
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema dhamira ya Serikali kuanzisha hati fungani inayofuata misingi ya Kiislamu (Sukuk) ni kupata fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Februari 22, 2025 wakati akizindua rasmi hati fungani hiyo Ikulu Zanzibar.
Amesema utaratibu wa Serikali wa kibajeti kupata fedha ulikuwa hautoshelezi kulingana na mahitaji makubwa ya utekelezaji wa miradi.
“Serikali imepanga kutekeleza miradi mingi ya maendeleo, utaratibu tuliokuwa tunatumia wa kibajeti tumeona haukidhi matakwa yetu kwa hiyo tukaona tubadilishe mwelekeo wetu wa namna ya kupata fedha na ndio maana tukaja na mpango huu wa Sukuk,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema baada ya kushauriana kwa kina, Serikali ikaamua kuna utaratibu huo ambao unakuwa na wawekezaji mbalimbali, kampuni binafsi na wafanyabiashara au mtu mmoja mmoja, kwani kila mmoja anapata faida yake kulingana na atakachokiwekeza.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, hati fungani hiyo inayofuata misingi ya Sharia sio tu kwamba ni ya kwanza kwa Zanzibar bali kwa Afrika Mashariki, hivyo Zanzibar imeanza na nchi zingine zitafuata baada ya kuona mfano.
Hata hivyo, amesema mafanikio hayo yatafikiwa kutokana na ushirikiano wa watu wote kila mmoja kwa nafasi yake, kwani kinachopatikana ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi na mtu binafsi.
Katika hatua ya kwanza Serikali inatarajia kupata Sh1.1 trilioni ambazo zinalengwa katika kutekelaza miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege, terminal 4 na uwanja wa ndege Pemba.
Miradi mingine ni ujenzi wa barabara, maji, umeme, masoko, ujenzi wa meli za kisasa, hospitali, kujenga ukumbi wa mikutano, madaraja na bandari.
Katika hatua nyingine Dk Mwinyi amesema kuna kauli ambazo zinatolewa kwamba Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) inauzwa kutokana na kupokea fedha hizo akiwataka waache upotoshaji.
“Kuna mtu mmoja kutoka kwenye chama cha siasa kwamba tunaiuza benki ambayo ilianzishwa na Abeid Aman Karume, leo ni miaka 60 kwa hiyo lazima tubadilike,’
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema uanzishaji wa hati fungani hiyo utaiwezesha Serikali kuwa na uwanja mpana wa kupata fedha kwa ajili ya miradi badala ya kutegemea mikopo na vyanzo vingine.
Dk Saada amesema hawakuwa na namna nyingine lazima watafute njia mbadala ya kupata fedha kwa sababu ya wananchi walivyokuwa na hamu ya maendeleo.
“Hili jambo ni kubwa na tunaamini kwamba litakwenda kuleta matokeo chanya mbeleni,” amesema Dk Saada.
Ametaja miongoni mwa faida za kuwekeza katika hati fungani hiyo inayofuata misingi ya sharia na kumilikiwa na SMZ kwa asilimia 99 ni uwazi, kwani mtu anayewekeza anafahamu fedha zake alizowekeza zinakwenda kufanya jambo gani.
“Yule anayewekeza jambo linatangazwa (public) kwa umma tofauti na hatifungani nyingine, hazitangazwi, pia inatoa faida badala ya riba kulingana na uwekezaji uliofanywa na mtu, huku mwekezaji mwenyewe anakuwa hana wasiwasi kwani anapata umiliki,” amesema.
Faida nyingine itakayopatikana katika hatifungani hiyo inayodumu kwa miaka saba, kila baada ya miezi sita mwekezaji anapata faida ya asilimia 10.5.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Juma Malik Akil amesema hatua ya kuanzisha hatifungani hiyo ni baada ya kupata changamoto ya benki yenye masharti magumu ya mikopo.
Amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha wa wa 2024/25 walitarajia kukopa Sh1.7 trilioni na mpaka sasa ni benki moja ya PBZ ambayo imeamua kusaidia Dola za Marekani 50 milioni.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Yusra Sukuk Co Ltd ambao ndio washauri elekezi, Sheikh Mohamed Issa amesema kuna umuhimu wa kuwekeza katika hati fungani hiyo ambayo fedha zake zinakuwa salama zaidi ikilinganishwa na uwekezaji mwingine.