Mwili wa mwanafunzi aliyekufa kwa kuchapwa viboko haujazikwa, sababu yatajwa

Simiyu. Mwili wa marehemu, Mhoja Maduhu (18), aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwasamba iliyopo Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, bado haujazikwa kutokana na majadiliano kati ya familia na Serikali kuhusu gharama za mazishi.

Msichana huyo alifariki dunia Februari 26, 2025 baada ya kudaiwa kuchapwa viboko 10 na kukanyangwa kichwani na mwalimu wake, Salim Chogogwe, jambo lililosababisha kifo chake.

Mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza ulipopelekwa kwa ajili ya uchunguzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Sunday Songwe, amesema jeshi hilo bado linamshikilia mwalimu Chogogwe kwa mahojiano kuhusiana na kifo cha mwanafunzi huyo, kwa hatua zaidi za kisheria.

Akizungumza na Mwananchi leo, Alhamisi, Machi 6, 2025, baba mdogo wa marehemu, Samwel Maduhu, amesema wameshindwa kuzika mwili huo kutokana na mazungumzo yaliyokuwepo kati ya familia na Serikali kuhusu gharama za mazishi.

Amesema kulikuwa na mvutano kati yao na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega ili ibebe gharama zote za mazishi.

“Tumechelewa kufanya mazishi ya binti yetu kwa kuwa tulikuwa na mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Busega, tulivutana kwa kweli lakini ikafikia hatua tukakubaliana kuwa gharama zote za mazishi zibebwe na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega,” amesema.

Amesema wamefikia uamuzi huo kutokana na mazingira ya kifo cha mwanafunzi huyo kusababishwa na mwalimu ambaye ni mtumishi wa Serikali akiwa kwenye kituo chake cha kazi.

“Mazingira ya kifo yanaonyesha wazi kuwa aliyesababisha kifo alikuwa akitimiza majukumu yake, lakini akatoa adhabu nzito na kali kinyume na kanuni za utoaji adhabu ya viboko shuleni na pia mwalimu huyo ni mwajiriwa wa Serikali kupitia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega,” amefafanua.

Amesema kilichobakia sasa ni kuhakikisha waliyokubaliana yanatekelezwa na familia itakaa na kupanga siku ambayo maziko.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faiza Salim, aliyefika nyumbani kwao na marehemu akiongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo, amekabidhi mchele na fedha.

“Tumefika hapa nyumbani kwa lengo la kuwapa pole na pia kuanza kutimiza yale tuliyokubaliana ili mazishi yafanyike, tumeleta mchele kilo 250 na fedha Sh1.14 milioni zisaidie shughuli za hapa nyumbani, pia, gharama zote za kuufuata mwili katika hospitali ya Bugando zitagharamiwa na Serikali,” amesema.

Ameongeza kuwa wataendelea kubeba gharama nyingine zitakazojitokeza na lengo ni kuhakikisha shughuli ya mazishi inafanyika kwa amani na utulivu.