoboa nchini humo.
“Ligi ya Tanzania imenikomaza pakubwa sana yaani ni kama shina kwahiyo nisingeweza kusimama na kuhimili mikiki ya Ligi ya Misri ambayo ina ushindani mkubwa lakini bado tumeendelea kupambana.” Msimu uliopita nyota huyo alifunga mabao sita kwenye mechi 18, msimu huu tayari ameweka kambani mabao matatu na asisti sita kwenye mechi 12.