
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuwapa nafasi wanawake katika ngazi mbalimbali ili kufikia malengo ya usawa wa kijinsia, huku akiwataka kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Dk Mwinyi amesema hayo leo Machi 6, 2025 katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoambatana na uzinduzi wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na uzinduzi mpango wa kitaifa wa kupambana na udhalilishaji kwa wanawake na watoto hapa Zanzibar, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Nyamazi Unguja.
“Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kiuchumi kupitia sera na mipango mbalimbali ya uwezeshaji, hivyo itazidi kutoa kipaumbele na kufarijika kuona wanawake wengi wanagombea katika ngazi mbalimbali hasa vyombo vya kutoa uamuzi,” amesema.
Amesema dhamira ya kumuwezesha mwanamke ni kuhakikisha anashiriki kwenye uchumi, kumkomboa na kumlinda dhidi ya utegemezi.
Amesema kwa Zanzibar kuna wilaya 11 na mikoa mitano hivyo hakuna sababu nafasi hizo wakosekane wanawake, kwani wapo wenye uwezo na wanapopewa nafasi hizo wanaonyesha utendaji uliotukuka.
Hata hivyo, kwa sasa mkuu wa mkoa mwanamke ni mmoja kati ya mikoa mitano na wakuu wa wilaya ni wawili kati ya wilaya 11.
“Wanawake wamekuwa muhimili mkubwa katika mambo mbalimbali, kwa hiyo niwasihi mjitokeze kwa wingi kuwania nafasi hizo na sisi serikalini tutaendelea kuwapa nafasi mbalimbali za kiutendaji na uongozi,” amesema Dk Mwinyi.
“Kwa lengo la kuhakikisha dhamira hiyo inafanikiwa, naagiza Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na wizara inayoratibu masuala ya majukwaa, kwa kushirikiana na wizara ya Kazi Uchumi na uwekezaji, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Biashara na wadau wengine kuandaa utaratibu kuhuisha majukwaa hayo ili yalete matokeo,” amesema.
Rais Mwinyi amesema, kupitia ZEEA, wananchi 34,746 wamenufaika kati ya hao wanawake ni 17,811 sawa na asilimia 51.2 ya wanufaika wote.
Katika uwezeshwaji huo wa mikopo, Sh34.9 bilioni zimetolewa na ZEEA, kati ya hizo Sh21 bilioni sawa na asilimia 60 zimetolewa kwa wanawake.
Naye mlezi wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, ambaye pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema katika kufikia malengo ya majukwaa hayo lazima wanawake wote kuwa kitu kimoja.
Naye waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma amesema wizara imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ili kufikia malengo ya wanawake wote.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeda Rashid Abdallah licha ya kuonesha kuwa wanawake asilimia 52 na wanaume kuwa na asilimia 48 katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, bado wanawake wako nyuma katika mipango ya kisiasa, kiuchumi na kijamii hivyo wakati umefika kuendelea kumjali na kumthamini mwanamke ili kufikia maendeleo yake.